Korea Kaskazini ipo tayari kukutana na Trump 'wakati wowote'

Rais Kim Jong-Un na Rais Donald Trump
Maelezo ya picha,

Rais Kim Jong-Un na Rais Donald Trump

Korea Kaskazini imeelezea kusikitishwa kwake na hatua ya rais Donald Trump kujitoa katika mazungumzo yaliyopangwa kufanyika juni 12 huko Singapore.

Kwa mujibu wa mashirika ya habari nchini humo, uamuzi huu umekuwa kinyume na matarajio ya dunia.

Inadaiwa kuwa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un alikuwa amefanya jitihada zote katika maandalizi ya mkutano huo na kwamba Pyongyang ilikuwa tayari kuhakikisha tofauti zilizopo kati ya taifa lake na Marekani zinasuluhishwa kwa namna yoyote na popote, lakini Trump mwenyewe amesema uwezekano wa kufanyika mazungumzo hayo bado upo.

Taarifa hizo pia zimeleta mshtuko kwa jumuiya ya kimataifa, ambapo katibu mkuu wa umoja wa mataifa Antonio Guterres, ameelezea kuguswa kwake na hatua hiyo ya Marekani huku naye rais wa Korea Kusini Moon Jae-In akitoa wito kuwepo kwa mkutano wa dharura wa viongozi wa juu wa usalama kuhusiana na suala hilo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Marekani imeghadhabishwa na hatua ya Korea kaskazini kufanya mazoezi juu ya rasi hiyo katika siku za nyuma

Mkutano huu ungejadili namna ya uondoaji wa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea kufuatia mkutano wa Korea zote mbili uliofanyika mwezi April mwaka huu.

Hata hivyo yapo baadhi ya mambo yanayotajwa kama dosari zilizo jionyesha kuelekea mazungumzo hayo na hasa kauli za kushinikiza msimamo wake ndani ya barua aliyomuandikia kiongozi wa Korea Kaskazini baada ya kuwa na mazungumzo na rais wa Korea kusini Moon.

Washington pia inailaumu Pyongyang kwamba haikuwa imara katika maandalizi na kwamba pale maofisa wa Marekani walipopanga kukutana na wanadiplomasia wa Korea kaskazini hawakutokea, dalili zilizokuwa mbaya kuelekea mazungumzo haya.

Chanzo cha picha, AFP/GETTY

Maelezo ya picha,

Donald Trump na Kim Jong-un walitarajiwa kukytana Singapore Juni 12

Je barua ya Trump imesema nini?

Trump amesema alikuwa 'akitazamia sana' kukutana na bwana Kim.

"Kwa huzuni, na kutokana na hasira kubwa na uhasama wa wazi uliodhihirishwa katika taarifa yako ya hivi karibuni, ninaona uwa sio sawa, kwa wakati huu kufanya mkutano uliopangwa kwa muda mrefu," Rais Trump alisema katika barua aliyomuandikia Kim.

"Unazungumzia uwezo wako wa nyuklia, lakini wetu ni mkubwa na wenye nguvu kiasi cha kwamba naomba hatutozitumia kabisa," aliongeza.

Lakini ameutaja mkutano huo kama 'nafasi iliyokosekana' akisema "siku moja natazamia sana kukutana na wewe".

Katika barua kwenye ikulu ya White house, Trump amesema hatua hiyo 'inarudisha nyuma sana jitihada kwa Korea kaskazini na ulimwengu', akiongeza kuwa jeshi la Marekani 'liko tayari ikihitajika' kujibu hatua yoyote isyo na mpangilio kutoka kwa Korea kaskazini.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Kim Jong-un alikutana kwa mara ya kwanza na Moon Jae-in katika mkutano ulio wa tatu kwa viongozi wa Korea zote kuwahi kukutana.

Kumekuwa na hisia gani?

Rais wa Korea kusini Moon Jae-in amesema 'amechanganyikiwa' na ni jambo la kujuta kwamba mkutano huo haufanyiki tena.

Ni maafisa wa KOrea kusini walioiarifu Marekani mara ya kwanza kuwa Kim yuko tayari kujadili uwezekano wa kusitisha mpango wake wa nyuklia.

Mnamo Aprili, viongozi wa Korea zote walifanya mkutano wa kihistoria mpakani, na kuahidi kusitisha uhasama na kushirikiana kueleka kusitisha matumizi ya silaha za nyuklia katika rasi ya Korea.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amesema Marekani na Korea kaskazini haizpaswi kuvunjika tamaa akieleka subra kubwa inahitajika.

Nchini Marekani, seneta wa Republican Tom Cotton amempongeza rais Trump kwa kuweza kuona 'udanganyifu wa Kim Jong-un'. Lakini seneta wa Democratic Brian Schatz amesema hatua hiyo ni kinachotokea wakati 'wasanii wanapokutana na wachochezi wa vita'.