Kuvunja Chungu:Mila ya wameru yenye nia ya kukemea

Image caption Mzee wa Mila akizungumza na BBC kuhusu mila ya kuvunja chungu

"Kuna mtu wa kwetu aliuawa hapa akavunjwa shingo…tuliwauliza watu wakakataa hivyo tukaenda kuvunja chungu.Ni mwaka juzi hayo yalitokea .

Baada ya ukoo huo kupoteza watu 17 ndani ya mwaka mmoja,wakaamua kuja kujisalimisha na kulipa faini.

Hii ni mara ya pili nnatumia chungu kusuluhisha matatizo yangu."Babu Godfrey anaeleza.

Babu huyo anasema muhusika aliyemdhuru ndugu yake alikamatwa na kupelekwa mahakamani ila akaachiwa baada ya muda mfupi. Hivyo baada ya kuona kifo cha ndugu yake hakijapata hukumu aliamua kwenda kutafuta chungu kupata haki ya ndugu yake itendeke.

Uonevu katika jamii ya wameru ndio chanzo cha tamaduni ya kuvunja chungu katika jamii mkoani Arusha kaskazini mwa Tanzania.

Hukumu hii ambayo hutolewa katika mahakama za jadi imekuja baada ya kuona kwamba sheria rasmi hazileti ufumbuzi wa matatizo yao.

Wazee wa eneo hilo la Meru lenye watu takribani laki mbili unusu katika takwimu za mwaka 2012 wanaamini kwamba kuvunja chungu imekuwa fimbo ya mnyonge.Zamani walikuwa wanakosa sehemu ya kushtaki maana mahakamani walikuwa wanashinda kesi.

Wazee hao wamekataa kuwa chungu hakina uhusiano wowote na nguvu za giza yaani kwa maana kuwa hakuna uhusiano wa kishirikina lakini ni suluhisho la migogoro katika jamii zao.

Image caption Kibali cha kutekeleza mila kwa jina kuvunja chungu

Chungu hakiingilii maamuzi ya mahakama , pili hakijumuishi ushahidi uliopatikana mahakamani au jina la mhusika bali kisasi kinamrudia yule aliyedanganya.

Bwana Jacob Kahaya ni katibu wa washiri yaani wazee wa kimila wa jamii ya wameru ambaye ni miongoni mwa wahusika wakuu wanaohakikisha kuwa adhabu ya chungu inafanyika kiufasaha anasema anaamini kuwa Imani ya dini ya Kikristo imepunguza kasi ya matumizi ya chungu ingawa wanaamini mila hiyo haitaisha.

Jamii inasema kuwa kama hakuna maasi basi hakuna chungu lakini kama yapo,chungu kitaendelea kuwepo kwa kuwa kinaleta hofu kwa watu kutotenda maovu"

Aidha kuna makosa ambayo hayavunjiwi chungu,mfano mtu akimtungisha mimba msichana hapasuliwi chungu hata kama mwenye mimba ameikataa mimba hiyo.Maana binti anaweza akawa amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na watu wengi kwa wakati mmoja na akawa hana uhakika wa nani mwenye ujauzito .

Chungu ni nini?

Katika jamii ya Wameru Chungu kinatumika kama dawa kwa wanaokimbia polisi,sheria,mahakama na watoao hongo.

Kuvunja chungu sio kitu kinachofanyika bila utaratibu,hivyo kama umeibiwa lazima mtu ufanye uchunguzi wako kwanza kwa ndugu tu kabla ya kibali hakijatolewa.

Huwezi kuvunja chungu hivi hivi mpaka wazee wa jadi wasikilize kesi yako na baada ya hapo tangazo linatolewa kwa siku 30 na huwekwa katika mitaa yote ya eneo husika na baada ya hapo mlalamikaji hupewa kibali. Mara nyingi mwenye kudai akishaweka tangazo la chungu wahalifu wanajisalimisha kabla.

Utaratibu wa uvunjaji chungu huwa na watu maalamu wakukivunja chungu hicho kwa muda wa siku 3 hadi 7.

Mvunja chungu hawezi kuvunja bila kibali cha barua kutoka kwa katibu wa mahakama ya washiri(wazee wa jadi).

Image caption Mila hizi bado zinatekelezwa kwenye baadhi ya maeneo nchini Tanzania

Na endapo mtuhumiwa atakutwa na hatia na akahukumiwa kufungwa jela na baada ya kutumikia kifungo , mtu huyo anaporejea uraiani anapaswa kulipa ng'ombe 49 kama faini .

Lengo la taratibu hizi ni kukemea

''Ni mara mbili nimevunja chungu na mwezi wa tatu mwaka huu mimi na ndugu yangu tulipata pigo la ng'ombe wetu kuibwa,na tulifanya juhudi ya kuwafuatilia eneo moja liitwalo Namalulu na tukaweka tangazo la upotevu huo lakini hakuna aliyejitokeza kukiri kuhusika kwake "mzee Ruben Lesiyo mshili.

Wazee wa jadi wanadai kuwa Chungu kinao uwezo wa kukamata ukoo mzima wa muhusika mpaka waombe radhi na kurudisha mali

Chungu kinapovunjwa,watu wanaoanza kuathirika ni wale watu wake wa karibu kama ndugu au walioshuhudia na mwizi mwenyewe anakuwa wa mwisho.Yani chungu ndio dawa yao..."

Aidha wanasema uvunjaji wa chungu sio kitu rahisi kukifanya la hasha.

Kuna chungu kikali na kisicho kikali,inategemea na ukali wa mdomo wa mtu wakati anashtakia tatizo lake.

„kila mwenye tatizo laki ana maamuzi ya kutoa fedha ama ng'ombe dume mkubwa ama fedha tasilimu laki tatu , si kila mtu anaruhusiwa kuvunja chungu tu"..mkazi wa Meru aliyewahi kuvunjiwa chungu.

Huduma hii ya kuvunja chungu haipo kwa wameru peke yake bali hata kwa wageni waliofika mkoani humo kufanya kazi tu.Mfano , hata kwa watu kutoka nje ya nchi inabidi waingie kwenye ukoo fulani ndio waweze kusaidiwa.

Jitihada za kutokomeza ndoa za utotoni

Wanawake wapigwa marufuku kupiga ngoma Burundi

Hata hivyo Vyungu ni nadra sana kuvunjwa hovyo ingawa waombaji ni wengi.Tangu mwaka 2009 takribani vyungu 20 vilivunjwa.

Senya Elly ni Afsa utamaduni wa kabila la wameru yeye anasema kwa sasa chungu hakivunjwi na tukio hilo hufanyika kwa baadhi ya watu walioamua kutumia adhabu hiyo kuadabisha watu waliofanya makosa makubwa na kukataa kutubu.

Senya anasema pia kwamba kuongezeka kwa ukristu na kupotea kwa wapagani ndio sababu kubwa ya tamaduni hii kupitwa na wakati.

''Mimi hata kama ni kijana mkazi wa mjini,nnaweza kwenda kuvunja chungu lakini lazima niende mahakamani kwanza nikishindwa kupata haki naenda kwenye chungu maana watu wanadhulumu sana"Thobius Mollel mkazi wa Arusha''.

''Mimi nadhani ni tamaduni inayoweka hofu tu lakini si kwamba inasababisha mabaya katika familia ila ni imani tu inayowapa woga watu "Geoge kutoka Arusha anaeleza