Maofisa wa wizara ya uvuvi wazua gumzo Tanzania

Anayepima samaki kwa rula ni kaimu wa meneja wa uhifadhi bahari na maeneo tengefu ,wizara ya mifugo na uvuvi ,John Komakoma akiwa pamoja na maofisa wengine

Chanzo cha picha, Twitter

Maelezo ya picha,

Anayepima samaki kwa rula ni kaimu wa meneja wa uhifadhi bahari na maeneo tengefu ,wizara ya mifugo na uvuvi ,John Komakoma akiwa pamoja na maofisa wengine

Mjadala mkali umeibuka katika bunge na mitandao ya kijamii nchini Tanzania baada ya maofisa wa wizara ya mifugo na uvuvi kuingia katika mgahawa wa Bunge na kubaini kuwa samaki waliokuwa hapo wamevuliwa kwa njia haramu.

Samaki hao walibainiwa kuwa wamevuliwa kwa uvuvi haramu ulidhihirishwa kwa vipimo vya rula.Picha ya maofisa hao walipokuwa wakipima samaki wakiwa katika mgahawa ilisambaa mitandaoni na wengine kuigiza kile ambacho maofisa hao walichokuwa wakikifanya.

Chanzo cha picha, Facebook

Maelezo ya picha,

Upimwaji wa samaki waliopikwa wazua mjadala Tanzania

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi nchini Tanzania Maofisa walikamata samaki kilo mbili waliokuwa na urefu wa chini ya sentimita 25 kati ya samaki 100 waliokuwa wamevuliwa kutoka Ziwa Victoria katika mgahawa huo wa bunge.

Licha ya kuwa mmiliki alikiri kosa na kudai kuwa alikuwa hajui au ingekuwa ni vigumu kwake kubaini kosa lile,bado alitozwa faini ya kulipa shilingi laki tatu ambayo ni sawa na dola 133.

Chanzo cha picha, Mtandaoni

Maelezo ya picha,

Maofisa wa wizara ya uvuvi wazua gumzo Tanzania

Baada ya hatua hiyo kufanyika na maofisa wa uvuvi ,baadhi ya wabunge walilalamikia usalama wao na hata hatua ya maafisa wa serikali kuwanyanyasa wananchi huku wengine waliliona jambo hilo kuwa la aibu kwao na wameshindwa kuheshimiwa hivyo wizara husika inapaswa kukaa na kupata uamuzi.

Chanzo cha picha, Twitter

Maelezo ya picha,

Baadhi ya picha zilizosambaa mitandaoni

Yaliyojiri mitandaoni

Hatua ya kupima urefu wa Samaki waliopikwa yaibua maswali mengi, je anapoandalia hakuna urefu unapungua?! akichemshwa hapungui urefu?samaki wanaofugwa kwenye mabwawa hutambulika vipi ? Hii hatua sio shambulio kwa wafuga samaki? Hakuna ubunifu mwingine zaidi ya huu?!

Wavuvi na walaji wa samaki sasa kitoweo hicho bila kupima kwa tepu au rula kabla ya kuvua au kula jamuhuri itakuhusu.Tanzania ya nyerere ipo wapi!

Tanzania tunakoelekea ni huku wavuvi kuanza kuvua wakiwa na rula au futi kamba kuwapima kimo samaki

Tunatembea na Tape measure kupima samaki urefu nchi jirani wanavua mpaka mayai... itakuwa binadamu wa kwanza hapa Tanzania alifanya kosa tukalaanika wote

Only in Tanzania bajeti mbadala ya upinzani inazuiwa kusoma ndani ya bunge but upimaji wa samaki na rula unapata nafasi ya kujadiliwa ndani ya bunge km jambo la dharuraa #ufalme umefitinika

Maelezo ya picha,

Ziwa Victoria

Pamoja na kwamba njia hiyo ya kudhibiti uvuvi haramu katika mgahawa imeleta taharuki kwa wengi.

BBC imefanya mahojiano na mtaalamu wa masula ya uvuvi na samaki (Jina tunalihifadhi) na yeye alisema kwamba katika taaluma ya bahari ,wataalamu wanaweza kujua kipimo cha samaki na hata umri ambao samaki anaoweza kuishi na kuliwa.

Kupima samaki si jambo geni katika taaluma yao ingawa awali walikuwa wanapima kwa wavuvi na walikuwa hawaendi kwenye mgahawa.

Kwa mfano samaki aina ya sato anapaswa kuvuliwa akiwa na uzito wa nusu kilo.

Kuna vipimo vya kuvulia samaki kulingana na aina ya samaki na kulingana na wavu.

Uvuvi unategemea wavu hivyo kama wavu mdogo na umevua samaki mvuvi anapaswa kunyang'anywa leseni ya kazi yake.

Kumekuwa na operesheni inayoendelea ili kuzuia wavuvi haramu ingawa mara nyingi inakuwa ngumu kuwakamata na athari inaendelea kuepo,hivyo wakizuiwa wanunuzi na walaji basi uvuvi haramu utaisha.

Mtaalamu huyo alidai kuwa jambo hilo ni sahihi kiutendaji ili kulinda viumbe hivi visipotee na kuharibiwa ni jukumu la serikali na mtu mmoja mmoja kupinga uvuvi haramu na matumizi ya bidhaa hizo kuna wakati Mwanza samaki wa sangara walipotea.

Utafiti mpya unaonyesha kwamba robo tatu ya aina zote za viumbe hai waishio kwenye maji yasiyo ya chumvi katika Ziwa Victoria lililopo Afrika Mashariki wamo hatarini ya kuangamia kutokana na uchafuzi wa mazingira na uvuvi uliopindukia.

Hiyo inatishia maisha ya takriban watu milioni 42 wanaoishi Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi.

Wahifadhi wa Mazingira wanatoa wito kwa matumizi bora ya ardhi na maji ya ziwa hilo kubwa zaidi za Afrika.

Utafiti huo wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Uasilia (IUCN) unaonesha asilimia 20 ya aina zote za viumbehai waliozingatiwa kwenye utafiti huo walibainishwa kuwa kwenye hatari ya kuangamia.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wavuvi wanaovua dagaa wana kipimo maalum tofauti na wavuvi wengine

"Samaki kupimwa kwa rula upo tangu zamani, ni dagaa peke yake ndio hawapimwa kwa njia hiyo maana wanaweza kukaa zaidi ya miaka 10 bila kukua"mtaalamu aeleza.