Pierre Nkurunziza asema ataachia madaraka 2020 Burundi

Rais Nkurunziza akiidhinisha marekebisho ya katiba
Maelezo ya picha,

Rais Nkurunziza akiidhinisha marekebisho ya katiba

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amesema kwamba hataomba kuchaguliwa tena baada ya muhula wake wa sasa kumalizika mwaka 2020.

Ametoa tangazo hilo akiwa eneo la Bugendana, Gitega ambapo alikuwa anaidhinisha katiba mpya ya nchi hiyo.

Mwezi uliopita, raia nchini humo walipiga kura na kuunga mkono kwa wingi marekebisho ya katiba ambayo yalifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo kubadilisha muhula wa rais kutoka miaka mitano kuwa saba.

Mwandishi wa BBC Bujumbura Ismail Misigaro amesema kwa sasa wengi wanatarajiwa kutakuwa na mabadiliko katika baraza la mawaziri karibuni.

Wengi waliamini Bw Nkurunziza ndiye aliyeshinikiza kufanyika kwa kura hiyo ya maoni ili kumpa fursa ya kuongoza taifa hilo hadi mwaka 2034.

Matokeo yaliyotolewa na tume hiyo yalionesha waliokuwa wanaunga mkono marekebisho hayo walikuwa 73.6%.

Waliokuwa wanapinga walikuwa19.3% ilhali kura 4.1% ziliharibika.

Asilimia 3.2 ya wapiga kura hawakuunga mkono upande wowote.

Wapiga kura zaidi ya 98% ya waliojiandikisha kuwa wapiga kura nchini humo hawakushiriki shughuli hiyo.

Rais wa Burundi walikuwa wanaamua iwapo muda wa muhula wa rais uongezwe kutoka miaka mitano hadi miaka saba, yenye kikomo cha mihula miwili.

Marekebisho hayo ya katiba yanamruhusu Nkurunziza kuwania uchaguzi wa mwaka 2020 na angeweza kuwania kwa mihula mingine miwili chini ya katiba mpya, kwani kuhesabiwa kwa mihula kungeanza tena baada ya mwaka huo.

Aliwania kwa muhula wa tatu mwaka 2015 hatua iliyozua utata na kusababisha msururu wa ghasia na jaribio la mapinduzi ya serikali.

Mamia ya watu walifariki na wengine 400,000 kukimbia nchi hiyo na kutorokea mataifa jirani.

Burundi imebadilisha katiba yake mara kadhaa miaka ya hivi punde.

Burundi ina historia ya machafuko tangu miaka ya 60, mabaya zaidi yakiwa ya miaka ya 90 ambapo vita vya wenyewe kwa wenyewe vilisababisha vifo vya zaidi ya watu 300,000.

Mkataba wa Amani uliotiwa sahihi Arusha ndio ulimaliza vita hivyo na kumwezesha Pierre Nkurunziza kuwa rais.

Alitarajiwa kuondoka madarakani mwaka 2015 lakini akaamua kuwania kwa muhula mwingine.