Ndoa ya mke uji: Najuta kufunga ndoa Ramadhani ikiwa karibu

  • Esther Namuhisa
  • BBC Swahili
Ndoa ya mke uji uleta majuto kwa wengi
Maelezo ya picha,

Ndoa ya mke uji uleta majuto kwa wengi,ingawa ndoa ni thawabu kwa Mwenyezi Mungu

Mwezi mtukufu wa Ramadhani unatajwa kuwa ni mwezi wenye neema ambapo, familia hujumuika kwa pamoja katika swala na chakula.

Waislamu wengi nchini Tanzania hutumia muda huo kujiandaa kwa kujitakasa kiroho.

Viongozi wa dini hiyo wanasisitiza kuwa mambo muhimu ya kuzingatia katika kipindi hiki ni kuwa wasafi wa kiroho na kimwili na kumrudia Mwenyezi Mungu.

Ni mafundisho haya ambayo husababisha watu wengi ambao wapo katika mahusiano ya nje ya ndoa kufunga ndoa.

Hata hivyo, wingi wa ndoa zinazofanyika katika msimu huu wa mfungo, baadhi zimekuwa na historia ya kukosa uimara, hivyo kupewa au kubandikwa jina la 'ndoa ya mke uji'.

Maelezo ya picha,

Marium Migomba ,Mshehereshaji na mtoa mafunzo kwa mabinti kabla ya kuolewa

Mariam Migomba ni mshehereshaji na mtaalamu anayewafundisha wasichana kabla hawajaolewa.

Anasema muda mfupi kabla ya Ramadhani wasichana huwa wanafika kwake kupata mafunzo ya jinsi ya kukaa na mume lakini mafunzo yanakuwa hayasaidii kwa kuwa lengo la baadhi yao huwa sio upendo wa dhati.

Wakati ambapo wengi wanasheherekea ndoa, wengine wanajuta kwa uamuzi waliochukua katika kipindi cha msimu kama huu.

Maelezo ya video,

Migomba: Usiwe na pupa na papara kujiingiza katika ndoa

Msichana mmoja mwenye umri wa miaka 24 ambaye kwa sasa anafanya kazi katika baa, ambaye tutamuita Mwanahamisi* (hakutaka jina lake litajwe) ni miongoni mwa wanaojuta.

Anasema alifunga ndoa mwaka jana kabla ya Ramadhani na baada ya mwezi huo, mume alimdanganya kuwa anasafiri na kushangaa mpaka leo hajarudi.

Dada huyo anasema kabla hajaolewa alikuwa anafanya kazi kwenye hoteli na alivyofunga ndoa ikambidi aache kazi hiyo ili amuhudumie mumewe.

Mwanahamisi anasema harusi hiyo haikuwa na neema hata kidogo maana mume wake alimtelekeza katika chumba walichokuwa wanakaa. Kodi ilimwishia na kwao ni mkoani Kigoma.

Maelezo ya picha,

Wasichana wakiwa wamejipamba kwa ajili ya sherehe

Wazazi wake hawakuwa na taarifa ya ndoa yao kutokana na mwanaume huyo kudai kwamba wafunge ndoa kwanza sababu mwezi mtukufu umekaribia na baadaye watajipanga vizuri wafanye sherehe ya kupeleka na mahari rasmi.

Lakini matokeo yake, sherehe haikufanyika na baadaye kuambulia kukimbiwa na meme na kubaki bila kazi wala hela za kujikimu.

Isitoshe, alijikuta na mimba. Hali iliyomfanya ashindwe kurudi katika kazi yake ya awali.

Maelezo ya sauti,

Kwanini ndoa zakithiri wakati Ramadhani?

Kwa sasa hafurahii kufanya kazi ya kuuza vinywaji baa kwa madai kwamba kazi hiyo ina udhalilishaji, licha ya kulazimika kuifanya kwa ajili ya kupata fedha za kujikimu yeye na mtoto wake ajae, ingawa sehemu anayofanya kazi, hawafahamu kama ni mjamzito.

