Israel yamshtaki waziri wake wa zamani Gonen Segev kwa kuipelelezea Iran

Israel yamshtaki waziri wake wa zamani Gonen Segev kwa kuipelelezea Iran
Image caption Israel yamshtaki waziri wake wa zamani Gonen Segev kwa kuipelelezea Iran

Israel imemuadhibu waziri wake wa zamani kwa kuipelelezea Iran. Idara ya ulinzi wa ndani Shin Bet imesema.

Gonen Segev, daktari aliyewahi kuhudumu kama waziri wa nishati miaka ya 1990, anadaiwa kusajiliwa na kampuni ya jinai ya Iran alipokuwa akiishi Nigeria.

Alitiwa mbaroni alipozuru Equatorial Guinea mwezi Mei kabla ya kusafirishwa kupitia ombi la polisi wa Israeli.

Segev mwenye umri wa miaka 62 alihukumiwa kifungo cha miaka mitano mnamo 2005 kwa kosa la ulanguzi wa madawa na kuunda pasipoti feki ya kidiplomasia.

Leseni yake ya kazi ilifutwa, lakini aliruhusiwa kufanya kazi kama tabibu nchini Nigeria, alipohamia mwaka wa 2007.

Taarifa iliyotolewa na idara ya Shin Bet mapema leo ilisema Segev alizuiliwa mwezi uliopita punde tu alipotua Israel.

Alichunguzwa kuhusu taarifa zilizodokeza kuwa huenda alifanya mawasiliano na maajenti wa jinai wa Iran na kusaidia mikakati yao dhidi ya Israel.

Wachunguzi walibaini kuwa Segev aliwasiliana na ubalozi wa Iran nchini Nigeria mwaka wa 2012 na kuongeza kuwa alizuru Iran mara mbili kukutana na wahusika wenzake, Shin Bet ilifafanua.

Imeongeza kuwa, Segev, alikutana na waajiri wake katika mataifa mengine na alipewa mitambo ya kisasa ya mawasiliano kumwezesha kutuma taarifa za kwa njia ya siri.

Shin Bet inadai kuwa Segev alitoa taarifa kuhusiana na sekta ya nishati ya Israel, Maeneo ya usalama ya taifa hilo, na kuhusu maafisa katika taasisi za kisiasa na usalama.

Aidha, Segev anadaiwa kuwaunganisha maafisa katika sekta ya usalama ya Israel na waajiri wake aliowatambulisha kama waekezaji.

Siku ya Ijumaa, Segev alihukumiwa katika mahakama moja Jerusalem kwa makosa ya "kumsaidia adui wakati wa vita na ujasusi dhidi ya taifa la Israel", pamoja na makosa mbalimbali ya "kutoa taarifa kwa adui".

Uamuzi wa kuzuia utoaji taarifa kuhusu kesi hiyo ilitolewa Jumatatu lakini taarifa zaidi zimezuiwa.

Mawakili wa Segev wamesistiza kuwa hukumu hiyo imeonyesha picha tofauti "Na kutofautiana na taarifa ya Shin Bett", Vyombo vya habari vya Israeli vimeripoti.

Tangu vuguvugu la kiislamu la Iran kuanzishwa 1979, ambapo viongozi wa kidini wenye misimamo mikali walipochukua hatamu, viongozi wa Iran wameitisha kumalizwa kwa Israel. Iran inapinga haki ya kudumu kwa Israel,na kuitambua kuwa mmiliki haramu wa ardhi ya waislamu.

Israel inaiona Iran kuwa tishio kwa kudumu kwake na imekuwa ikisema kuwa Iran isiweze kupata silaha za kinuklia.

Viongozi wake wanahofia upanuzi wa Iran Mashariki ya Kati.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii