Matumizi ya nishati mbadala yanaweza kunusuru uharibifu wa mazingira Tanzania

  • Esther Namuhisa
  • BBC Swahili
Nishati mbadala wa mkaa
Maelezo ya picha,

Nishati mbadala ya mkaa

"Mama yangu nilimnunulia zawadi ya mtungi wa gesi lakini kila nikimtembelea nilikuta anatumia mkaa, nilipomuuliza kwa nini hatumii gesi ambayo ni rahisi na haraka, akaniambia anaogopa itaisha haraka na kwamba vipo vyakula kama maharage ambavyo hawezi kutumia gesi kwa sababu yanachukua muda mrefu. Aliniambia pia kuwa chakula kama wali huiva vizuri zaidi akitumia mkaa," anasimulia Samwel mkazi wa jijini Dar es Salaam.

Mama yake Samwel hayuko peke yake katika imani hiyo kuhusu mkaa na gesi, wapo wengi. Matembezi yangu katika Jiji la Dar es Salaam nilikutana na kina mama Samwel wengi, wenye kuamini zaidi katika matumizi ya mkaa badala ya gesi.

Majira ya jioni nikipita katika maeneo ya Msasani jijini Dar es Salaam niliwakuta vijana wanawasha majiko yao ya mkaa tayari kwa ajili ya kukaangia chakula maarufu kwa vijana mijini, chips, na kuchoma nyama maarufu kama mishikaki. Hawa pia wanaamini kwamba hakuna nishati zaidi ya mkaa wanayoweza kutumia katika kazi yao.

"Ha ha haaa sasa unadhani naweza kuchoma mishikaki kwa kutumia jiko la umeme au gesi, siwezi lazima nitumie mkaa," alisema Ahmed Juma, mchoma mishikaki jijini Dar es Salaam.

Chanzo cha picha, Imani Nsamila

Maelezo ya picha,

Nishati ya mkaa inatumiwa zaidi nchini Tanzania

Imani hiyo kuhusu nishati ya gesi au umeme, inadhihirisha uwepo wa watu wengi wanaotumia nishati ya mkaa au kuni kwa sababu ndio iliyo rahisi na inafahamika zaidi nchini kuliko nishati mbadala ambayo hawaifahamu.

Mkaa wa Idrisi

Pamoja na imani hiyo hasi dhidi ya nishati mbadala, wabunifu wameendelea kuibua nishati mbali mbali zinazoweza kutumika badala ya mkaa na kuni.

Chanzo cha picha, Mkaa wa Idris

Maelezo ya picha,

Mbunifu wa nishati ya mkaa mbadala

Idris Hamis, mkazi wa Tabora ni miongoni mwa wabunifu wa nishati mbadala, amepata umaarufu umaarufu kupitia mtandao wa kijamii kutokana na ubunifu wake wa mkaa mbadala.

Katika simulizi kuhusu ubunifu wake, anasema anapata soko la bidhaa zake kupitia mitandao ya kijamii, kwamba imemsaidia kuhamasisha watu waache kukata miti na kutumia mkaa mbadala.

Idris anasema mkaa wake anautengeneza kwa kutumia mabaki ya mazao pamoja na maranda ya mbao, zote hizo ni taka tunazotumia kila siku.

Idris ambaye taaluma yake ni sheria, anasema kilichomvutia zaidi kuingia katika ubunifu huu ni mapenzi yake katika mazingira, anatamani mazingira yaendelee kubaki kama yalivyokuwa awali, ukataji miti unamuumiza sana.

Amehamisika zaidi hadi kubuni nishati hiyo kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yanayoiathiri dunia hivi sasa.

Chanzo cha picha, Imani Nsamila

Maelezo ya picha,

Mkaa mwingi unaoingia Dar es Dar-e-salaam unatoka Tabora

"Tabora ni sehemu ambayo tunajivunia kwa asali lakini kukatwa kwa miti hiyo kunaweza kuleta athari kubwa sana katika jamii na hata hizo sifa za Tabora ni mkoa wa asali, Tabora ni mkoa wenye miti mikubwa sana ya miombo itapotea," Idris anaeleza.

Sifa kuu ya mkaa huo ambao ameupa jina lake la Idris, hautoi moshi na unaweza kupikia sehemu yeyote hata ndani ya nyumba.

Vile vile ni mkaa wenye gharama nafuu na unasaidia kusafisha mazingira kwa kuondoa mazalio ya mbu na kuwasaidia jamii kuwa katika mazingira mazuri.

Kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala

Maelezo ya picha,

Januari Mkamba akiwa katika maadhimisho ya siku ya mazingira

Asilimia 70 ya wakazi wa Dar es salaam wanapikia kwa kutumia nishati ya mkaa na kuni licha ya kwamba jiji hilo lina umeme karibu kila sehemu na gesi inapatikana kwa urahisi.

„Kila mwaka tunakata takriban ni hekari milioni moja ya miti ambapo ni takribani asilimia 70 za miti zinakatwa kwa ajili ya mkaa na kutokana na hilo asilimia 61 ya nchi yetu inakabiliwa na jangwa na hivyo utaona asilimia kubwa tatizo linatokana na matumizi ya mkaa," anasema January

Maeneo mengi unakotoka mkaa, wakazi wake hawatumii Mkoa wa Tabora ndio unaleta mkaa kwa wingi zaidi jijini Dar es salaam wakati wakazi wake hawatumii hiyo misitu.

Ubunifu na utafiti unabidi uendelee kupewa kipaumbele ili kuokoa misitu yetu.

Kwa sasa serikali inaona ni ngumu kuweka zuio moja kwa moja mpaka nishati hiyo ifahamike na wengi na ipatikane kwa bei nafuu.

Pamoja na udhibiti wa misitu katika hifadhi za taifa, bado wapo watu ambao huwa wanakata miti huko kwa ajili ya kutengeneza mkaa na kuuza kwa bei nafuu hivyo iwapo zuio la kukata miti na usafirishaji miti litawekewa mkazo basi nishati mbadala itaweza kusaidia.

Fazal Issa kutoka asasi ya kiraia ya Forum cc anasema tatizo la ukataji miti ambayo inatumika kwa ajili ya kupikia bado ni kubwa.

Mkaa ni gharama tumia nishati mbadala," ni kampeni ambayo imelenga kuleta hamasa kubwa ya mkaa mbadala ili kuondoa tatizo hili maana kumekuwa na makatazo mengi na sheria nyingi ambazo hazifanyiwi kazi.

Hamasa na ubunifu unahitajika ili kuondoa tatizo hili kuanzia kwenye taasisi za serikali na kwenye shule.