Kituo kinachotoa hifadhi kwa watoto wa wazazi walio gerezani Tanzania

  • Esther Namuhisa
  • BBC Swahili
Nyumba ya kulea watoto walioko gerezani
Maelezo ya picha,

Nyumba inayolea watoto waliozaliwa gerezani

Kwa kawaida vituo maalum vya kuwalea watoto nchini Tanzania huwa vina watoto ambao ni yatima au walemavu.

Lakini katika nyumba ya mtakatifu Gabriel iliyoko mkoani Arusha nchini Tanzania, ni kituo maalum cha kulea watoto ambao mama zao wanatumikia kifungo gerezani .

Maisha huko ni sawa na yale ya shule ya bweni, na ukifika katika kituo hicho utaona picha nyingi za watoto pamoja na ratiba maalum ya wiki inayoelekeza mambo gani wanapaswa kufanya wanapoamka mpaka wanapokwenda kulala.Mwisho wa ratiba hiyo kuna sentensi yenye herufi kubwa inayosema 'Kutabasamu ni Lazima'.

Kituo hiki chenye watoto 25 kilichoanza mwaka 2003, kinahudumiwa na sister aliyetunukiwa tuzo ya wanawake wenye mafanikio nchini Tanzania mwaka wa 2018.

Chanzo cha picha, Sista Flora

Maelezo ya picha,

Sista Flora alitunuikiwa tuzo ya mwanamke mwenye mafanikio kwa mwaka 2018 kwa kuweza kuwatunza watoto waliozaliwa gerezani

Lakini watoto wanaoishi katika kituo hicho walifikaje hapo na maisha ya namna hiyo wanayaonaje?

Maisha yanafananaje ukizaliwa gerezani

Maelezo ya picha,

"Sikuwa najua wazazi wangu walipo mpaka nilipofika darasa la saba,kuna wakati nilihisi labda wamekufa ," Sophia anaeleza

"Ninaulizwa maswali mengi na wenzangu kwamba inakuwaje na mama sista, kwani mimi ni yatima lakini mara zote nakwepa kuwapa jibu sahihi na kubaki kutafakari na kutamani kuwa na wazazi kama watoto wengine," Anneth anaeleza.

Aneth anasema alifikishwa katika kituo hicho mwaka 2009 baada ya wazazi wake wote wawili kufungwa kwa kosa la mauaji, jambo ambalo lilimshangaza kwa nini wazazi wake wote wawili walitekeleza mauaji hayo.

Prisca ni msichana wa kidato cha tatu anayenuia kuwa wakili hapo baadae. Anasema anasoma kwa bidii ili amsaidia mama yake atakapotoka gerezani.

James, mwenye miaka 14, anasema hakumbuki ni lini alifika katika kituo cha Gema.

La kusikitisha zaidi hamjui baba yake lakini wakati yuko darasa la tano mwaka 2015, mama yake aliwahi kumtembelea lakini hakumchukua na alimwambia asome kwa bidii maana yeye hana uwezo wa kumtunza bado.

David, ambaye alikuwa pamoja na mama yake, anasema anafuraha sana kwa kuwa sasa anamuona mama yake kila wakati lakini upendo alioupata katika kituo cha Gema ulimwezesha kuishi kwa amani na furaha.Mpaka sasa kituo hicho kinamsomesha.

Makuzi ya watoto gerezani yakoje?

Maelezo ya video,

Catherine Malle: Aliwahi kufungwa gerezani na mtoto

Catherine Malle ni mama yake David ambaye anasema kipindi anaingia gerezani mwaka 2005 kwa kupatikana na kosa la kumpiga mtoto wa kambo mwenye umri wa miaka saba yeye alikuwa na watoto wake mwenyewe wawili; mmoja mwenye umri wa miaka mitatu na mwingine alikuwa ni David mwenye umri wa mwaka mmoja.

Anasema hawezi kusahau siku hiyo alivyokamatwa na akaenda na mtoto wake mdogo polisi na yule mwenye miaka mitatu akamuacha kwa jirani kwa kutegemea kuwa atarudi lakini mwisho wa siku akahukumiwa kifungo cha miaka mitano.

