Maafisa wakuu wa Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa Kenya wakamatwa kuhusiana na rushwa

Vijana wa Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS)
Maelezo ya picha,

Vijana wa Shirika la Vijana wa Huduma kwa Taifa wakiwa wamepanga foleni kwenye kituo cha kupigia kura mjini Nairobi, Agosti 07, 2017, kabla ya kusambazwa kulinda vituo vya kupigia kura

Mkuu wa Shirika la Vijana wa Huduma kwa Taifa nchini Kenya (NYS) Richard Ndubai, pamoja na maafisa wengine wakuu, wamekamatwa na polisi kwa tuhuma za ufisadi.

Hii inafuatia agizo la Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Umma aliyeagiza kushtakiwa kwa washukiwa wote waliotajwa katika kashfa ya Shilingi bilioni 9.

Maagizo ya Mkurugenzi wa mashtaka ya Umma Noordin Haji yametolewa baada ya kupokea taarifa kuhusu kampuni 10 na pia zaidi ya watu 40 binafsi waliotajwa katika sakata hiyo NYS scandal kutoka kwa Mkurugenzi wa uchunguzi wa Uhalifu George Kinoti.

"Mkurugenzi mkuu wa Mashtaka ya Umma amechunguza nyaraka zinazohusiana na sakata inayoendelea katika NYS na ameagiza mashtaka yafunguliwe mara moja dhidi ya wite waliotajwa kushukiwa ," iliandika ofisi ya mwendesha mashtaka wa umma kwenye ukurasa wake wa Twitter Jumatatu asubuhi.

Washukiwa wengine kadhaa pia wamekamatwa na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani katika kipindi cha saa 24, kulingana na afisa mmoja katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma.

Pesa hizo zinadaiwa kuchukuliwa kutoka kwenye shirika hilo katika kipindi cha miaka mitatu, kwa mujibu wa duru mbali mbali.

Kashfa zinazoikumba serikali Kenya

  • Sh8bn katika Shirika la Vijana wa Huduma kwa Taifa (NYS)
  • Sh2bn katika Wizara ya Mazingira na Maliasili katika upanzi wa miti
  • Sh1.9bn katika Shirika la Kitaifa la Nafaka na Mazao (NCPB)
  • Sh0.6bn katika Shirika la Mafuta la Kenya Pipeline
  • Sh10 milioni katika Hazina ya Ustawi wa Vijana
  • Kutolewa kwa zabuni ya mabilioni ya pesa shirika la kusambaza umeme, Kenya Power

Chanzo: Vyombo vya habari Kenya

Sakata hiyo ya NYS inadaiwa kutekelezwa katika mpango uliowahusisha maafisa wa ngazi ya juu wa serikali na 'wauzaji hewa' na pigo jipya kwa juhudi za rais wa Kenya Uhuru Kenyatta katika juhudi zake za kukabiliana na ufisadi.

Mwanamke aliyeuzia serikali hewa

Mwanamke anayedaiwa 'kuuzia hewa' NYS ni miongoni mwa waliokamatwa, akiwa pamoja na jamaa zake.

Vyombo vya habari vilisema Ann Wambere Ngirita alipokea malipo ya Sh59 milioni pesa za Kenya ( $586,000; £440,000) bila kuwasilisha chochote kwa shirika hilo la serikali.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari Kenya, jumla ya watu 17 wamekamatwa kuhusiana na kashfa zinazodaiwa kuchangia kufujwa kwa Sh9bn pesa za Kenya ($88m) katika NYS.

Bi Ngirita anasema alikuwa amepewa kandarasi ya kuuzia shirika hilo nyama ya mikebe, mananasi, maharagwe, biskuti na nyundo.

Lakini hakuwasilisha bidhaa hizo kwa shirika hilo.

Anasema alipewa kandarasi hiyo na mkandarasi mwingine na hafahamu iwapo kuna chochote kilichowasilishwa kwa NYS.

Bi Ngirita anadaiwa kusema alichofanya pekee kupewa kazi ni kwenda afisi za NYS eneo la Gilgil, magharibi mwa jiji la Nairobi na kuomba apewe zabuni ya kuuzia shirika hilo bidhaa.