Mike Sonko: Gavana wa Kenya anayehofia usalama jiji lake

Bw Sonko alihutubu katika kanisa moja eneo la Kasarani, Nairobi Jumapili Haki miliki ya picha MIKE SONKO/TWITTER
Image caption Bw Sonko alihutubu katika kanisa moja eneo la Kasarani, Nairobi Jumapili

Gavana wa Nairobi Mike Sonko amesema hahitaji tena ulinzi kutoka kwa serikali wiki chache baada ya walinzi wake kupunguzwa.

Kiongozi huyo ambaye alikuwa amedai maisha yake yamo hatarini alisema wananchi wanatosha kumlinda.

Alirejea jijini Nairobi Jumapili ambapo alihudhuria ibada katika kanisa moja eneo la Kasarani, kusini mashariki mwa jiji hilo baada ya kudaiwa kulikimbia jiji.

Walinzi wake walipunguzwa kutoka hadi watano katika hatua ambayo serikali ilisema ililenga kupunguza idadi ya maafisa wa polisi ambao wanatumiwa kuwalinda "watu mashuhuri".

Taarifa zinadokeza kwamba awali alikuwa na walinzi kati ya 15 na 26.

Kwa wiki moja, vyombo vya habari Kenya vimekuwa vikiripoti kuwa gavana huyo alikuwa ameamua kuhama kutoka Nairobi na kuanza kuendeshea shughuli zake kutoka nyumbani kwake eneo la Mua, kaunti jirani ya Machakos.

Picha zilisambaa mtandaoni zikidaiwa kumuonyesha akiongoza kikao cha baraza la mawaziri wa serikali ya kaunti ya Machakos kutoka nyumbani kwake.

Gazeti la Nation linasema mkutano huo uliandaliwa kuwakutanisha pamoja mawaziri hao siku ya Jumapili, na baadaye kikao cha kufuatiliza kikafanyika Jumanne.

Naibu Mkurugenzi wa mawasiliano wa baraza la jiji Elkana Jacob kupitia taarifa Alhamisi, alisema: "Sijui ni kwa nini watu wanadai kwamba Gavana Mike Sonko 'amezingirwa'. Gavana ana nyumba nyingi katika miji mbalimbali: Garissa, Kisumu, Mombasa, Kilifi, Malindi, Machakos, Nairobi, miongoni mwa mingine."

"Isitoshe, ana haki ya kuandaa mikutano katika nyumba yake yoyote ile, kwa hivyo tunafaa kujizuia kutoa madai kwamba Sonko ameenda mafichoni."

Alisema gavana huyo ni mtu huru, aliyechaguliwa na wapiga kura Nairobi.

Jumapili, akizungumza eneo la Njiru, Kasarani katika kanisa la AIPCA Bw Sonko alisema alipashwa habari na mmoja wa maafisa wakuu wa polisi kwamba wapo watu wanaotaka kumuua.

Alidai afisa aliyemdokezea hivyo ametishiwa maisha.

Alilinganisha hali yake ya sasa na ya kiongozi wa chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga na wenzake wa muungano wa upinzani wa NASA ambapo walipokonywa walinzi kwa muda na serikali wakati wa mzozo wa kisiasa uliohusiana na uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

"Walinzi wa Raila Amolo Odinga walipoondolewa, aliendelea na maisha au hakuendelea nayo? Gavana Joho alipopokonywa walinzi (gavana wa Mombasa), maisha yaliendelea. Viongozi hao wengine wa Nasa waliopokonywa walinzi, maisha yao yaliendelea au haya kuendelea?"

"Hata mimi nikiwa Kaunti ya Nairobi, maisha yangu na raia yataendelea. Ninaamini wananchi ni usalama tosha. Sihitaji usalama wa polisi tena."

Haki miliki ya picha MIKE SONKO/TWITTER
Image caption Gavana huyo akihutubu wakati wa sherehe ya kupanda miti 12 Mei eneo shule ya Moi Forces, Mathare jijini Nairobi

Sonko alijipatia umaarufu kutokana na mtindo wake usio wa kawaida alipokuwa mbunge wa eneo la Makadara, Nairobi.

Anafahamika kwa kuvalia vito, mikufu na bangili za thamani.

Alipokuwa mbunge, alikuwa akiandamana 'kutetea wanyonge' na wachuuzi walipokuwa wanafurushwa kutoka maeneo yao ya kazi na serikali ya jiji.

Anakumbukwa pia kwa kuongoza waandamanaji Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai (ICC) The Hague, Uholanzi kulalamikia kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta ambayo baadaye ilisitishwa.

Alipokuwa seneta, alianzisha kundi kwa jina Sonko Rescue Team ambalo lilikuwa likitoa huduma kama vile maji, matibabu na misaada wakati wa mazishi.

Wakati mmoja alipoitwa kusaidia familia zilizokuwa zimeathiriwa na bomoa bomoa jijini mwaka 2014, alimpigia simu Rais Kenyatta na kumuweka kwenye kipaza sauti. Rais alitoa agizo ubomoaji usitishwe.

Alipoingia uongozini kama gavana wa Nairobi, ameonekana kuchukua hatua ambazo zinaenda kinyume na aliyokuwa akitetea.

Anaongoza mpango wa kuwaondoa wachuuzi katikati mwa jiji na pia kuondoa wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma kutoka katikati mwa jiji.

Mambo Muhimu kuhusu Mike Sonko

  • Alizaliwa Februari 1975
  • Alikuwa mbunge wa Makadara 2010-2013
  • Alichaguliwa seneta wa Nairobi Machi 2013
  • Alichaguliwa kuwa gavana wa Nairobi Agosti 2017
  • Serikali ilitangaza kupunguza walinzi wake hadi watano 16 Mei, 2018

Bw Sonko anaamini magenge ya wafisadi ambao wamekuwa wakifaidi chini ya serikali za awali ndio maadui wake wakuu na amekuwa pia akilaumu serikali ya awali ya Dkt Evans Kidero kwa kuzembea kazini.

Amekuwa akiapa kuyaangamiza magenge hayo.

Siku chache zilizopita, aliwashangaza wengi kwa kupendekeza uteuzi wa wakili mzaliwa wa Kenya Miguna Miguna ambaye kwa sasa yupo Canada baada ya kufurushwa na serikali kwa tuhuma kwamba aliukana uraia wake wa Kenya na hakuomba tena kuwa raia.

Bw Miguna, ambaye aliwania ugavana dhidi ya Sonko uchaguzini Agosti mwaka jana, alikuwa amemkosoa mwanasiasa huyo wakati huo na kusema hawezi kutegemewa kuongoza jiji kubwa kama Nairobi.

Haki miliki ya picha MIKE SONKO/TWITTER

Jumapili, Bw Sonko alitetea hatua yake ya kumteua Miguna na kusema ni yeye pekee anayeweza kukabiliana vilivyo na magenge ya wafisadi katika serikali ya jiji la Nairobi.

Bw Sonko alisema wanaotarajia kuwa tofauti kati yake na wawakilishi wa wadi wanaohudumu kama madiwani kutachangia kuondolewa madarakani kwake kwamba wamenoa.

"Kama bunge, nawaheshimu. Ndio walio na mamlaka ya kuniambia niwasilishe jina la mtu mwingine, lakini hilo halitatufanya tugombane. Tunacheza siasa za kisasa Nairobi," alisema jana.

"Nimependekeza uteuzi wa Miguna kuwa naibu wangu na ni bunge la kaunti litakaloamua."

Bw Miguna anahitaji kuidhinishwa na bunge hilo kabla ya uteuzi rasmi.

Mada zinazohusiana