Mtalii anusurika baada ya kumpapasa Simba Serengeti, Tanzania

Simba akiashiria kuwa tayari kwa mashambulizi

Chanzo cha picha, WILDLIFE SIGHTINGS

Maelezo ya picha,

Simba akiashiria kuwa tayari kwa mashambulizi

Mtu mmoja ameelezwa kuwa ''mtalii mjinga ambaye hajapata kutokea'' baada ya kutoa mkono wake na kumpapasa Simba Tanzania.

Picha za video za tukio hilo la ajabu zilionyesha mwanaume huyo akipapasa manyoya ya simba huku akipiga picha kwa kutumia simu yake ya mkononi katika hifadhi ya taifa ya Serengeti nchini Tanzania.

Simba aligeuka haraka akatazama dirisha lililo wazi, kisha akanguruma ishara kuwa yuko tayari kushambulia, watalii waliokuwa ndani ya gari waliruka na kuharakisha kufunga kioo baada ya sauti iliyosikika ikipayuka ''funga kioo''

Picha hizo zilitolewa kwenye mtandao wa Youtube ukiwa na jina ''Watalii wajinga kupata kutokea'' Watu wengi wakikosoa kilichofanywa na watalii hao.

Inaaminika kuwa simba ambaye awali alionekana kwenye video alikuwa karibu na gari ya watalii akitafuta kivuli.

Chanzo cha picha, WILDLIFE SIGHTINGS

Maelezo ya picha,

Watalii walihatarisha maisha yao kwa kumpapasa simba manyoya

Katika Video hiyo iliandikwa: ''Simba mara kadhaa hutumia magari kupata kivuli kama eneo halina miti, lakini haina maana kuwa simba wanawaamini binaadamu".

"Kujaribu kuwashika ni jambo la kijinga sana lililofanywa na watalii hao".

Mlinzi wa mbuga nchini Afrika Kusini Naas Smit aliliambia jarida la The Sun kuwa ''Wanaofanya kazi kwenye mbuga wanafahamu kasi ya simba na angeweza kujeruhi mkono wa mtu aliyemgusa.

''Angekuwa na nguvu za kuwavuta watalii kupitia kwenye dirisha na kuwaua papo hapo mbele ya marafiki zao lilikuwa jambo la kijinga sana kufanya''.

''Ilikuwa bahati sana walinusurika simba ni wanyama hatari sana''

''Kama simba angemuua mtu kwenye eneo hilo askari wangepaswa kumuua simba hasa kama angakuwa dume, vinginevyo kungekuwa na madhara makubwa," alieleza Smit.

Uliitazama hii ya duma aliyeingia gari la watalii Tanzania?

Maelezo ya video,

Duma 'awajulia hali' watalii kwenye gari Tanzania