Mtoto wa kwanza azaliwa kisiwani Brazil baada ya miaka 12

Fernando de Noronha island, Brazil. File photo

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Fernando de Noronha kina baadhi ya fukwe za kuvutia zaidi duniani

Kisiwa kimoja nchini Brazil ambapo ni marufuku kwa mwanamke kujifungua kinasherehekea mtoto wa kwanza kuzaliwa humo katika kipindi cha miaka 12.

Kisiwa cha Fernando de Noronha kinachopatikana 370km (maili 230) kutoka mjini Natal, kina wakazi takriban 3,000 lakini hakika hospitali za kujifungulia waja wazito.

Wanawake wanaotaka kujifungua hutakiwa kusafiri bara.

Mwanamke ambaye hakutana jina lake litajwe alijaliwa msichana Jumamosi kisiwani humo.

Anasema hakufahamu kwamba alikuwa mja mzito na kwamba alipigwa na butwaa.

Mshangao

Mwanamke huyo anaaminika kuwa na miaka 22.

"Ijumaa usiku nilianza kuhisi maumivu na nilipokwenda kwenye bafu nitagundua kitu kikitoka kupitia miguu yangu," amenukuliwa na tovuti ya O Globo.

"Ni wakati huo ambapo babake mtoto alifika na kumchukua mtoto huyo. Alikuwa mtoto, msichana. Nilipigwa na butwaa."

Mtoto huyo alichukuliwa na kupelekwa hospitalini baadaye.

Maafisa wa serikali eneo hilo wamethibitisha kisa hicho.

"Mamake mtoto, ambaye hataki jina lake lifichuliwe, alianza kupatwa na uchungu wa kuzaa akiwa nyumbani," taarifa ya serikali inasema, kwa mujibu wa O Globo.

"Familia hiyo inasema haikufahamu kuhusu mimba ya mwanamke huyo."

Ili kusherehekea kisa hicho nadra cha kuzaliwa kwa mtoto kisiwani, wakazi wanaisaidia familia hiyo, na kuwapa nguo za kuvaliwa na mtoto huyo, ripoti zinasema.

Fernando de Noronha ni kisiwa ambacho kina baadhi ya fukwe maridadi zaidi duniani na ni maarufu kwa hifadhi ya viumbe wa baharini.

Kisiwa hicho hupatikana eneo la hifadhi ya bahari na idadi ya watu imekuwa ikidhibitiwa kwa muda kisiwani humo.