Rushwa: Wakuu wa ununuzi wa bidhaa serikalini Kenya wapewa likizo ya lazima

Wanaharakati waliandamana Alhamisi wiki iliyopita kumshinikiza Rais Kenyatta kuchukua hatua
Image caption Wanaharakati waliandamana Alhamisi wiki iliyopita kumshinikiza Rais Kenyatta kuchukua hatua

Serikali ya Kenya imewaagiza wakuu wote wa vitengo vya ununuzi wa bidhaa na huduma katika wizara na mashirika ya umma kwenda likizo ya lazima ya mwezi mmoja huku juhudi za kukabiliana na ufujaji wa mali ya umma zikionekana kushika kasi.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Wizara ya Usalama na Mambo ya Ndani Mwenda Njoka inasema maafisa hao wanafaa kukabidhi majukumu kwa manaibu wao kwa sasa.

Bw Njoka amesema ametuma taarifa hiyo kwa niaba ya msemaji wa serikali Bw Eric Kiraithe.

Maafisa hao pia hawataruhusiwa kusafiri nje ya nchi bila idhini ya Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua.

"Ingawa shughuli hii inalenga kubainisha iwapo watumishi hawa wanafaa kuendelea kushikilia afisi hizo za umma, na kuendelea kuaminika katika idara ya utumishi wa umma, shughuli hii itafanyika kwa njia ya haki na bila kupendelea upande wowote, kwa umakini na kwa kuheshimu haki za kikatiba za wahusika," taarifa hiyo iliyopakiwa katika ukurasa wa Twitter wa kitengo cha mawasiliano cha rais inasema.

"Rais amejitolea kuunda idara ya utumishi wa umma ambayo inakidhi mahitaji na kuakisi matamanio ya Wakenya bila maafisa hao kutumia nafasi hiyo vibaya kujitajirisha au kujifaa."

Wakuu hao wa ununuzi wa bidhaa na huduma wanafaa kutoshikilia majukumu huku shughuli ya kuwapiga msasa ikitarajiwa kuanza.

Maafisa hao wanatakiwa kuwasilisha taarifa kuhusu mali wanayomiliki, madeni waliyo nayo na taarifa kuhusu kazi walizozifanya awali.

Maelezo hayo yanafaa kuwasilishwa kwa afisi ya Mkuu wa Utumishi wa Umma katika jumba la Harambee, Nairobi kufikia Ijumaa.

Bw Njoka hata hivyo amesema wataendelea kupokea mishahara yao kama kawaida katika kipindi hicho.

Hatua hiyo ndiyo ya karibuni zaidi kuchukuliwa na Rais Kenyatta baada yake kuahidi kukabiliana vikali na ufisadi serikalini wakati wa sikukuu ya Madaraka.

Bw Kenyatta, wakati wa maadhimisho hayo mjini Meru, aliagiza wakuu wote wa ununuzi wa bidhaa na huduma katika serikali, wachunguzwe upya kufikia mwisho wa mwezi huu.

Watatakiwa pia kupimwa kwa kifaa ambacho ni cha kubaini iwapo mtu anasema ukweli au anahadaa.

Watakaobainika wanasema uongo baada ya kutumiwa kwa kifaa hicho watafutwa kazi.

Mada zinazohusiana