Mke uji huwa ni maamuzi ya haraka

Maelezo ya picha,

Harusi iliyofanyika siku chache kabla ya Ramadhan

Bi Chiku ambaye ni mkazi wa Buguruni, anasema haikuwa muda mrefu tangu alipopata mwanamme waliyependana ambaye alikuwa Mkristo.

Wakati wakiwa bado wako kwenye uhusiano, ulipofika mwezi Shaaban, yaani mwezi unaotangulia Ramadhani, ilimbidi akatae kuendelea na mahusiano hayo kwa sababu ya kipindi cha Ramadhani kilikuwa kinakaribia.

"Hakuwa na ugumu wowote kuoana. Mimi yule mtu wangu na Ramadhani hauruhusiwi kuwa unafunga na hawara, hairuhusiwi kupewa hela na hawara, hairuhusiwi kununuliwa futari na hawara," anasema.

"Yeye hizo huduma ilikuwa ni lazima anipe na nikaona haina haja kutengana kutokana na Ramadhani… hivyo tukaamua kufunga ndoa."

Siku mbili tu kabla ya Ramadhani, mwanamme huyo aliridhia kubadilisha dini na kuwa Muislamu na ndoa yao haikuwa ya gharama yeyote kwa sababu ilikuwa ni ndoa ya ghafla.

Kwa maana haikuwa na tarumbeta bali ilikuwa ya ubani, shehe na ndugu wote waliifahamu.

Chiku anasema wakati wameanza kufunga, kumi la kwanza, mume wake alikuwa anajaribu kwenda msikitini na viongozi wa dini walikuwa karibu naye kumfundisha.

Ila walivyoingia kumi la pili na la tatu, hapo ndipo visa vilipoanza na ndoa ikawa kama geresha.

"Maana mara nyingi tukimaliza kufuturu kuna ile swala ya saa mbili ya Ishaa, na baadaye kufuatiwa na swala ya Tarawekh, na baadae watu hukesha msikitini maarufu kukaa itikafu,"anaeleza.

"Lakini sasa yeye baada ya kukesha msikitini akawa anaenda kulala kwa mwanamke mwingine wakati huo wa mwezi mtukufu.

"Nilikuwa napewa taarifa na mashekhe huku wakihoji kwanini halali msikitini? Wakati huo huo, nyumbani pia halali, lakini wazazi wakawa wanasema nivumilie maana yeye ni mgeni katika dini,"Chiku anafafanua.

Maelezo ya picha,

Ramadhani

Chiku anasema, ndoa yake ilifikia tamati siku ya Iddi pili, baada ya mashekhe kualikwa wazungumze naye na mwanamme huyo akachukizwa na kitendo hicho na kutoa talaka.

Ndoa hizi zenye umaarufu wa jina la 'mke uji' haziwaathiri wanawake pekee.

Maelezo ya picha,

Wanaume pia huathirika ndoa za mke uji

Hata wanaume pia hukumbwa na changamoto kama hiyo.

Bw Matibwa ambaye ni mkazi wa Msasani anasema yeye hakutaka kuoa kwa ajili ya kuchekesha watu.

Alikuwa na nia thabiti ya kuongeza mke wa pili, maana alikuwa hataki kufanya zinaa na alitaka kumrudia Mwenyezi Mungu.

Ila baada ya kuoa tu, anasema alipata mtihani wa kukosa ajira na alipomwambia mke mpya, hali ikaanza kuwa ngumu kwa upande wake, hivyo kuvunjika kwa ndoa hiyo kabla hata ya miezi sita.

Bw Matibwa anasema kuwa tukio lile lilimuumiza sana, ingawa mpaka sasa yuko na mke wa kwanza ambaye walikuwa wameshazoeana kwa raha na shida.

Bwana huyo anasema, hivi karibuni uchungu wa kumpoteza mke wake wa pili umemrudia maana ameolewa tena Ijumaa iliyopita na ndoa imekuwa kipindi hicho hicho cha Ramadhani.

"Bado ninampenda mke wangu wa pili mpaka kesho licha ya kwamba inabidi nikubali kwa sasa kwa kuwa ameolewa.

Lakini tatizo kubwa ni maadili tu na siku hizi hamna wazee wa kutusuluhisha," anaongeza kusema.