Mafia: Kisiwa cha Tanzania ambapo kuoa wake wengi ni kawaida

Bwana Khasim na wake zake, Nuru na Khadija
Maelezo ya picha,

Bwana Khasim na wake zake, Nuru na Khadija

Je wajua kuwa katika ndoa za mitala upo uwezekano mume kuishi na wake zake hata watatu katika Nyumba moja?

Katika maeneo mengi ya pwani ya Afrika mashariki, ndoa hizo zimeshamiri, Sababu kuu ikiwa suala la dini na utamaduni wa maeneo ya pwani, huku katika maeneo mengine likibaki kuwa mjadala mkali hasa kwa wanawake.

Katika kisiwa cha Mafia mkoa wa pwani nchini Tanzania ndoa za mitala zimejaa karibu kila Nyumba, jambo ambalo husababisha wake wenza kukaa nyumba moja.

Kutokana na hali hii kuwa ya kawaida katika kisiwa hiki cha Mafia, niliweza kuzungumza na watu kadhaa, ambao wana wake zaidi ya mmoja.

Mmoja wao aliyenivuta zaidi ni bwana Ally Khasim, ana wake wawili ambao wanaishi katika Nyumba moja lakini vyumba tofauti, na hawajawahi kuwa na mgogoro wowote kati yao, jambo ambalo si mara nyingi hutokea.

Maelezo ya picha,

Ndoa za mitala zimeshamiri hasa maeneo ya pwani ya Tanzania

Mke mkubwa anaitwa khadija, na wa pili anaitwa Nuru, khadija anasema kuwa hakukubaliana na uamuzi wa mume wake wa kuongeza mke wa pili lakini baada ya kumshawishi akaona ni jambo la kawaida, na kwa upande wa Nuru mke wa pili alikubali kuingia katika ndoa ya wake wengi kwa hiari yake.

Ndoa hiyo ya bwana Khasim na wake zake imedumu kwa miaka 14 bila migogoro na ugomvi baina ya wake zake , jambo ambalo ni nadra.

''hawajawahi kugombana kwa lolote lile labda mikwaruzano ya kawaida baina yangu mimi na mmoja kati yao, ambapo ni jambo la kawaida baina ya mume na mke'' anasema khasim

Nilipomuuliza Nuru , mke mdogo kuwa alitarajia kukutana na mikasa ya uke wenza, alinambia kuwa mwanzoni alidhani angekutana nayo lakini akakuta hali ni tofauti.

''Mwanzoni nilitarajia kuwa nitakutana na visa, lakini nashukuru sana baada ya kukaa na mke mwenzangu kwa muda hatujawahi kugombana tunafanya kila kitu kwa ushirikiano'' anasema Nuru.

Naye mke mkubwa, bi Khadija anasema kuwa yeye hana matatizo yoyote na alipokuja mke mdogo na yeye hakua na matatizo hivyo wamekua wakiishi kwa amani na upendo katika ndoa yao.

Nilimuuliza pia bwana Khasim kama anatarajia kuongeza mke wa tatu, akanambia akiwa sawa kiuchumi basi ataongeza, na wake zake wanakubali kumkaribisha kukaa naye kama huyo mke wa tatu atakua mpole na mtulivu kama wao.

Kwa bwana Khasim, wake zake na watu wengine wa pwani suala la ndoa za mitala si ajabu, ni sehemu ya maisha yao, lakini mbali na dini niliambiwa pia suala la chakula lina mchango mkubwa wao kuoa wake wengi kutokana na kula samaki wa aina mbalimbali ambao wao wanaamini inawaongezea nguvu za kiume.

''mi nakubali kabisa sisi tunapenda kuoa wake wengi, mimi nina wake wawili na ukiachana na dini sisi watu wa pwani bwana, tunakula vyakula vya kuleta nguvu mke mmoja pekee hatoshi, kwani ana mambo mengi, anaweza akajifungua akaa miezi mitatu minne, sasa sisi uvumilivu huo hatuna ndio mana tunaoa wanawake hata watatu na tunataka utulivu pia'' anasema Khamis Saburi mkazi wa kisiwa cha Jobondo, Mafia.

Mbali na mitazamo hiyo wapo wachache ambao hawana mpango wa kuongeza mke, kama bwana Ally Njenge,

''kama huwezi kuridhika na mke mmoja basi ni hulka yako tuu, mi nina mke mmoja na siwezi kuongeza mwingine, kwanza ni kujiongezea gharama lakini pia matatizo tuu kwanini usiridhike na huyo mmoja?

Katika maeneo mengine ya bara, bado suala hilo lina mjadala mkali, huku wanawake hawataki kusikia kabisa kuolewa uke wenza.