Watoto Tanzania kukaguliwa kubaini iwapo wamekeketwa

Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Jamii Bi Sihaba Nkinga alisema mwaka jana kuwa kiwango cha ukeketaji wa wasichana na wanawake Tanzania ni asilimia 32 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Jamii Bi Sihaba Nkinga alisema mwaka jana kuwa kiwango cha ukeketaji wa wasichana na wanawake Tanzania ni asilimia 32

Afisa mmoja mkuu wa serikali nchini Tanzania ametaka wataalamu wa afya kuwa wakiwakagua watoto kubaini iwapo wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa ukeketaji wakati wananapofanya uchunguzi wa kawaida.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile alisema hayo wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika iliyofanyika jijini Arusha, kwa mujibu wa taarifa ya wizara.

Alisema kuwa baada ya mangariba kuzuiwa kufanya ukeketaji kwa vijana wa kike sasa wamebadilisha mbinu zao na kuanza kuwakeketa watoto wachanga.

Naibu huyo wa waziri alisema Serikali itatoa waraka kwa waganga wakuu wa mikoa yote, watoto wanapopelekwa kliniki kupimwa afya, wafanyiwe ukaguzi ili kuwabaini kama wamefanyiwa vitendo vya ukeketaji.

"Kumeanzishwa mchezo wa kuanza kuwakeketa watoto wachanga, bahati nzuri hilo liko ndaniya uwezo wangu. Agizo langu kwa leo, kwamba serikali iandike, itoe waraka kwa waganga wakuu wote wa mkoa," alisema.

"Mtoto yeyote atakayebainika amekeketwa, wazazi husika watachukuliwa hatua. Jambo hili linawezekana na ni agizo na utekelezaji wake uanze mara moja," alisema, kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi.

Mkuu wa wilaya ya Arusha Fabian Daqaro aliunga mkono kauli hiyo na kusema: "Tusiangalie tu mtoto analishwa nini bali pia, namna ya kumlinda dhidi ya ukeketaji. Lazima tufanye hivi ili tuwasaidie na tusipofanya hivi hatuwezi kufanikiwa katika jitihada hizi."

Huwezi kusikiliza tena
Kwa nini ukeketaji wa wanawake haujaisha Tanzania?

Dkt Ndugulile akizungumza Jumatano alisema matukio ya ukatili wa jinsia ni mengi kuliko matukio ya ujambazi nchini Tanzania na ndio maana Serikali imeanzisha madawati 500 ya Jinsia kwa Jeshi la polisi kote nchini.

Kadhalika, serikali imeanzisha namba mpya simu ya 116 ambapo mtu yoyote ambaye amefanyiwa ukatili wa kijinsia anaweza kuitumia kupata msaada.

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika hufanyika 16 Juni kila mwaka kufuatia mauaji ya watoto zaidi ya 2,000 yaliyofanyika katika kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini mwaka 1976.

Watoto hao waliuawa na polisi wa serikali ya Makaburu ya wakati huo waliokuwa wanaandamana kupinga mfumo wa utoaji elimu wa kibaguzi uliokuwa unawakandamiza watoto wa Kiafrika.

Nchini Tanzania, serikali iliadhimisha rasmi siku hiyo Jumatano badala ya Jumamosi kutokana na kuwepo kwa shughuli nyingine za kitaifa Jumamosi na pia maadhimisho ya siku kuu ya Eid ul-Fitr.

Naibu waziri huyo alisema serikali pia imeanzisha madawati ya kamati ya ulinzi na usalama kwa wanawake na watoto katika ngazi ya Mkoa hadi Wilaya.

Lengo ni kuhakikisha haki zote za Msingi kwa watoto zinalindwa na kutekelezeka ili watoto watanzania waweze kushiriki kikamilifu katika Tanzania ya viwanda.

Huwezi kusikiliza tena
Miss.Tanzania apambana na ukeketaji nchini Tanzania

Wakati wa maadhimisho hayo Jumatano, naibu waziri huyo alizindua kamati ya ulinzi na usalama kwa wanawake na watoto mkoani Arusha na kuwakabidhi Mwongozo uliondaliwa na Wizara kama nyenzo ya kufanyia kazi kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Bi Sihaba Nkinga alisema Arusha ni miongoni mwa mikoa mitano yenye ukatili mkubwa kwenye eneo la ukeketaji.

Alisema haki kuu za watoto ni haki ya kusikilizwa, kuendelezwa, kuishi, kulindwa na kutobaguliwa.

Kwa mujibu wa serikali, Mkoa wa Manyara unaoongoza kwa asilimia 58, Dodoma (47), Arusha (41), Mara (32) na Singida (31) kwa ukeketaji.

Kwa nini imekuwa vigumu kukabiliana na ukeketaji?

Katika baadhi ya jamii Afrika Mashariki, ni utamaduni unaoathiri hadhi ya mwanamke katika jamii. Baadhi ya jamii, mwanamke haruhusiwi kuolewa au kutangamana na wasichana wengine wa rika lake iwapo hatapashwa tohara.

Katika jamii ya Wamaasai kwa mfano, mwanamke huwa na wakati mgumu kuthibitisha kwamba yeye ni mwanamke kamili iwapo hajapashwa tohara.

Aidha, watoto wake huchukuliwa na jamii kama wasiokubalika.

Sherehe ambazo huambatana na upashaji tohara na wazazi wa msichana kutambuliwa kama wazee katika jamii iwapo binti mabinti wao wamepashwa tohara huwafanya kutaka sana mabinti wao wakeketwe.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii