WHO yatoa tahadhari kuhusu watu kuumwa na nyoka

Mashambulizi ya nyoka yameleta madhara makubwa duniani
Maelezo ya picha,

Mashambulizi ya nyoka yameleta madhara makubwa duniani

Nchi wanachama wa mkutano wa shirika la afya duniani wamepitisha azimio la kutambua kuumwa na nyoka kuwa ni suala linalohitaji kupewa kipaumbele katika kulishughulikia.

Maelfu ya watu hufa kila mwaka na wengine kuwa walemavu kutokana sumu inayotokana na shambulio la nyoka.

WHO inasema athari zinazotokana na kuumwa na nyoka zimeendelea kuwa moja kati ya magonjwa ya kitropiki ambayo hayatiliwi maanani.

Kufikiwa makubaliano hayo kwa nchi wanachama wa WHO , kuna nia ya kuhakikisha kuwa kunakuwa na mbinu za kuzuia, kutibu na kukabili mashambulizi ya nyoka.

Makundi ya mbalimbali ya wanaharakati wa masuala ya afya yamesifia azimio hilo na kusema kuwa hatua hiyo inafungua milango katika kupunguza vifo na ulemavu duniani kote.

Shirika la Afya duniani sasa lina jukumu la kuja na mpango wa pamoja kuimarisha programu za tiba, kuzuia na kurekebisha.

Hii itahusisha kutoa dawa za kupambana na sumu kwa bei rahisi, dawa ambazo ilikua gharama kupatikana kwenye nchi zilizo masikini hasa zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.

Maelezo ya picha,

Wataalam wanasema zaidi ya watu 100,000 hufa kutokana na madhara ya kuumwa na Nyoka

Hali ya umaskini na kutokuwa na vituo vya afya vinavyokidhi mahitaji kumesababisha vifo vya maelfu ya watu huku wengine wakitafuta tiba kwa matabibu wa kienyeji ambao husababisha madhara zaidi.

Lakini mpango huu mpya utalenga kuwafundisha watoa huduma wa afya jinsi ya kushughulikia mtu aliyeumwa na nyoka na elimu ya huduma ya kwanza kwa jamii iliyo hatarini.

Kila mwaka zaidi ya watu laki moja hufa duniani kutokana na kuumwa na nyoka asilimia 20 kutoka barani Afrika.

Karibu watu nusu milioni wana ulemavu wa kutokuona, kukatwa viungo na ulemavu mwingine kutokana na mashambulizi ya nyoka.

Dondoo za huduma ya kwanza baada ya mtu kuumwa na nyoka:

  • Jaribu kukumbuka umbo na rangi ya Nyoka:

Kufahamu namna ambavyo Nyoka anavyofanana kunasaidia wakati wa matibabu baadaye, lakini usijaribu kumshika kwa kuwa utakuwa hatarini hata akaleta madhara kwa mtu mwingine.

  • Ondoka eneo la hatari

Kama uko mwenyewe mbali na msaada, jambo la kwanza ni kwenda eneo lenye usalama.Tafuta eneo ambalo utaomba msaada.Kama uko na watu wengine wacha wakubebe kama inawezekana,ili kupunguza kiasi cha sumu kutembea mwilini,wataalam wanaeleza.

  • Usifyonze sumu kutoka kwenye jeraha

Sumu huingia ndani kabisa kwenye eneo la kati ya ngozi na misuli na husambaa mara moja (ndani ya dakika moja).Hivyo haiwezekani kuondoa sumu kwa kunyonya kwani itazidisha maumivu na uharibifu zaidi pasipo na ulazima.

  • Ondoa vitu vilivyovaliwa sehemu iliyoathiriwa

Vua vitu kama pete au nguo zinazobana katika eneo ambalo madhara yametokea kama mkononi kwa sababu vinaweza kusababisha damu kutotembea vizuri.