Wahamiaji takribani 35 wapoteza maisha baada ya Boti kupinduka Tunisia

Tukio lilitokea karibu na visiwa vya Kerkennah Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Tukio lilitokea karibu na visiwa vya Kerkennah

Takriban wahamiaji 35 wamepoteza maisha baada ya boti yao kupinduka kusini mwa pwani ya Tunisia, Serikali ya nchi iyo imeeleza.

Wahamiaji wengine 67 kutoka Tunisia na maeneo mengine waliokolewa na vikosi vya uokoaji vya pwani.

Tunisia imekuwa njia mpya muhimu kwa wahamiaji wanaojaribu kuvuka kuelekea barani Ulaya .

Hali hii imejitokeza baada ya hatua zinazochukuliwa nchini Libya dhidi ya wanaosafirisha binaadamu, ambao wamekuwa wakifanywa watumwa, wakiteswa na kuuawa.

Ajali ya mwisho kutokea Tunisia ilitokea kwa boti iliyokuwa imebeba takriban watu 180, wengi wao raia wa Tunisia, Waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo ameeleza.

''Boti ilikuwa umbali wa maili tano kutoka katika visiwa vya Kerkennah .''Ilieleza wizara kwenye taarifa iliyonukuliwa na shirika la habari la AFP.

Image caption Wahamiaji wamekuwa wakisafiri kuelekea Ulaya

Raia wa Tunisia na watu wengine wenye asili ya Afrika hutafuta kuvuka bahari ya Mediterranea kutumia boti zisizo na ubora kutoka Tunisia kwenda Sicily Italia.

Vifo hivi vimetokea siku moja ambayo Waziri mpya wa mambo ya ndani Matteo Salvini akizungumza alipotembelea Sicily kuwa Kisiwa hicho kikome kuwa ''Kambi ya wakimbizi wa Ulaya.''

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Wahamiaji tisa, wakiwemo watoto sita wamezama eneo la Antalya nchini Uturuki

Wakati huo huo, askari wa pwani nchini Uturuki wamesema wahamiaji tisa, wakiwemo watoto sita, wamezama katika tukio kama la Tunisia katika pwani ya eneo la Antalya.

Muhimu: BBC imetumia neno ''Wahamiaji'' ikimaanisha watu wote ambao wako safarini wakiwa bado hawajakamilisha taratibu halali za kupata hifadhi.Kundi hili linawahusisha watu wanaokimbia vita, kama vile Syria, ambao wanaweza kupatiwa hifadhi ya ukimbizi, pia watu wanaotafuta kazi na maisha mazuri, ambao serikali zinaweza kuwaita wahamiaji wa kiuchumi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii