Trump afichua malipo kwa nyota wa filamu za ngono Stormy Daniels

Trump Stormy
Image caption Stormy Daniels

Rais wa Marekani Donald Trump alifichua rasmi kuwa alirejesha fedha kwa wakili wake baada ya kumlipa nyota wa filamu za ngono ili kumzuia kufichua uhusiano wao.

Ofisi ya Maadili ya Serikali ya Marekani iligundua Jumatano kuwa Trump huenda alifichua malipo hayo akitangaza matumizi ya fedha awali.

Matumizi hayo ya fedha yanaonyesha kuwa alimlipa Michael Cohen kwa matumizi ya fedha ya mwaka 2016 kati ya dola 100,001 na 250,000.

Malipo kwa Stormy Daniels yanaweza kuwa tatizo la kisheria kwa rais kwa sababu yanaweza kuonekana kama matumizi mabaya ya pesa za kampeni.

Awali Trump alikana kufahamu malipo ya dola 130,000 kwa Stormy Daniels.

Bwana Cohen, hata hivyo, amekubali kulipa zaidi ya dola laki moja na thelathini kwa nyota wa masuala ya ngono Stormy Daniels muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu wa Uraisi mnamo mwaka 2016.

Stormy anaeleza kuwa alilipwa kiasi hicho ili kumziba mdomo kuhusiana na kuwepo na tuhuma za uhusiano baina yake na bwana Trump na inajitokeza sasa kinyume na makubaliano ya awali.

Image caption Stormy anadai aliwahi kuwa na uhusiano na bwana Trump mnamo mwaka 2006 ,na walikutana katika hoteli ya Lake Tahoe

Mnamo mwezi Aprili, raisi Trump alisema hakumbuki kama bwana Cohen alikuwa amemlipa Bi Daniels kabla ya uchaguzi wa 2016. Malipo ya Trump kwa Cohen mara ya kwanza yalithibitishwa na Rudy Giuliani, ambaye ni mmoja wa mawakili wa rais katika mahojiano ya televisheni.

Bwana Giuliani anasema shughuli hiyo ilikuwa na kazi moja tu kumnyamazisha bi Daniels kuhusu "mashtaka ya uwongo na ya udanganyifu" kwamba alifanya ngono na Trump, lengo likiwa ni kumsafisha mgombea nafasi ya uraisi wa wakati huo ambaye sasa ni rais wa Marekani.

Baadaye wiki hiyo hiyo, Raisi alisema Bwana Giuliani alihitaji muda wa kukusanya taarifa za ukweli.

Mada zinazohusiana