Rais wa Afrika Kusini Ramaphosa asema mshahara wake ukatwe nusu kusaidia wakfu wa Mandela

Rais Cyril Ramaphosa ni miongoni mwa watu matajiri nchini Afrika Kusini
Maelezo ya picha,

Rais Cyril Ramaphosa ni miongoni mwa watu matajiri nchini Afrika Kusini

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza kuwa atatoa msaada kiasi cha nusu ya mshahara wake kusaidia watu wasiojiweza.

Bwana Ramaphosa alisema lengo lake ni kuhamasisha watu wenye uwezo kutoa sehemu ya mapato yao kusaidia kujenga nchi.

Mchango wa dola za Marekani 130,000 zitatolewa kwa mfuko wa Nelson Mandela.

Ramaphosa ni mmoja kati ya watu watajiri zaidi Afrika Kusini akiwa na mali zenye thamani ya dola za marekani milioni 450.

Wakosoaji wamekuwa wakimshutumu kutoguswa na hali ya umaskini wa watu, alikosolewa pia kwa kutumia dola milioni 2 kununua nyati na mtoto wake mwaka 2012.

Rais huyo mwenye miaka 65 alikuwa mfanya biashara kabla ya kuwa makamu wa Rais mwaka 2012.

Uamuzi wake wa kutoa sehemu ya mshahara wake umesababisha kuwepo kwa hisia tofauti nchini Afrika Kusini.

Mwandishi wa BBC, Pumza Fihlani anasema wengine wanaona pesa hizo si kitu ikilinganishwa na mali alizonazo wengine wanaona kuwa hatua hii inalenga kurejesha utamaduni wa kutoa huduma kwa Umma ndani ya chama tawala ANC.

Maelezo ya picha,

Rais Ramaphosa aliingia madarakani baada ya Jacob Zuma kulazimishwa kujiuzulu

Akizungumza ndani ya Bunge la nchi hiyo siku ya Jumatano, Rais Ramaphosa amesema aliamua kutoa mchango kwa ajili ya kumuenzi Baba wa taifa hilo, hayati Nelson Mandela.

fedha hizo zitazinduliwa tarehe 18 mwezi Julai wakati wa kumbukumbu ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mandela

Bwana Ramaphosa alikuwa rais mwezi Februari baada ya Jacob Zuma kulazimishwa kujiuzulu kutokana na shutuma za vitendo vya rushwa.

Waziri wa madini Gwede Mantashe alisema mwezi Januari kuwa Ramaphosa hatajihusisha na vitendo vya rushwa kwa kuwa hana shida na pesa.

''Yeye ni tajiri, ikiwa ataiba tutamuuliza ''kwa nini unaiba, kwa sababu unavyo vya kutosha? '' alisema Mantashe.

Viongozi wengine wamefanya nini?

Rais wa Marekani Donald Trump huchangia mshahara wake wa mwaka kiasi cha dola 400,000 kwa ajili ya miradi mbalimbali.

George Weah wa Liberia hupeleka asilimia 25 ya mshahara wake kwa mwaka kiasi cha takriban dola 100,000 kwenye mfuko wa maendeleo

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari alichukua asilimia 50 tu ya mshahara alipoingia madarakani mwaka 2015

Rais wa Urusi Vladmir Putin alichukua asilimia 10 ya mshahara mwaka 2015 kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.