Pacha walioungana Maria na Consolata wazikwa Iringa, Tanzania

pacha

Watu wengi walijitokeza Iringa kuwaaga pacha waliokuwa wameungana Maria na Consolata waliofariki mwishoni mwa juma.

Miongoni mwa waliofika ni viongozi mbali mbali wa dini na kiserikali, akiwemo waziri wa elimu Prof Joyce Ndalichako.Pacha hao walizikwa katika makaburi ya Tosamaganga baada ya ibada ya wafu kufanyika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCU).

Askofu Jimbo Katoliki Njombe, Alfred Maluma amesema vifo vya Pacha hao vinafaa kutumiwa na Watanzania kukumbushana wajibu wao kwa watu wenye ulemavu.

"Wameacha somo hilo, tuwajali watu wenye ulemavu hilo ndilo somo walilotuachia Maria na Cobsolata."

Amesema Mungu aliwaumba pacha hao kwa mfano wa sura yake na akawapa uhai kwa kipindi walichokuwa duniani.

Vifo vya Maria na Consolata ambao walikuwa ni wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Ruaha vimegusa wengi hasa kutokana na ujasiri walioonyesha wakati wa uhai wao.

Vile vile watakumbukwa kwa ucheshi wao.

Pacha hao wameandaliwa jeneza moja lenye mfumo wa watu wawili, misalaba miwili na watazikwa katika kaburi moja.

Mkuu wa Shirika la Maria Consolata, Jane Nugi alikuwa ameambia gazeti la Mwananchi kwamba pacha hao waliamua eneo ambalo watazikwa.

Alisema katika uhai wao walichagua kuzikwa kwenye eneo wanalozikwa viongozi wa kanisa Katoliki eneo hilo.

"Wakati wakiumwa walisema wangetamani kuhifadhiwa tunakohifadhiwa sisi hivyo watazikwa kwenye makaburi ya Tosamaganga," alisema.

Pacha hao walifariki dunia wakiwa katika hospitali ya Iringa usiku wa kuamkia Jumamosi.

Kifo chao kiliwagusa wengi Tanzania, wengi wakituma salamu zao za rambirambi kupitia mitandao ya kijamii.

Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli, ambaye mapema mwaka huu alikutana na pacha hao, alieleza kusikitishwa kwake na vifo vyao.

"Nimesikitishwa na kifo cha Maria na Consolata. Nilipokwenda hospitali waliliombea taifa. Walikuwa na ndoto ya kulitumikia taifa," aliandika Rais Magufuli kwenye Twitter.

Maisha ya Maria na Consolata

Maria na Consolata Mwakikuti walizaliwa eneo la Ikonda, wilaya ya Makete kusini magharibi mwa Tanzania mwaka 1996.

Walisoma shule ya msingi ya Ikonda kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Maria Consolata na baadaye wakasomea hadi kidato cha sita katika shule ya Udzungwa wilaya ya Kilolo.

Septemba mwaka jana, baada ya kufaulu mtihani wa kidato cha sita, walijiunga na chuo kikuu cha kikatoliki cha Ruaha, Iringa.

Walianza kuugua maradhi ya moyo na Desemba wakahamishiwa taasisi ya maradhi ya moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam ambako walilazwa kwa miezi miwili.

Wamekuwa wakitatizwa na afya tangu wakati huo.

Walipofaulu mtihani wa kidato cha sita, walieleza furaha yao kuu baada ya kufaulu mtihani na kueleza ndoto zao.

"Tulipokea matokeo yetu tukiwa kwenye mazingira ya nyumbani tu, tukiendelea na shughuli zetu za kila siku, tukaambiwa matokeo yametoka na tumefanya vizuri, tulikuwa tukiwaza kabla ya hapo, unajua kwenye mitihani ya mwisho huwezi kujiamini sana," alieleza Consolata.

Huwezi kusikiliza tena
Pacha walioshikana Tanzania walikuwa na ndoto kuu

Walieleza sababu za kuchagua chuo cha Ruaha kwenye mkoa waliokuwa wanaishi tofauti na vyuo vingine au kama ilivyo kwa wanafunzi wengine ambao hupenda kubadili mazingira.

