Rwanda yawa mmoja wa wadhamini wa Arsenal kuvumisha utalii wake

Arsenal kutangaza utalii wa Rwanda
Maelezo ya picha,

Arsenal kutangaza utalii wa Rwanda

Rwanda imetangaza mpango wa ushirikiano na timu ya Arsenal inayocheza ligi kuu ya England.Ushirikiano huo wa miaka 3 unalenga kuimarisha sekta ya utalii nchini Rwanda,uwekezaji na maendeleo ya mchezo wa soka.

Kwa mujibu wa mapatano hayo,Rwanda itakuwa mshirika rasmi wa Arsenal wa sekta ya utalii Kwa kipindi cha miaka 3 kuanzia msimu ujao , fulana za timu ya Arsenal mkono wa kushoto zitakuwa na nembo yenye maneno ya 'visit Rwanda' au ''Tembelea Rwanda''.

Hii itahusu timu ya kwanza,timu ya wachezaji walio chini ya umri wa miaka 23 na timu za wanawake.Pia imetangazwa kwamba maneno hayo ya Tembelea Rwanda yatakuwa yakionekana kwenye mabango maalum ya kibiasara ndani ya uwanja wa Emerates wakati wa mechi za Arsenal.

Mkataba huo ulisainiwa Jumanne baina ya klabu ya Arsenal na mamlaka ya maenedeleo ya Rwanda kupitia kitengo chake kinachohusika na utalii na maendeleo

Haikutangazwa ni kitita kiasi gani cha pesa ambacho Rwanda imetoa ili kutangazwa kwenye jezi za Arsenal.

Ruka Twitter ujumbe, 1

Mwisho wa Twitter ujumbe, 1

Afisa wa Arsenal anayehusika na biashara Vinai Venkatesham amekaribisha ushirikiano huo aliotaja kuwa wa kusisimua kushirikiana na nchi ya Rwanda kutokana na kasi yake ya maendeleo na pia kuunga mkono nia ya Rwanda ya kujenga sekta yake ya utalii.

Afisa huyo amesema shati ya Arsenal inaonekana mara milioni 35 kwa siku duniani kote na ni moja ya timu zinazoonekana zaidi ulimwenguni.

Arsenal inasema wachezaji wake wa timu za wanaume na wanawake watazuru Rwanda pamoja na mameneja kuandaa mafunzo ya mpira kwa lengo la kusaidia maendeleo ya soka nchini Rwanda.

Kwa mujibu wa Benki ya dunia, Rwanda ni ya pili kwa urahisi wa kufanya biashara barani Afrika na imetambulika kwa uongozi wake katika masuala ya utalii na ushindani, tuzo iliyotolewa na Baraza la dunia la utalii na pia katika mkutano wa kimataifa wa kiuchumi.

Sekta ya utalii ni ya kwanza kuingiza fedha katika hazina ya serikali.Kulingana na mamlaka ya maendeleo ya Rwanda ,mwaka jana watalii wapatao milioni 1.3 walizuru mbuga tatu za wanyama zilizoko nchini humo ikiwemo mbuga mashuhuri ya Volcano inayohifadhi Sokwe.