Wabunge wa Tanzania wamepimwa HIV katika vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi

Waziri wa Afya Tanzania Ummy Ali Mwalimu ni miongoni mwa waliotangulia kupimwa HIV mjini Dodoma asubuhi hii
Maelezo ya picha,

Waziri wa Afya Tanzania Ummy Ali Mwalimu ni miongoni mwa waliotangulia kupimwa HIV mjini Dodoma asubuhi hii

Wabunge nchini Tanzania wamefanyiwa vipimo vya virusi vya Ukimwi huko mjini Dodoma ikiwa ni jitihada za viongozi hao kuishi kwa mfano katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Mbali na vipimo vya hiari, wabunge hao pia watakuwa na shughuli mbali mbali kama njia moja wapo ya kuunga mkono jitihada za serikali katika kampeni yake ya upimaji virusi vya ukimwi nchi nzima imezinduliwa na Waziri mkuu Kassim Majaaliwa.

Kwa mujibu wa takwimu za serikali takriban watu milioni 1.4 wanaishi na virusi vya ukimwi lakini ni asilimia 52 tu walio na ufahamu kuhusu hali zao.

Serikali imeidhinisha kampeni ya miezi sita inayonuiwa kuwatibu watu wanaoishi na virusi vya HIV kwa dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo (ARVs).

Maelezo ya video,

Je ni wabunge wote Tanzania wanaopimwa HIV

Zaidi ya wabunge 300 wa Tanzania wanatarajiwa kutoa mfano mwema kwa kujipima hadharani katika makao ya bunge Dodoma.

Tayari waziri wa afya nchini Ummy Ali Mwalimu , spika wa bunge Job Ndugai pamoja na viongozi wengine wametangulia kupimwa asubuhi hii.

Mwenyekiti wa kamati ya bunge inayohusika na masuala ya HIV, Bw Oscar Mukasa, amesema kuwa kundi hilo litaandaa shughuli kadhaa kuunga mkono kampeni ya serikali ya nchi nzima ya kupima virusi vya HIV, wakati wa kampeni iliyozinduliwa na waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa siku ya Jumanne.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Kampeni hiyo ilizinduliwa na waziri mkuu Kassim Majaliwa (picha maktaba)

Kampeni hiyo inayofahamika kama 'Furaha Yangu' inafanywa kwa ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na shirika la maendeleo ya kimataifa la Marekani la USAID, mradi ya afya wa Tugole na washikadau wengie katika sekta ya afya.

Kati ya shughuli zingine ambazo zitachukuliwa na bunge kwa mujibu wa Bw Mukasa ni pamoja na kongamano kuhusu wajibu wa viongozi katika kupambana na virusi vya ukimwi.

Maelezo ya picha,

Spika wa bunge Job Ndugai na viongozi wengine tayari wamepima

Pia kutakuwa na maonyesho kuhusu shughuli zinazofanywa na mashirika yasiyo ya serikali katika kupambana na virusi vya ukimwi kuanzia Ijumaa hadi Jumamosi.

Kwa mujibu wa tume ya kupambana na ukimwi Tanzania (TACAIDS), virusi vya ugonjwa huo vimewaathiri zaidi vijana wa kati ya miaka 14 hadi 25.