Mamoudou Gassama: 'Spiderman' aliyeishangaza Ufaransa kwa kumuokoa mtoto kutoka kwenye jengo la ghorofa apewa uraia

Mamoudou Gassama meets Emmanuel Macron
Maelezo ya picha,

Bw Gassama alikutana na Emmanuel Macron Jumatatu

Mhamiaji wa Mali amepongezwa kama shujaa baada ya kukwea sehemu ya mbele ya jengo la ghorofa mjini Paris kumuokoa mtoto aliekuwa kwenye uzio wa ubaraza wa ghorofa ya nne kwenye jengo refu.

Video ya Mamoudou Gassam akimuokoa mtoto ilisambaa sana kwenye mitandao ya kijamii.

Alivuka kutoka kwenye ubaraza mmoja hadi mwingine kwa muda wa chini ya dakika moja akamvuta mtoto huyo aliyekuwa amekwama na kumsalimisha.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron baadaya kukutana na Bw Gassama kwenye makazi yake ya Elysee Palace Jumatatu kumshkuru binafsi alitangaza kumpa uraia wa taifa hilo.

Maelezo ya picha,

Bila kujali harati, Mamoudou Gassama alivuka kutoka veranda moja hadi jingine la jengo

Alimpa pia medali ya ushujaa na kumuahidi nafasi ya kazi katika idara ya zima moto.

Ruka Facebook ujumbe, 1

Haipatikani tena

Tazama zaidi katika FacebookBBC haihusiki na taarifa za kutoka mitandao ya nje.

Mwisho wa Facebook ujumbe, 1

Meya wa Paris Anne Hidalgo pia alisifu sana ushujaa wa mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 22, na akasema alimpigia simu kumshukuru.

Alimuelezea kama "Spiderman wa 18", akimaanisha wilaya nambari 18 ambako uokoaji huo ulifanyika mjini Paris.

Maelezo ya picha,

Akiwa na stakabadhi yake ya kuthibitisha uraia wake

Maelezo ya picha,

Wakati alipokuwa kwenye ghorofa ya nne Bw Gassama alimvuta mtoto na kumuweka pahala salama

"Hongera kwa Mamoudou Gassama kwa tendo lake la ujasiri la kumuokoa mtoto," ulisema ujumbe wa Twitter wa Hidalgo.

"Alinielezea kwamba alikuwa amewasili kutoka nchini Mali miezi michache iliyopita akiwa na ndoto ya kujenga maisha yake hapa.

"Nilimjibu kwamba ishara yake hii ya ushujaa ni mfano kwa raia wote na kwamba Jiji la Paris bila shaka litakuwa tayari kumuunga mkono katika juhudi zake za kuishi Ufaransa.

Kisa hicho kilifanyika Jumamosi jioni kwenye mtaa mmoja uliopo kaskazini mwa jiji la Paris.

Bw Gassama aliwaambia waandishi wa habari kuwa alikuwa akipita tu mtaani ndipo alipoona umati wa watu umekusanyika mbele ya jengo.

"Nilijitolea kwa sababu alikuwa ni mtoto," gazeti la Le Parisien lilimnukuu akisema . "Nilikwea jengo... Namshukuru Mungu nilimuokoa."

Wahudumu wa kampuni ya zima moto jijini Paris walifika eneo la tukio na kupata tayari mtoto ameokolewa.

"Kwa bahati nzuri , kulikuwa na mtu mwenye nguvu za mwili na mwenye ujasiri wa kwenda na kumchukua mtoto," aliliambia shirika la habari la AFP.

Maafisa wa eneo hilo walionukuliwa na vyombo vya habari vya Ufaransa walisema kuwa wazazi wa mtoto huyo hawakuwa nyumbani wakati alipookolewa.

Baba yake amekuwa akihojiwa na polisi akishukiwa kumuacha mwanae bila mtu wa kumuangalia, zimeeleza taarifa za mahakama.

Inaaminiwa kuwa, mama yake hakuwa Paris wakati wa tukio hilo.