Mabaki ya ndege iliotoweka na abiria 10 nchini Kenya yapatikana

Wataalam wa jeshi wanaoshiriki katika operesheni ya usakaji wa mabaki ya ndege hiyo katika msitu wa Aberdare
Maelezo ya picha,

Wataalam wa jeshi wanaoshiriki katika operesheni ya usakaji wa mabaki ya ndege hiyo katika msitu wa Aberdare

Mabaki ya ndege ya kampuni ya FlySax yaliopatikana katika eneo la Aberdares yameharibika vibaya kulingana na katibu wa idara ya uchukuzi Paul Maringa.

Kulingana na afisa huyo mabaki hayo ya ndege ya 208 Cesna yenye nambari ya usajili wa 5Y-CAC yalipatikana mwendo wa saa kumi na mbili alfajiri kufuatia operesheni kali ya usakaji wa ardhini uliotekelezwa na wataalam wa jeshi .

Kundi la wakokoaji wakiwemo madaktari watakaoshirikiana na maafisa wa msalaba mwekundu tayari limepelekwa katika eneo hilo.

Maelezo ya picha,

Baadhi ya maafisa wa uokoaji pamoja na waandishi habari katika msitu wa Aberdare

Hatma ya wafanyikazi wa ndege hiyo pamoja na abiria wanane ambao majina yao tayari yametangazwa na vyombo vya habari haijulikani.

Kreni mbili za angani kutoka katika ndege za jeshi na polisi zitaongoza juhudi za uokoaji baada ya hali ya anga kuimarika.

Ndege hizo mbili zitashirikiana na ndege zengine tano kuwabeba abiria na wafanyikazi wa ndege hiyo ambao hali yao haijulikani.

Ilitoweka kwa saa 36 na juhudi za kuitafuta siku ya Jumatano ziliathiriwa na hali mbaya ya anga.

Maelezo ya picha,

Baadhi ya maafisa wa usalama wanaoshiriki katika operesheni ya uokoaji wa ndege aina ya Flysax katika msitu wa Aberdare

Ndege hiyo inayodaoiwa kufanyiwa ukaguzi wa mitambo mara kwa mara ilikuwa imesafiri kuelekea Homabay na Maasai Mara mapema siku ya Jumanne kabla ya safari hiyo ya kuelekea Nairobi.

Marubani wake wawili waliripotiwa kuwa na uzoefu na inahofiwa kwamba ilipaa na kuingia katika eneo lenye hali mbaya ya anga juu ya mlima wa Aberdare katika eneo la Kinangop huko Nyandarua ambapo mawimbi yake ya simu yalipatikana mwendo wa saa kumi na moja jioni siku ya Jumatano.

Mara ya mwisho ya mawasiliano kati ya marubani wa ndege hiyo na mnara wa kudhibiti ndege uliopo katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi ni wakati ndege hiyo ilipokuwa umbali wa kilomita 60 kutoka Nairobi.

Ilitarajiwa kutua katika uwanja huo wa JKIA mwendo wa saa kumi na moja jioni kufuatia safari hiyo ya saa moja kutoka Kitale.