Korea Kaskazini yabomoa eneo la kujaribia silaha za nyuklia

Punggye-r site in North Korea, 23 May 2018
Maelezo ya picha,

Picha ya eneo la kufanyia majaribio silaha za nyuklia Korea Kaskazini la Punggye-ri kabla ya kuharibiwa

Korea Kaskazini imeharibu mashimo yaliyo katika eneo pekee la majaribio ya silaha za nyuklia, ili kupunguza taharuki kati yake na Korea Kusini na Marekani.

Waandishi wa habari wa kimataifa katika eneo la majaribio ya silaha za nyuklia la Punggye-ri lililo kaskazini mashariki walishuhudia mlipuko mkubwa.

Pyongyang ilitangaza kusitisha shughuli zake za nyuklia mwanzoni mwa mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kidiplomasia kati yake, Korea Kusini na Marekani.

Kilitokea nini siku ya Alhamisi

Mashimo matatu yalilipuliwa mbele ya wanahabari wa kimataifa takribani 20.

Milipuko miwili ilitokea asubuhi na mingine minne nyakati za jioni.

Mwanahabari wa Sky News Tom Cheshire alikuwa mmoja wa wanahabari waliokuwa kwenye eneo hilo,Amesema milango ya tunnels ilikuwa imefungwa huku ikiwa na nyaya kila mahali.

''Tulipanda milimani na kutazama shughuli hiyo umbali wa mita 500 kutoka kwenye eneo hilo''

''Walihesabu, tatu,mbili, moja, kisha ukatokea mlipuko mkubwa, uliweza kuuhisi, kulikuwa na vumbi jingi, joto kali, mlipuko ulitoa sauti kubwa.

Korea Kaskazini imekwishafanya majaribio sita ya nuklia tangu mwaka 2006 kwenye mfumo wa mashimo yaliyochimbwa chini ya mlima Mantap.

Inaaminika kuwa ni eneo pekee la majaribio duniani mpaka sasa.