Ramadhan: Mataifa ambayo Waislamu watafunga muda mrefu zaidi

Young Muslim praying

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Greenland Waislamu watafunga saa 22

Waislamu wanaendelea na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, moja ya nguzo tano kuu katika dini ya Kiislamu.

Kutokana na tofauti katika macheo na machweo, Waislamu watafunga kwa vipindi tofauti mataifa mbalimbali duniani.

Watakaofunga muda mrefu zaidi ni wale walio mataifa ya kaskazini mwa dunia.

Greenland Waislamu watafunga kwa saa 22 na Iceland na Urusi saa 20.

Nchini Uingereza, mfungo utadumu saa 19.

Afrika Mashariki, Waislamu kwa wastani watafunga saa 13 kwa siku.

Ramadhan ni nini?

Ramadhan ni moja ya nguzo tano kuu katika dini ya Kiislamu.

Mwezi huo, Waislamu hujifunga kula na kunywa kuanzia macheo hadi machweo.

Kufunga wakati huu huwawezesha Waislamu kujitolea zaidi katika dini na kumkaribia Allah.

Kando na kufunga, ni wakati pia wa kutafakari kiroho, kuswali, kutenda matendo mema na kujumuika na familia na marafiki.

Waislamu hufanya juhudi za kipekee kuungana na wengine katika jamii na kuwasaidia wale wanaohitaji usaidizi katika jamii.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Tende mara nyingi huliwa wakati wa iftar

Huwa ni kawaida kwa Waislamu kula chakula asubuhi kabla ya mawio, suhur, na jioni wakati wa kufungua baada ya jua kutua, ambacho hufahamika kama iftar.

Mwisho wa kufunga, baada ya machweo, familia na marafiki hujumuika pamoja kufungua.

Wengi pia huenda Msikitini kuswali.

Kwa ni mfungo ni sasa?

Ramadhan imekuwa mwezi huu kwa sababu ndio wakati Koran tukufu ilipofichuliwa kwa mara ya kwanza kwa Mtume Muhammad.

Ramadhan huwa ni mwezi wa tisa katika kalenda ya Kiislamu, lakini tarehe hiyo hubadilika kila mwaka.

Hii ni kwa sababu dini ya Kiislamu hufuata kalenda inayotumia mzunguko wa mwezi, hivyo hubadilika tofauti na kalenda inayotumiwa na mataifa ya Magharibi inayofuata jua.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Iftar msikitini

Ni kila mtu hufunga?

Si kila Mwislamu hufunga wakati wa Ramadhan.

Watoto, wanawake waja wazito, wazee na wagonjwa au wanaosafiri wameruhusiwa kutofunga wakati wa mwezi huu mtukufu.

Watoto hutakiwa kuanza kufunga punde wanapobalehe, ambapo kawaida huwa ni wakiwa na miaka 14.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wasichana wa Kiislamu wakionesha mikono yao iliyopambwa kwa henna baada ya maombi ya Eid Al-Fitr

Mtu mzima anaweza kufidia siki ambazo hakufungwa wakati wowote katika mwaka au kulipa fidyah, ambapo mtu hutoa msaada wa chakula au pesa kwa kipindi ambacho hakufunga.

Mwisho wa mwezi wa ramadhan, ambao mwaka huu utakuwa 14 Juni, au karibu na hapo, huwa kuna maadhimisho ya siku tatu ya sikukuu ya Eid al-Fitr.