Senegal yafufua matumaini ya Afrika kwa kuilaza Poland

'Sadio Mane hupiti' Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption 'Sadio Mane hupiti'

Hatimaye timu ya Afrika imepata ushindi kombe la dunia nchini Urusi baada ya Senegal kuifunga Poland 2-1.

Hii ni baada ya timu nyingine kutoka bara Afrika kupoteza mechi zao za ufunguzi.

Bao la M'Baye Niang kunako dakika ya 60 limeipa Senegal ushindi huo wa kihistoria na kuvunja rekodi ya Poland ya kutofungwa na mpinzani kutoka Afrika.

Senegal ilitangulia dakika ya 37 baada ya Thiago Cionek kuelekeza mkwaju wa Idrissa Gana Gueye langoni na kuwa mchezaji wa kwanza wa Poland kujifunga kombe la dunia.

Kipindi cha kwanza kilikamilika Senegal ikiongoza 0-1.

Niang alizidisha uongozi wa timu hiyo dakika ya 60 baada ya kurudi uwanjani kwa ruhusa ya refa Shukralla Nawaf. Aliingia kwa kasi na kuwahi pasi ya Grzegorz Krychowiak iliyokuwa ikimlenga kipa Wojciech Szczesny.

Mchuano ulichukua mkondo mwingine dakika ya 86 baada ya Grzegorz Krychowiak kuipa Poland bao lao la kwanza kwa kufunga mkwaju ulioletwa na winga wa Hull City Kamil Grosicki.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Lewandowsky akabwa

Goli hilo lilikaribia kuirejesha Poland kwenye mchezo lakini mabeki wa Simba wa Teranga walisalia kuwa makini.

Beki wa Senegal anayeichezea Napoli, Kalidou Koulibaly alimkaba Robert Lewandowski na kumlazimu asubiri hadi dakika ya 50 kabla ya kupata nafasi ya kulenga goli - kupitia frikiki.

Ingawa hakufunga goli, Sadio Mane aliisumbua safu ya nyuma ya Poland iliyoonekana kulemekwa baada ya beki wa kutegemewa Kamil Glik kukosa mchuano hu.

Kocha wa Senegal Aliou Cisse ambaye alishiriki kombe la dunia mara ya mwisho 2002 akiwa nahodha wa timu hiyo, alionekana kuchukua tahadhari na kuimarisha ngome ya timu yake.

Cisse, ambaye ni kocha mwenye umri mdogo kombe la dunia mwaka huu, kiungo wa West Ham Cheickou Kouyate na kumuondoa Alfred Ndiaye.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Poland hoi

Niang alituzwa kuwa mchezaji bora wa mechi kwa kuipa Senegal alama tatu muhimu.

Kufuatia matokeo hayo, Senegal wanashikilia alama sawa na Japan na kuwa viongozi wenza wa Kundi H.

Senegal itachuana na Japan kwenye mechi yake ya pili siku ya Jumapili 24/6/2018.

Ushindi huo umesherekewa na mamilioni ya mashabiki wakiwemo wachezaji wa soka wa zamani na wa sasa.

Wengi wanahisi kuwa Senegal itarejesha fomu iliyoiletea umaarufu mwaka wa 2002 walipofuzu hadi hatua ya robo fainali.