Mwanamume aliyetoweka nyumbani arudi na kukuta familia ikiomboleza mwili ikidhani ni wake

Mwili huo ambao bado haukuwa umetambuliwa ulirudishwa chumba cha kuhifadhi maiti.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Mwili huo ambao bado haukuwa umetambuliwa ulirudishwa chumba cha kuhifadhi maiti.

Mwanamume kutoka kijiji kidogo cha Santa Teresa nchini Paraguy alirudi nyumbani baada ya siku tatu na kugundua kuwa familia yake ilikuwa ikiomboleza mwili ambao ilidhani ni wake.

Juan Ramón Alfonso Penayo, 20, alikuwa ameonekana mara ya mwisho siku ya Alhamisi akiondoka nyumbani kwao karibu na mpaka wa Brazil.

Eneo hilo linakumbwa na mzozo mkali kati ya magenge ya madawa ya kulevya, na wakati Bw Panyao hakurudi nyumbani familia ilidhani alikuwa amekumbwa na maafa.

Wakati polisi walipata mwili uliokuwa na majeraha mbaya siku ya Jumapili familia iliamua kuwa ulikuwa ni wake.

Familia iliandaa mazishi kijijini lakini Bw Penayo alitokea ghafla na kuwapata wakiomboleza mwili uliokuwa kwenye jeneza wakidhani ni wake.

Baada ya Bw Paneyo kurudi mwili huo ambao bado haukuwa umetambuliwa ulirudishwa chumba cha kuhifadhi maiti.

Haijulikani Bw Penayo alikuwa wapi au alikuwa anafanya nini wakati wa siku hizo tatu ambazo hakuwa hajulikani yuko wapi.