" Kufungwa gerezani ni mtihani mkubwa sana kwa wanawake kwa sababu jela ni sawa na kufa ingawa mara nyingine katika jamii tunashindwa kuzifahamu sheria sawasawa. Mama ukifungwa gerezani ni watoto ndio wanateseka zaidi bila hatia," Catherine aeleza.

Aidha anasema lugha ya gerezani huwa sio nzuri na changamoto huwa ni wafungwa wenyewe kwa wenyewe mara nyingi wanachanganyikiwa kwa upweke wa muda mrefu licha ya upendo wa askari wa gerezani.

``Kwa kweli inaniuma sana kuona mtoto wangu anasikia matusi makubwa makubwa na hakuna namna maana humo kuna watu wamechanganyikiwa kutokana na kesi walizokumbana nazo, malezi ya mtoto kwenye gereza ni magumu sana kuna wakati unahitajika kwenda shambani hivyo inabidi utafute rafiki mahabusu aweze kukuangalizia mtoto wako, Catherine aeleza."

Sista Flora Ndatwa anawaleaje watoto wa wafungwa

Maelezo ya picha,

Malezi kwa watoto hawa ni tofauti hivyo huwa wanahitaji ushauri wa saikolojia kila wakati

Sister Flora anasema wazo hilo la kuwalea watoto waliopo gerezani walilipata wakati walipokuwa wanawatembelea mama walioko magerezani na kukuta wakiishi na watoto wao katika mazingira ambayo si salama kwa makuzi ya watoto.

Na walipowauliza mbona wako hapo na watoto,hudai kuwa wapo nao maana hawana mtu wa kumuachia au ananyonyesha.

Hivyo tukaona vyema kuanzisha kituo na kuwachukua watoto wakiwa na miaka miwili na akiwa chini ya miaka miwili atachukuliwa kama mzazi ataomba sana na kuna sababu maalum.

Safari ya kufika hapo alipo haikuwa rahisi na anasema ilimuhitaji kuandika barua nyingi za miradi ili aweze kupata ufadhili,jambo ambalo anashukuru Mungu sana maana ofisi za serikali ya mkoa wa Arusha, Tanapa pamoja na ufadhili kutoka nje ya nchi wameweza kumsaidia sana.

Lakini vilevile sister Flora anasema haamini katika kuwa na kituo cha kulea watoto kwa kutegemea msaada tu hivyo wamefanikiwa kuwa na shule ya msingi ambayo ina watoto 550 ambao wanafanya vizuri sana mpaka wamepewa tuzo kutoka wizara ya elimu mwaka jana.

Maelezo ya picha,

Shule ya msingi inayomilikiwa na kituo cha Mtakatifu Gabriel

''Changamoto za kifedha zipo lakini lazima tujitahidi na hata pale tunapoomba msaada watu waone tumefanya nini na tunahitaji nini.Watoto saba wako sekondari na wameenda kusoma shule binafsi ili wapate elimu bora, basi kuku wanaofuga na bustani inasaidia kujikimu."

Sista anakutana na changamoto gani?

Sista anasema kimalezi watoto hawa wanakuwa tofauti na watoto wengine.

"Wengi huwa wameathirika kisaikolojia kutokana na tabia mbalimbali walizoziona gerezani,maana mara nyingine unakuta unamuita mtoto anakuja alafu anachuchumaa na kusema nimekuja meja,najaribu kuwaelewesha kuwa mimi sio meja na wanakuwa hawaoni shida kutumia maneno yasiyofaa."

Changamoto nyingine ni pale ambapo wazazi wao wanapotoka gerezani wanakuwa hawaji kuwachukua watoto wao na sababu kubwa ni kutokuwa na uwezo wa kuwahudumia kutokana na kukaa gerezani muda mrefu, hivyo watoto wanakuwa wametelekezwa kabisa na tunakosa majibu ya kueleza wako wapi maana gerezani hawapo tena wakati walikuwa wamezoea kwenda kuwaona kila mwezi.