"Kwanza tunapenda mazingira ya Iringa, hatukutaka kwenda Dar es Salaam kwa sababu ya kwanza tunapenda kuishi pamoja na walezi wetu Masista waliokuwa wanatulea tukiwa wadogo na pili mikoa mingine ni mbali na tunapoishi. Pia ni kwa sababu kwa hali yetu tulivyo hatumudu kuishi kwenye mazingira ya joto. Mji wa Iringa ni baridi, hali hii tumeizoea.''

Walitaka kuolewa na mwanamume mmoja.

Maria na Consolata walikuwa wamewahimiza wazazi kuwajibika ipasavyo kwa watoto wao wenye ulemavu wakisema hakuna lisilowezekana.

"Wazazi washukuru Mungu kupata watoto wenye changamoto kama wao wasione kuwa na mtoto mlemavu ni laana. Pili wawaone kama watoto wengine na kuwapa mahitaji yao ya msingi, wawawezeshe, wawapatie nafasi ya kujiendeleza maana wakiwezeshwa wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri.''

Mapacha walioungana wakoje?

Mapacha walioungana huwa ni wachache sana kutokea au kuwepo ,katika watoto laki mbili wanaozaliwa kila mwaka anazaliwa mtoto mmoja tu wa aina hiyo.

Watoto wengi huwa hawawezi kuishi ,hufa mara baada ya kuzaliwa au mimba huharibika.

Watoto hawa uzaliwa katika uzao wa yai moja,hufanana na wana jinsia moja.

Kuzaliwa kwa watoto hawa huwa kuna hali ya kustaajabisha,kwa ujumla Watoto hao wanaweza kuishi wakizaliwa katika hali hiyo huwa ni kati ya asilimia 5 mpaka asilimia 25

Katika rikodi za historia zinasema kwamba mapacha wa kuungana wengi wanaoweza kuishi kwa muda mrefu ni wa kike,kwa asilimia 70

Mapacha walioungana wamegawanyika katika sehemu tatu

•73% wameunganika kuanzia kwenye kifua na tumbo

•23% wanakuwa wameunganika katika sehemu ya chini ya mapaja na miguu

•4% wanakuwa wameunganika kichwa

Mapacha walioungana waliowahi kuwa maarufu duniani

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mapacha Eng na Chang

Kwa miaka mingi mapacha walioungana wameendelea kuishi kutokana na matokeo ya tafiti nyingi zilizofanywa na majaribio mengi ya upasuaji yaliyofanyika

Mapacha wa kwanza wa kuungana waliojipatia umaarufu mkubwa duniani walijulikana kama 'siamese' majina yao yalikuwa ni Eng na Chang .

Mapacha hao walizaliwa mwaka 1811 waliweza kuishi kwa miaka 63 na kufanikiwa kupata watoto 22 kutoka kwa wadada wawili ndugu waliowaoa wakiwa na umri wa miaka 21,Chang alikuwa na watoto 12 na Eng watoto 10.

Walipozaliwa jamii ilitaka kuwauwa lakini kwa kudhaniwa kuwa wataleta mikosi na walioneka kuwa nio viumbe wa ajabu.

Mapacha wa kuungana na maisha yao ya ndoa

Katika karne ya ishirini,mapacha wa kuungana walikuwa wanazuiwa kuoa au kuolewa nchini Marekani

Na hii iliibua hisia za wengi pale ambapo wanamuziki ambao ni wacheza filamu wa nchi hiyo Daisy na Violet walipotaka kuolewa.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Daisy na Violet mapacha waliokuwa wacheza filamu

Watu wengi waliwaona kuwa maumbile yao hayawezi kuwaruhusu kuolewa au kupata wenza ingawa mapacha wenyewe wanajiona wamekamilika.

Kwa upande wa Chang na Eng ambao walifanikiwa kuoa, maisha yao ya ndoa yalikuwa na changamoto nyingi hasa pale ambapo wake zao walipoanza kugombana na kupelekea wake hao kuishi kwenye nyumba mbili tofauti.

Kwa maisha yao yote mapacha hao walikuwa wanaishi kwa mke mmoja siku tatu na mwingine siku tatu.

Vilevile mapacha kutoka Tanzania,Consolata na Maria ndoto yao kubwa baada ya shule ni kuolewa na mume mmoja.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii