Chanjo ya majaribio ya Ebola yaanza kutolewa DRC

Chanjo hiyo ilitumika kwanza kwa kiasi fulani wakati wa janga la Ebola Afrika magharibi kati ya mwaka 2014- 2016 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Chanjo hiyo ilitumika kwanza kwa kiasi fulani wakati wa janga la Ebola Afrika magharibi kati ya mwaka 2014- 2016

Maafisa wa Shirika la afya Duniani (WHO) na Serikali ya Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo leo wameanzisha mpango wa kutoa chanjo ya majaribio dhidi ya ugonjwa wa Ebola ili kudhibiti kusambaa zaidi kwa virusi vya ugonjwa huo.

WHO linasema limewatambua zaidi ya watu 500 ambao huenda wamekaribiana na waathiriwa wa ugonjwa wa Ebola nchini Congo.

Watakuwa miongoni mwa watu wa kwanza watakaopewa chanjo hiyo ya majiribio.

Awamu ya kwanza ya chanjo hiyo ya majaribio iliwasili nchini Congo siku ya Jumatano.

Kumekuwa na milipuko mitatu ya Ebola nchini DRC tangu janga la mwaka 2014-2016 katika Afrika ya magharibi.

Dalili za Ebola

  • Dalili za Ebola ni homa, kufuja damu na kuharibika kwa mfumo mkuu wa neva.
  • Maafa ya ugonjwa huu huweza kufika asilimia tisini - lakini mzuko wa hivi punde unasababisha maafa 55% .
  • Ugonjwa huo huchukua muda wa siku ishirini na moja kukomaa.
  • Hakuna kinga wala tiba
  • Huduma za msaada na kudhibiti kupoteza maji mwilini kutokana na kuharisha au kutapika husaidia katika kupona
  • Inafikiriwa kuwa popo ndio hubeba virusi vya ugonjwa huo.

Ufanisi wa Chanjo ya Ebola

Uchunguzi uliofanyiwa chanjo ya ugonjwa wa Ebola umebaini kuwa inaweza kumkinga mtu kutokana na virusi vya ugonjwa huo kwa takriban mwaka mmoja.

Utafiti huo uliochapiswa katika jarida la New England Journal of Medicine, ulifanyiwa nchini Liberia na kuwashirikisha wagonjwa 1,500.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ugonjwa wa Ebola uliwaua zaidi ya watu 11,000 nchini Liberia, Sierra Leone na Guinea, kati ya mwaka 2014-2015.

Wale waliopewa chanjo hiyo walifanikiwa kupata kinga yenye nguvu kwa karibu mwaka mmoja.

Majaribio hayo yanaonyesha kuwa chanjo hizo zote zinaweza kutumiwa kuokoa maisha wakati wa majanga ya ugonjwa wa Ebola siku za usoni.

Ugonjwa wa Ebola uliwaua zaidi ya watu 11,000 nchini Liberia, Sierra Leone na Guinea, wakati wa mlipuko wa ugonjwa huo mwaka 2014-2015.

Tunafahamu nini kuhusu dawa inayotumiwa?

Chanjo hiyo iliyotengenezwa na kampuni ya Merck bado haijapewa kibali, lakini ilifanikiwa katika majaribio kiasi wakati wa janga la Ebola Afrika magharibi.

Dkt Michel Yao, kutoka WHO, ameiambia BBC kwamba chanjo hiyo imefanyiwa majaribio nchini Guinea na kwamba "takriban watu wote waliopewa chanjo hiyo hawawezi kupata ugonjwa huo".

WHO limetuma zaidi ya dosi 4,000 za chanjo hiyo kwa Jmahuri ya Kidemokrasi ya Congo, huku fungu jengine la dosi ya ugonjwa huo likitarajiwa kutumwa hivi karibuni.

Maafisa wa afya na wanaosimamia kuzikwa kwa maiti za waathiriwa ni miongoni mwa watakaotangulia kupewa chanjo hiyo , kabla ya mpango mzima kuenezwa kwa zaidi ya watu 500 ambao huendna wakawa wamewakaribia waathirwa wa ugonjwa huo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii