Mwani unavyowapa furaha wanawake Zanzibar, na kukabili mabadiliko ya tabia nchi

Sihaba na Hifadhi ni wakulima wa mwani Zanzibar
Image caption Sihaba na Hifadhi ni wakulima wa mwani katika kikundi cha Furahia Wanawake Zanzibar

Majira ya saa 12 asubuhi nakutana na akina mama wakiwa wamebeba kamba zenye rangi ya njano zikiwa zimefungwa pamoja na kamba za kijani, wamejitwika kichwani mizigo ya vijiti kama kuni wakielekea baharini.

Wengine wakiwa wamefika tayari wanakoelekea, muonekano wa eneo hilo ni sawa na shamba katika bahari.

Unaweza kudhani ni mpunga uliopandwa katika bahari, lakini la hasha ni mwani, kwa Kiingereza seaweed au macroalgae.

Na asubuhi ya leo wamefika wakulima wengi wa zao hilo hapo kwa sababu maji yametoka.

Image caption Wakulima wa mwani wakielekea shambani

Kilimo hicho, wanasema hutegemea kupwa na kujaa kwa maji baharini.

Furahia Wanawake, ndilo jina la kikundi cha wanawake hao wapatao 30 wanaolima mwani pembezoni mwa bahari katika kijiji cha Paje kilichopo Kusini mwa Kisiwa cha Unguja.

Mwanaisha Makame ni miongoni mwa wanawake hao ambao wote wamevalia nguo zilizowafunika juu mpaka chini. Anasema siku hizi, kilimo cha mwani ni cha kubahatisha, kuna wakati unapita mwezi mzima bila kulima.

"Jua limekuwa likiathiri sana kilimo chetu ,hivyo unakuta miezi miwili tunalima na mwezi mzima tunashindwa kulima kwa sababu kila tukipanda mwani wakati wa jua mwani unaungua," anaeleza Mwanaisha.

Changamoto wanayopitia wanawake hawa kwa sasa si jambo geni kwao na pengine hivi sasa kuna unafuu.

Wanawake hawa wanasema kuwa mwaka 2006, mwani ulianza kupotea na ilipofika mwaka 2010 hadi mwishoni mwa mwaka 2014 mmea huo wa mwani ulipotea kabisa katika visiwa vya Zanzibar na kusababisha wakulima wa mwani kupungua kutoka 400 hadi 150.

Image caption Jua kali linaathiri ukuaji wa mwani

Riziki Juma ni miongoni mwa wakulima wa mwani walioacha kabisa kilimo hicho.

Yeye aliacha ukulima huo yapata miaka miwili sasa, baada ya mwani kupotea kwa kipindi cha miaka mitatu.

Mwani ni wa msimu

"Mwani ulikuwa unanifaidisha lakini sasa nnakaanga sambusa na samaki. Shida ya mwani una msimu, kuna wakati wa mvua mtu unahangaika sana kupanda lakini jua likija linaharibu hivyo faida yake ni ndogo kama huna biashara ya kujishikiza," anasema Riziki.

Riziki aliongeza kuwa gharama ya kulima mwani ni kubwa na mwisho wa siku unaweza usipate faida.

Kilo ya mwani ni kati ya shilingi 600 na 1,000 za Tanzania, haufiki hata ya dola moja ya Kimarekani.

Licha ya changamoto ya uzalishaji mwani visiwani humo, bado Zanzibar inatajwa kuwa nchi ya tatu duniani kwa kuzalisha zao hilo kwa wingi na ubora.

Waziri wa Biashara wa Serikali ya Zanzibar, Balozi Amina Salum anasema awali walikuwa hawajui matumizi ya mwani, lakini hivi sasa hali ni tofauti, matumizi yake yanafahamika, kwamba hutumika kutengeneza bidhaa mbali mbali.

Image caption Waziri wa Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Amina Salum

Hata kama mauzo yake yapo chini, bado unaweza kutumika visiwani humo humo kutengeneza bidhaa zake badala ya kutegemea kuuza mwani wenyewe.

Badala ya kuuza mali ghafi sasa tunaweza kutengeneza bidhaa kutoka kwenye mwani na kutumia humu nchini.

Kwa sasa tuko kwenye hatua za mwisho za kutengeneza chapa ya kitaifa ya kutengeneza sabuni, vitendea kazi tayari tuko navyo kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Ustawi wa Viwanda (UNIDO).

Image caption Sabuni za mwani kutoka Zanzibar

Kuna sifa nyingi ambayo sabuni ya mwani inasifiwa, ni nzuri kwa watoto, wanawake na wanaume wakati wa kunyoa ndevu maana inafanya ngozi kuwa nyororo.

Takriban asilimia 90 ya wanaolima mwani ni wanawake na wengi wao hawana elimu hivyo jitihada zinachukuliwa hivi sasa kuwawezesha kupata utaalamu kwa kuwaleta wataalamu kutoka nje kuwafundisha.

"Tunataka kujipanga kutengeneza karajina (mwani uliosagwa) hapa ili waweze kununua hapa badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi ," Waziri balozi Amina. .

Mwani ni pesa, Mwani ni chakula na mwani ni zawadi kutoka kwa Mungu

Image caption Bi Mwanaisha Makame, akipika chakula ambacho kinatumia kiungo cha mwani

Hiyo ni misemo ambayo wakulima wa mwani bado wanayo katika visiwa hivyo vya Zanzibar, lakini je, misemo hiyo ina ukweli wowote wakati hali ya hewa inazidi kuiathiri mimea hiyo?

