Watafiti: Kwa nini unafaa kula angalau yai moja kwa siku

eggs

Chanzo cha picha, Getty Images

Utafiti ambao uliwashirikisha watu laki tano nchini China unadokeza kwamba kula yai moja kwa siku kunaweza kusaidia kupunguza hatari ya kupata maradhi ya moyo na kiharusi.

Wataalamu wanasisitiza kwamba ni lazima mtu ale mayai kwa njia ifaayo, na mtu awe anakula lishe bora yenye afya, ndipo aweze kupata manufaa hayo.

Lakini bado wasiwasi kwamba ulaji wa mayai mengi unaweza kudhuru afya ya binadamu kwa sasa unaonekana kupungua.

"Mtu anaweza kufikiria zaidi kuhusu tahadhari ambazo zimekuwa zikitolewa na wataalamu wa lishe, lakini kilichobainika kutoka kwa utafiti huu wa China ni kwamba kula angalau yai moja kwa siku hakuongezi hatari ya kuugua maradhi ya moyo, na badala yake kuna faida," anasema Prof Nita Forouhi, wa Chuo Kikuu cha Cambridge.

Utafiti huo, ambao matokeo yake yamechapishwa katika jarida la masuala ya moyo la Heart, ulifanywa baada ya miaka mingi ya watu kuonyesha dhidi ya ulaji mayai.

Watu walikuwa wakitahadharishwa kwamba kula mayai kunaweza kuwasababisha kuambukizwa viini vya salmonella na pia kwamba yana kiwango cha juu cha cholesterol.

Mayai mangapi bora?

Siku hizi, wengi wa madaktari huwa hawashauri watu kutokula mayai, kwani ni miongoni mwa vyakula vyenye virutubisho na madini mengi zaidi ya manufaa kwa mwili.

Yana protini ya kiwango cha juu pamoja na Vitamini A, D, B na B12, na pia madini ya lutein na zeaxanthin ambayo yanaweza kuzuia mtu kupata matatizo ya macho atakapozeeka.

"Moja - hata mawili - kwa siku ni sawa kabisa," anasema Dkt Frankie Phillips, kutoka kwa Chama cha wataalamu wa Lishe Uingereza.

"Watu hawafai kuwa na wasiwasi wa kula mayai mengi."

Dkt Phillips anasema onyo pekee watu wanafaa kuzingatia ni kwamba kula chakula cha aina moja pekee kwa wingi kuna maana kwamba "watu wanakosa madini na virutubisho ambayo hupatikana kutoka kwa vyakula vingine."

Chanzo cha picha, PA

Na ingawa mayai yana protini, Dkt Phillips anasema kawaida mwili hupata protini za kutosha kutoka kwa vyakula vingine, na kula protini kupindukia kunaweza "kuwa mzigo kwa figo".

Wakfu wa Moyo Uingereza (BHF) uliondoa ushauri wake wa kuwataka watu wasile mayai zaidi ya matatu kwa wiki mwaka 2007 kutokana na kutokea kwa utafiti mpya kuhusu cholesterol.

Cholesterol

Kwa mujibu wa ushauri wa Huduma ya Taifa ya Afya Uingereza (NHS), "ingawa mayai yana cholesterol, kiwango cha mafuta kutoka kwa mafuta na vyakula vingine tunavyovila huathiri zaidi kiwango cha chorestrol kwenye damu kuliko kinavyoathirika kutokana na ulaji wa mayai."

Kimsingi, mayai sio chanzo cha matatizo ya kuwepo na kiwango cha juu cha chorestrol kwenye damu. Ni mafuta tunayoyatumia.

Kwa mujibu wa Heart UK, yai la kawaida (58g; 2oz) huwa na mafuta 4.6g. Lakini ni robo pekee ya mafuta hayo huwa mafuta mabaya, yaani yale yanayoongeza kiwango cha chorestrol.

Siagi na jibini hali ni tofauti.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mayai yanavyotumiwa huwa na manufaa kwa mwili

Yapikweje?

Kwa kuangazia jinsi tunavyopika mayai, mayai ya kuchemshwa ndiyo bora zaidi.

Wataalamu wengi wa lishe hupinga kukaangwa kwa mayai kwa sababu mara nyingi mafuta hutumiwa na hivyo kiwango cha cholesterol anachokula mtu huongezeka.

Mayai mabichi au yalivyopikwa kidogo tu pia ni sawa, mradi tu yawe yalitokana kwenye mazingira safi.

Mayai yaliyopikwa ndiyo njia bora zaidi ya kujikinga na maambukizi.

Usinunue mayai ambayo yamevunjika kwani yanaweza kuwa yameingia uchafu au bakteria.

Wengi bado wanakumbuka jinsi ya kutumia maji kwenye bakuli kubaini iwapo yai limeharibika au la.

Iwapo litazama, ni bora na lisipozama limeharibika.

Chanzo cha picha, Reuters

Mayai mengi huwa katika kiwango kizuri kwa siku 28 tangu yanapotagwa.