Wapiga kura waidhinisha marekebisho ya katiba Burundi

Rais Nkurunziza amepiga kura yake kituoni ECOFO Buye, tarafani Mwumba, Mkoa wa Ngozi
Maelezo ya picha,

Rais Nkurunziza akipiga kura yake Buye, tarafani Mwumba, Mkoa wa Ngozi Alhamisi

Tume ya Uchaguzi nchini Burundi imetangaza kwamba kambi iliyokuwa inaunga mkono marekebisho ya katiba nchini humo imeshinda kura ya maamuzi iliyofanyika wiki iliyopita.

Hatua hiyo inampa Rais Pierre Nkurunziza nafasi ya kuongoza taifa hilo hadi mwaka 2034.

Matokeo ya muda yaliyotolewa na tume hiyo yanaonesha waliokuwa wanaunga mkono marekebisho hayo walikuwa 73.6%.

Waliokuwa wanapinga walikuwa19.3% ilhali kura 4.1% ziliharibika.

Asilimia 3.2 ya wapiga kura hawakuunga mkono upande wowote.

Wapiga kura zaidi ya 98% ya waliojiandikisha kuwa wapiga kura nchini humo hawakushiriki shughuli hiyo ya Alhamisi.

Rais wa Burundi walikuwa wanaamua iwapo muda wa muhula wa rais uongezwe kutoka miaka mitano hadi miaka saba.

Marekebisho ya sasa ya katiba yanamruhusu Nkurunziza kuwania uchaguzi wa mwaka 2020 na anaweza kuwania kwa mihula mingine miwili chini ya katiba mpya, kwani kuhesabiwa kwa mihula kutaanza tena baada ya mwaka huo.

Aliwania kwa muhula wa tatu mwaka 2015 hatua iliyozua utata na kusababisha msururu wa ghasia na jaribio la mapinduzi ya serikali.

Mzozo wa kisiasa wa wakati huo ulisababisha watu zaidi ya 400,000 kuikimbia nchi hiyo, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Kiongozi wa upinzani nchini humo Agathon Rwasa alikuwa awali ametangaza kuwa hatokubali matokeo ambayo yangetangazwa akitaja kuwa kura hiyo iligubikwa na udanganyifu mkubwa na vitisho kwa wafuasi wake.

BwRwasa aliitaka tume ya uchaguzi kufutilia mbali matokeo na kuitisha kura mpya.

Akizungumza na BBC kwa njia ya simu, kiongozi huyo wa upinzani anasema wafuasi wake walifanyiwa vitisho na vitimbi kuanzia kampeni hadi siku ya uchaguzi .