Bomoa bomoa Rwanda kutafuta makaburi ya halaiki

Bomoa Bomoa Rwanda
Maelezo ya picha,

Nyumba zaidi zinabomolewa Rwanda ili kutafuta makaburi ya halaiki

Nyumba kadhaa zimelengwa katika ubomoaji nchini Rwanda wakati maafisa wanatafuta makaburi ya halaiki mwezi mmoja baada ya makaburi mengine kugunduliwa ya watu waliouawa katika mauaji ya kimbari mnamo mwaka 94 huko Kabuga nje ya mji mkuu Kigali.

Wahusika wa shughuli ya kufukua masalio ya miili ya watu waliouawa wanasema kwamba tayari wameshafukua masalia ya watu zaidi ya 400 na kwamba mashimo zaidi yanapatikana kila uchao.

Sasa nyumba hizo zimelengwa kwa ubomoaji ili kutafuta mashimo zaidi.

Inakadiriwa kwamba takriban watu 7000 walizikwa katika makaburi ya halaiki nchini.

Wakuu wa kitengo cha kupambana dhidi ya mauaji ya kimbari wanasema watawafidia wamiliki wa nyumba ambapo hakuna masalio ya miili ya watu yatakayopatikana baada ya ubomoaji.

Katika kitongoji cha Kabuga - kaskazini mashariki mwa jiji la Kigali, wananchi wanafukua makaburi ya pamoja kutafuta masalia ya miili ya watu waliouawa katika mauaji ya kimbari mwaka 94.

Maelezo ya picha,

Masalio hayo yanakusanywa kando katika nyumba moja.

Masalio hayo yanakusanywa kando katika nyumba moja.

Nyumba nyingi zimeshabomolewa baada ya watu kushuku kuwa zilijengwa juu ya makaburi ya pamoja.

''Sasa tufanye nini? tumeshajua kwamba nyumba yetu ilijengwa juu ya masalia ya miili ya watu, eti tukatae nyumba isibomolewe ili miili hiyo itafutwe?'' anasema mmoja wa wanawake aliyekuwa anafungasha virago vyake kuondoka.

Wengine wameishia katika njia panda wasijue pa kuelekea.

''Tulipajenga hapa kabla ya Mauaji ya Kimbari. Je tulipachimba shimo tena na kuzika miili ya watu? Ingekuwa vizuri wakabomoa nyumba wanazoshuku kwamba kulizikwa watu. Viongozi tumewafahamisha kwa sababu nimemuuliza babangu akaniambia kwamba nyumba zote hizi alizijenga kwa mpigo mwaka 1987.'' Anasema mwanamke mwingine mkaazi wa kitongoji cha Kabuga.

Maelezo ya sauti,

Mashamba ya Rwanda yameshambuliwa na viwavi jeshi.

Mkuu wa kata ya Kabuga Nyiraneza Phillomene anafuatilia siku hadi siku shughuli za kufukua, anasema nyumba zote wanazoshuku kuwa na makaburi ya pamoja hakuna budi zibomolewe.

''Kwa vyovyote vile haya masalio ya miili ya watu waliouawa katika Genocide, yana thamani ya kiutu kuliko hizi nyumba zilizopo hapa.

Huu ni uamuzi kutoka ngazi za juu, unavyoona ni kwamba pia kuna mashine ya katapila, si kwamba imekuja kutoka ngazi ya kata!''

Mkuu wa jumuiya inayotetea maslahi ya manusura wa mauaji ya kimbari ameiambia BBC kwamba wameshafukua miili ya watu zaidi ya 400 na kwamba mashimo ya pamoja tisa zaidi yalipatikana mnamo wiki iliyopita.

Ameeleza kwamba shughuli ya kufukua bado inaendelea kiasi kwamba wanazidi kupata mashimo zaidi mlimozikwa watu ambayo hata hayakufikiriwa.

''Watu walimwagiwa tindikali na chumvi ili mifupa iharibike haraka kama njia ya kupoteza ushahidi.

Maelezo ya picha,

Mifupa midogo sana na nywele zimepatikana baada ya baadhi ya mashimo kufukuliwa

Tunapofukua tunapata mifupa midogo midogo sana, na nywele. Watu wengine walikatwa katwa kama nyama za ng'ombe. Pia tindikali iliteketeza kabisa mifupa ya vichwa kiasi kwamba ni vigumu kutambua kichwa kimoja'' alisema mkuu wa jumuiya inayotetea maslahi ya manusura wa mauaji ya kimbari.

Nguo zilizochanika na kupatikana ndani ya makaburi hayo ya pamoja ndiyo ishara pekee inayotumiwa na watu kutambua jamaa zao kutokana na kwamba inachukua muda nguo kuharibika.

Shughuli hii ya kufukua makaburi haya ya pamoja huenda ikachukua muda mrefu kufuatia ukubwa wa maeneo yanayokisiwa kwamba kulizikwa watu mwaka 1994.