"Kwa sasa naweza kutumia mwani kutengeneza vitu mbalimbali kama vyakula, juisi, chachandu, pilipili, kachumbali, chipsi (viazi karai), tambi, chaulo, visheti, cake, pipi, jam ya matunda, sabuni, shampoo na mafuta ya kupaka na nywele," Safia Hashim.

Image caption Bi Safia Hashim akiwa nje ya nyumba yake ambayo aliijenga kutokana na mapato ya mwani

Safia Hashim ni miongoni mwa wanawake waliofaidika sana na kilimo cha mwani visiwani Zanzibar, sasa hivi anamiliki nyumba na aliwanunulia watoto wake boti.

Safia anasema alipata mafunzo ya miezi mitatu kutoka kwa mtaalamu kutoka Indonesia na sasa anaendelea kupata mafunzo na yeye pia anatoa mafunzo katika maeneo mbali mbali visiwani humo.

Sihaba Mustafa ni miongoni mwa wakulima wa mwani ambaye aliathirika sana kiafya kipindi mwani ulipoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa, lakini pamoja na misukosuko aliyokutana nayo katika kilimo hicho, hakukata tamaa.

"Zamani tulikwa hatujui thamani ya mwani lakini sasa hivi tunajua kuwa mwani una matumizi chungu nzima na umeanza kutufaidisha," anasema.

"Kutengeneza bidhaa kumeleta matumaini mapya na tunawafundisha hata watoto wetu, tunaona faraja ya kilimo hichi licha ya changamoto ya hali ya hewa inayotukabili. Kuna wataalamu wengi wa sayansi hivyo bado tunaamini kwamba suluhisho tutalipata."

Image caption Wakulima wa mwani wanaojifunza kuogelea katika kijiji cha Mungoni Zanzibar

Huku wataalamu wa sayansi ya bahari wakiendelea na utafiti, pia wanajaribu kutafuta mbinu mbalimbali za kukomboa kilimo hicho.

Dkt Narman Jawad anasema kilimo cha mwani kikikoma kitawaathiri sana wanawake na ndio maana wameanza kutafuta namna nyingine ya kuwafaidisha wakulima kwa kutafuta mbinu mpya za kulima katika maji mengi.

Flower Msuya ambaye ni mtafiti wa mwani yeye anasema kilimo cha mwani kina soko kubwa sana Zanzibar.

Mwani ni wa pili kuingiza fedha za kigeni Zanzibar, kilimo cha zao hilo kina manufaa makubwa sana kwa wanawake wa visiwa hivyo kwa kuwa kimeboresha maisha ya wengi.

"Katika utafifi wetu tumebaini kuwa mwani unaoitwa cottonie unaweza kulimwa kwenye maji mengi na ndio mwani bora zaidi

Hivyo tunatumia tuber note kulima mwani huo, njia hiyo inatumia neti na bomba kupanda mwani kwenye bahari badala ya vijiti.

Baada ya kulima mwani katika maji ya kina kifupi inabidi tubadili namna ya kulima mwani kwenye kina kirefu na tumeshaona joto sio jingi kiasi hicho katika maji mengi na hizi tekinolojia tumeanza kuwapa watu," Dkt Flower alieleza .

Wanawake wanaolima mwani, hivi sasa, wanajifunza kuogelea ili waweze kulima mwani katika maji mengi bila changamoto.

Jina ni miongoni wa wakulima hao aliyeanza kulima mwani katika maji mengi. Anasema: "...ninafurahia sana kujifunza kuogelea, ndio hivyo hivyo tunajifuza taratibu kuogelea na sasa ni takribani miezi minane tumeanza kulima mwani katika maji mengi."

Kuna mwani aina mbili unaolimwa Zanzibar

Kotonii na spinosam

Image caption Mwani aina ya spinosamo ukiwa umekaushwa
Image caption Mwani aina ya Kotonii

Kotonii ni nzito na ambayo kilo moja huuzwa shilingi 1,000 za Kitanzania na imekuwa ni ngumu kuota wakati spinosam inauzwa bei rahisi, shilingi 500 na ndio inayoota katika vijiji vingi kisiwani humo.

Mwani umebadili mtazamo wa tamaduni ya Zanzibar

Image caption Hifadhi Makame mwenye watoto saba ambao wote wanalipiwa ada kutokana na fedha za mwani

Mwani umebadilisha mtazamo sio tu kiuchumi lakini hata kitamaduni piavisiwani Zanzibar.

Awali wanawake wa Zanzibar walikuwa hawatoki nje na walikuwa wanatarajia mume ndio alete kila kitu nyumbani.

Mwanzo ulikuwa mgumu maana kuna baadhi ya wanawake walikuwa wanapata vitisho hata vya kuachwa na waume zao lakini baadaye hali ilibadilika waume zao walipoanza kuona maabadiliko ya kipato wanachokipata na kusaidia familia.

Mohamed Mzale ambaye ni miongoji mwa wahamasishaji jamii katika Kijiji cha Paje, kisiwani Unguja, anasema kuwa zamani alikuwa anaona ugumu kumuachia mke wake kwenda kulima mwan.

Alihisi watoto walikuwa wanateseka na mke wake alikuwa hapati muda wa kupumzika.

"Mwanzoni ilikuwa vigumu sana maana kuruhusu mke kwenda baharini mahali ambapo kuna wavuvi wengi haikua rahisi," anasema.

"Hivi sasa wanawake hao wanajua kupangilia muda wa kwenda kulima mwani na wana kituo maalum cha kulelea watoto wao wakati wanapokuwa hawapo na ninawaunga mkono kwa juhudi zao."

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii