Mwezi waonekana: Waislamu kuadhimisha Siku kuu ya Eid ul-Fitr Ijumaa

Mwezi waandmwa katika maeneo tofauti ya Afrika mshariki

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mwezi waandmwa katika maeneo tofauti ya Afrika mshariki

Mabilioni ya Waislamu kote duniani Watasherekea siku kuu ya eid-ul-fitr siku ya Ijumaa baada ya kuandamwa kwa mwezi katika maeneo mbalimbali duniani.

hatua hiyo inaashiria kukamilika kwa mwezi mtukufu wa wa Ramadhan mwaka wa 1439 kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu.

Hapa Afrika Mashariki, viongozi wa kidini wametoa matangazo rasmi na kuondoa wasiwasi juu ya iwapo kesho ni siku ya eid.

Nchini Tanzania, Mufti wa taifa hilo Sheikh Abubakar Zuberi Bin Ally kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) ametangaza kuonekana kwa mwezi kwenye maeneo ya Rufiji, Pemba na Morogoro.

Wakati huo huo, kadhi mkuu nchini Kenya Sheikh Ahmed Mohdhar amedhibitisha kuunga kauli taarifa za kuandamwa kwa mwezi hivyo basi akawarai Waislaumu kufanya ibada kwa pamoja hapo Ijumaa.

Tayari, mapema wiki hii, serikali ya Kenya ilitenga siku ya Ijumaa kuwa likizo rasmi kwa watumishi wa umma kuwawezesha waumini wa kiislamu kuadhimisha siku hiyo.

Kwenye nchi jirani ya Uganda, Mkurugenzi wa sheria, katika baraza kuu la Waislamu nchini humo, UMSC, Sheikh Yahaya Ibrahim Kakungulu, naye ametoa tangazo rasmi lililopokewa kwa furaha.

Mataifa mengi duniani yakiongozwa na Saudi Arabia nayo yametoa matangazo ya aina hiyo huku waumini hao wakitarajiwa kuungana kwa pamoja kwenye ibada.