Muhamiaji wa Mali atangazwa shujaa Ufaransa kwa kumuokoa mtoto ghorofani

Mamoudou alionekana kupanda ghorofa hiyo kwa kasi ambayo ilisaidia kuokolewa kwa mtoto huyo
Maelezo ya picha,

Mamoudou alionekana kupanda ghorofa hiyo kwa kasi ambayo ilisaidia kuokolewa kwa mtoto huyo

Kijana mmoja raia wa Mali ambaye ni mhamiaji katika mji wa Paris Ufaransa amekuwa kivutio kikubwa na kupata umaarufu kwa haraka kwa ujasiri wake ambapo amemwokoa mtoto mwenye umri wa mika minne aliyekuwa akining'inia kwenye ghorofa ya nne.

Video ambayo imesambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii imemwonyesha kijana huyo Mamoudou akipanda kwa kasi kwa mbele kwenye ghorofa hiyo na kumwokoa mtoto huyo ambaye alikaribia kudondoka na hata kupoteza maisha kama asingeokolewa mapema.

Sasa kijana huyo mhamiaji amepata heshima kubwa nchini Ufaransa ambapo Rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron amemkaribisha Bwana Gassama ikulu Elysee leo Jumatatu kumshukuru binafsi na kumwita kuwa Spiderman wa karne 18.

Maelezo ya picha,

Baada ya kufika ghorofa ya nne alimvuta haraka mtoto

Meya wa Mji wa Paris Anne Hidalgo pia alipongeza shujaa huyo mwenye umri wa miaka 22 na akasema amemwita kumshukuru.

"Nakubali Mamoudou Gassama kwa kitendo chake cha ujasiri kilichookoa maisha ya mtoto," Bi Hidalgo aliandika kwenye mtandao wa tweeter.

"Alinieleza kwamba alikuwa amefika kutoka Mali miezi michache iliyopita akitaka kutafuta maisha yake hapa.

"Nilijibu kuwa kitendo chake cha kishujaa kimekuwa mfano kwa wananchi wote na kwamba Jiji la Paris litakuwa tayari kumsaidia katika jitihada zake za kukaa nchini Ufaransa."

Tukio hilo lilitokea siku ya Jumamosi jioni kwenye barabara ya kaskazini mwa jiji hilo la Paris.

Bwana Gassama aliwaambia waandishi wa habari kwamba alikuwa akitembea wakati alipoona umati uliokusanyika mbele ya jengo hilo.

"Nilifanya hivyo kwa sababu alikuwa mtoto," gazeti la Le Parisien lilimnukuu akisema. "Nilipanda ... Asante Mungu nimemwokoa."

Kikosi cha uokoji na zima moto cha mji wa Parisi walisema wafanyakazi wake walifika eneo la tukio na kukuta mtoto huyo tayari ameokolewa.

"Kwa bahati, kulikuwa na mtu ambaye alikuwa na afya nzuri na ambaye alikuwa na ujasiri wa kwenda na kumwokoa mtoto," msemaji kikosi hicho aliliambia shirika la habari la AFP.

Mamlaka za mitaa ziliwambia waandishi wa habari nchini Ufaransa kuwa wazazi wa mtoto hawakuwa nyumbani wakati tukio hilo.

Baba wa mtoto huyo anahojiwa na polisi kosa la kumwacha mtoto wake bila uangalizi.