Maswali mengi kutoka kwa watoto ni miongoni mwa changamoto na mara nyingi sista anasema huwa anakosa kutoa jibu ambalo si sahihi sana maana hawezi kusema mama yako aliua au alifanya kosa lipi.

''Kwa nini mama yangu anavaa nguo ya bluu kila siku na wengine wanavaa ya njano na wengine za kawaida,'' ni swali tunaloulizwa na watoto mara kwa mara.

''Kwa kawaida huwa tunawadanganya lakini baadae wanajua huo ni uongo, na wanaumia sana hasa anapojua sare ya mama yake inamaanisha ni kifungo cha maisha."

Licha ya changamoto hizo, sista anasema watoto hawa ni wa kipekee na wanasoma kwa uchungu sana ili waweze kusaidia jamii.

''Wazazi wao huwa wanafarijika sana kwa huduma ambayo tunawapa na wanashukuru.Wanasema ndugu wasingeweza kuwalea watoto wao kama wanavyowalea kwenye kituo".

Je,malezi ya gereza si salama?

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Gerezani sio sehemu salama kwa malezi ya watoto,watu wanapaswa kutovunja sheria

Mkuu wa gereza la Arusha, Ramadhani Mkele, anasema huko ndani kuna watoto wanaingia na mama zao na kuna ambao wanajifungua humo wakiwa mahabusu au gerezani.

Kamanda anasema gerezani sio sehemu salama kwa malezi ya mtoto licha ya jitihada zao kuwapa malezi bora wafungwa hao.

Kulingana na wakuu wa gereza hilo, mtoto anaweza kuishi mama yake gerezani mpaka akiwa na miaka saba ambapo anapaswa kuanza shule hivyo ustawi wa jamii pia huwa wanasaidia.

Watoto walioko na miaka mitatu au minne huwa wanaanza chekechea wakiwa gerezani.

''Ni faraja kwa upande wa Arusha kwa kuwa na kituo hicho karibu, maana wazazi huwa wanakataa hata ndugu zao wasiwachukue watoto na chaguo lao ni watoto kuchukuliwa na sista," kamanda Mkele anaeleza.

''Sisi huwa tunatoa ruhusa maalum kwa watoto hawa kuendelea kuja kuwaona wazazi wao na kila baada ya miezi mitatu huwa tunajumuika pamoja.

''Ni utaratibu ambao unaleta matumaini hata kwa wafungwa wenyewe.

''Gereza limeweka utaratibu maalum kisheria namna ambavyo watoto wanapaswa kukaa ndani na mama zao.Lakini gereza sio sehemu sahihi ya kukuuza mtoto. Kanuni ya sheria ya mtoto ya 20 inasema lazima kuwe na makazi maalum ya mtoto.

Watu wanapaswa kujua sheria na kuzifuata na kuepuka kutenda makosa."

Athari za watoto wanaozaliwa magerezani

Mtaalam wa saikolojia kutoka Wellness Tanzania anasema mara nyingi mazingira huwa yanajenga tabia ya mtoto yeyote anapokua.

Mwanasaikolojia huyo anasema watoto wa miaka miwili huwa hawaelewi kinachoendelea gerezani. Hivyo basi wakitoka nje mlezi anatakiwa acheze na akili zao ili wasione tofauti ya maisha gerezani na nje.

Ingawa watoto huwa wanatabia ya kuuliza kama wataona kuna tofauti, mlezi anafaa kuwaeleza maisha yote ni sawa.

Umri wa kutambua mambo vizuri huwa ni miaka mitano mpaka sita.

Lakini watoto pia huwa wanatofautiana,Unaweza kumuona mtoto wa miaka miwili ni mwerevu zaidi ya mtoto mwingine wa umri huo huo.

Kuna ambao wana kumbukumbu kubwa, haswa kama alishuhudia jambo ambalo sio la kawaida.

Aidha kukaa kwenye kituo maalum ni sawa na mazingira ya shule za bweni ambazo zinawafanya wengi watambue vile ambavyo hawapaswi kutambua.

Mwisho wa siku wanaathirika katika makuzi kama hawatakuwa na uangalizi mzuri.