Tanzania: Kinana aipatia CCM siri tatu za kusalia uongozini

Aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha CCM Abdulrahman Kinana

Chanzo cha picha, Kinana/Facebook

Maelezo ya picha,

Aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha CCM Abdulrahman Kinana

Aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha mapinduzi nchini Tanzania CCM, Abdulrahman Kinana amewaaga wabunge wa chama hicho, huku akiwaachia wasia kuhusu vitu vitatu ambavyo wanafaa kufanya ili kuleta amani miongoni mwa Watanzania.

Ameyataja mambo hayo matatu katika sherehe ya kumuaga ilioandaliwa na wabunge hao huku wakimkaribisha rasmi katibu mkuu mpya wa chama hicho Bashiru Ally.

Kwa mujibu wa gazeti la The Citizen nchini Tanzania, anasema kuwa CCM imekuwa na baadhi ya makatibu wakuu walioondoka .

''Nilitumia uwezo wangu wote kujitolea kufanya kazi kwa bidii na kutumia uzoefu wangu ili kuhudumu.Ninyi ndio mahakimu wangu, je nilifanya kama ilivyohitajika?

Kinana aliendelea kusema kwamba iwapo kuna matatizo yoyote basi yalikuwa yake.

Na iwapo kulikuwa na ufanisi basi ulitokana na ushirikiano wa wanachama wote wa CCM na wabunge. CCM sio chama cha viongozi, ni chama cha wananchi.

Chama chetu bado kina nguvu, kinapendwa na kuheshimiwa ndani na nje ya mpaka wetu.

''Chama kiko sawa kilivyo'', Kinana alisema.

Amesema kile kilicholeta ufanisi katika chama na kile ambacho kinafaa kuendelea kutekelezwa ni mambo matatu.

''Tunafaa kutekeleza ahadi tulizotoa kwa raia kwa kuwa ziko katika manifesto yetu, kujiandaa kwa chaguzi ndogo na kujiandaa kwa uchaguzi mkubwa.

Aliongezea: Iwapo serikali itatekeleza ahadi ilizotoa kwa wananchi , wananchi wataendelea kuiamini. Na iwapo serikali itaangazia matatizo yanayowakumba wananchi watahisi kufarijiwa na mutaendelea kuchaguliwa kwa idadi kubwa. Na mwisho wa siku CCM itaendelea kuongoza.