Kwa nini ni vigumu kuiga mtindo wa uchezaji ngoma wa Michael Jackson

Michael Jackson's antigravity tilt

Chanzo cha picha, Manjul Tripathi

Wataalam wa upasuaji kwenye ubongo na uti wa mgongo wameeleza kwa undani ni kwa namna gani marehemu Michael Jackson alivyofanikiwa katika kucheza miondoko yake iliyoonekana kuwa isiyowezekana katika video yake ya 'Smooth Criminal'.

Katika mitindo yake ya 1987, Michael anainama kuanzia kwenye vifundo vya miguu, nyuzi 45 huku akiuweka mwili wake wima kama ubao.

Mtindo huu ambao wengi wamejaribu kuuiga, umefanyika kutokana na uwepo wa viatu maalum na nguvu kwenye ya uti wa mgongo wake.

Wataalamu wa tiba ya uti wa mgongo wamewatahadharisha watu wanaojaribu miondoko hii inayoelezwa kuwa ya hatari, kwamba wanaweza kuumia wakifanya hivyo.

Manjul Tripathi na wenzake kutoka taasisi ya tiba na utafiti Chandigarh, India, wanasema kwenye jarida la Neurosurgery ''wanenguaji wengi waliofundishwa wenye uti wa mgongo ulio na nguvu huweza kuinama kuanzia nyuzi 25 mpaka 30 wakiinamia mbele wakati wakicheza miondoko hiyo. Michael Jackson alifikisha mpaka nyuzi 45 uchezaji ambao haukuwa wa kawaida kwa yeyote aliyekuwa akishuhudia

Michael Jackson aliwezaje?

Ikiwa mtu atataka kujaribu miondoko ya kuinama kama ile ya kwenye wimbo wa Smooth Criminal, atagundua kuwa shinikizo zaidi linakuwa kwenye kano kuu nyuma ya vifundo vya mguu, badala ya kwenye uti wa mgongo.

"Hii inaruhusu mtu kuinama mpaka nyuzi kadhaa iwapo utainamia mbele, hata kwa mtu mwenye uwezo na nguvu za kufanana na Michael, " anaeleza Profesa Tripathi.

Chanzo cha picha, RUBEN RAMOS

Michael aliweza kuinama zaidi kuliko uwezo wa kawaida kwa sababu viatu vilikuwa vikimsaidia

Mkato wa umbo la 'V' kwenye visigino vya viatu vyake na wachezaji ngoma wake ambavyo viliingia kwenye misumali yenye nguvu sana ilivyokuwa imepigiliwa kwenye sakafu ilimwezesha yeye na wacheza ngoma wake kufanikisha uchezaji huo wa kipekee.

Kabla ya kutumia viatu vya aina hiyo, Michael alikuwa akitegemea nyaya zilizokuwa zikipitishwa kiunoni ili kuwaaminisha watu kuwa mtindo wake ni halisi.

Inaelezwa kuwa yeye na wasanii wenzake wa Hollywood waliazima wazo la viatu kutoka kwa wana anga wa nchini Marekani, ambavyo vilikuwa vikiwekwa kwenye reli wakati hakuna nguvu zozote za uvutano.

Pamoja na viatu hivyo kutengenezwa maalum kwa ajili ya kuwezesha minenguo hiyo, bado ni vigumu kufanikisha kwa kuwa nguvu zinahitajika hasa kwenye uti wa mgongo na misuli ya miguu, wameeleza madaktari.

''Mashabiki wa Michael Jackson, wamejaribu kuiga mtindo huu wakashindwa, mara nyingi wamekuwa wakipata majeraha'' walitahadharisha.

Daktari Tripathi amesema ''uwezekano wa kujeruhi vifundo vya mguu ni mkubwa.Unahitaji kuwa na misuli yenye nguvu na msaada kwenye vifundo vya mguu.''Si kazi rahisi''