Makamu wa rais wa zamani wa DRC Jean Pierre Bemba aondolewa hatia ICC

Jean Pierre Bemba

Mahakama ya ICC imemuondolea makamu wa rais wa zamani wa nchini DRC Jean Pierre Bemba makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu ambayo alikuwa amepatikana nayo.

Alikuwa anatumikia kifungo cha miaka 18 jela kutokana na makosa hayo.

Bemba alikuwa amepatikana na hatia mwezi Machi mwaka 2016 kwa makosa ya uhalifu, uliotokea katika nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, kati ya mwaka 2002 na 2003 na akahukumiwa 21 Juni.

Mahakama hiyo imetoa uamuzi huo kufuatia rufaa aliyoiwasilisha kupinga hukumu hiyo.

Uamuzi wa mahakama umepokelewa kwa shangwe na wafuasi wake waliokuwepo ukumbi wa mahakama, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

Alilaumiwa kwa kushindwa kuwazuia waasi wake wasiwaue na kuwabaka watu.

Jaji leo amesema mwanasiasa huyo hawezi kulaumiwa kwa vitendo vya waasi hao.

Jaji Christine Van den Wijngaert pia amesema majaji waliomhukumu mwaka 2016 walikosa kuzingatia juhudi zake za kujaribu kuzuia uhalifu huo punde baada yake kufahamishwa kwamba makosa hayo yalikuwa yakitokea.

Kesi hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa ICC kuangazia ubakaji kama silaha wakati wa vita.

Aidha, ilikuwa mara ya kwanza kwa mshtakiwa kuhukumiwa kwa makosa yaliyotekelezwa na watu wengine waliokuwa chini ya mamlaka yake.

Reuters wanasema Bemba anatarajiwa kuendelea kuzuiliwa huku uamuzi ukisubiriwa kuhusu rufaa ya kesi dhidi yake ya kukaidi uamuzi wa mahakama.

Image caption Baadhi ya wafuasi wa Bemba walikusanyika kufuatilia uamuzi wa mahakama kupitia runinga Kinshasa

Akitoa hukumu mwaka 2016, Jaji Sylvia Steiner alikuwa amesema kuwa Bemba alishindwa kudhibiti waasi wake ambao walitumwa kwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Bemba alikuwa ametuma zaidi ya wapiganaji 1,000 kwenda nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, kumsaidia rais wa zamani Ange Felix Patasse, kukubiliana na jaribio la mapinduzi.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii