Jasusi wa Urusi aliyewekewa sumu Uingereza aondoka hospitalini

Sergei Skripal in Moscow court. Photo: August 2006 Haki miliki ya picha Moscow District Military Court/TASS
Image caption Sergei Skripal

Aliyekuwa jasusi wa Urusi Sergei Skripal ameondoka hospitalini miezi miwili baada ya kuwekewa sumu ya neva huko Salisbury Uingereza.

Jasusi huyo wa umri wa miaka 66 alipatwa amezirai kwenye kiti tarehe 4 Machi pamoja na bintiye Yulia.

Walipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Salisbury.

Yulia Skripal aliruhusiwa kuondoka hospitalini tarehe 9 Aprili na kupelekwa eneo salama.

Mkurugenzi wa matibabu Lorna Wilkinson amesema kuwa kuwatibu wawili hao imekuwa changamoto kubwa.

DS Nick Bailey - afisa wa polisi ambaye aliwahudumia wawili hao siku waliwekewa sumu pia aye alitibiwa lakini aliondoka hospitalini.

Image caption Yulia na Sergei Skripal walitibiwa hospitali ya Salisbury

Serikali ya Uingereza iliilaumu Urusi kwa shambulizi hilo, huku waziri mkuu wa Uingereza Theresa May akilaani vikali kitendo hicho.

Lakini serikali ya Urusi imekana kuhusika na kuilaumu Uingereza kwa kubuni taarifa bandia.

Mwaka 2006 Skripal kanali wa zamani alifungwa nchini Urusi miaka 13 kwa kufichua siri kuhusu majasusi wa Urusi barani Ulaya.

Lakini mwaka 2010 alikuwa mmoja wa wafungwa waliobadilishwa kati ya Urusi na Uingereza.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wachunguzi

Wakati wa uchunguzi maeneo kadha ya Salisbury yalifungwa wachunguzi wakijaribu kubaini ni wapi wawili hao waliwekewa sumu.

Kiwango kikubwa zaidi cha sumu hiyo kilipatika kwenye mlango wa mbele wa nyumba yao.

Oparesheni ya mamilioni ya pesa kusafisha eneo hilo inaendelea. Sehemu mbili walizozuru waili hao bado zinatajwa kuwa hatari sana.

Mada zinazohusiana