Trump asema Korea kaskazini bado ni 'tishio kubwa'

Donald Trump and Kim Jong-un walk beside each other at the Capella hotel in Singapore Haki miliki ya picha KEVIN LIM / THE STRAITS TIMES / HANDOUT

Rais wa Marekani Donald Trump ameidhinisha upya vikwazo dhidi ya Korea kaskazini akitaja taifa hilo kuwa 'tishio liliso la kawaida' kutokana na silaha zake za nyuklia - siku 10 tu baada ya kutamka kwamba hakuna hatari yoyote kutoka kwa Pyongyang.

"Hakuna tena tishio kutoka Korea kaskazini," alituma ujumbe mnamo Juni 13, siku moja baada ya kukutana na kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong-un huko Singapore.

Hatua hiyo imekuja wakati Marekani na Korea kusini zimefutilia mbali mazoezi mawili ya pamoja ya kijeshi.

Wizara ya ulinzi Marekani Pentagon imesema lengo ni kuunga mkono majadiliano ya kidiplomasia.

Inafuata uamuzi wa mapema wiki hii kusitisha mazoezi makubwa ya kijeshi ya pamoja katiya Marekani na Korea kusini yaliopangwa Agosti.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wanajeshi wa Marekani na Korea Kusini wanafanya mazoezi mnamo Aprili 2017

Rais Trump ameahidi kusitisha 'uchokozi wa kivita' wa kila mwaka kati ya washirika katika hatua ambayohaikutarajiwa kwenye mkutano wake na Kim, akiutaja kuwa "uchokozi" na "ulio na gharama kubwa".

Hilo limezusha mshtuko kwa wengi, kutokana na kuwa katika siku za nyuma Marekani imelalamika kuwa mazoezi hayo ni ya ulinzi tu na yalio muhimu kwa muungano wake wa kijeshi na Seoul.

Je Trump amebadili msimamo wake kwa Korea kaskazini?

Ndivyo inavyoonekana, lakini Marekani imekuwa na 'hali ya dharura kitaifa' iliyoidhinishwa kuhusiana na Korea kaskazini tangu 2008.

Tangu hapo marais wamekuwa wakiidhinisha hali hiyo kuendelea mtawalia na vikwazo dhidi ya Pyongyang.

Rais Trump aliendeleza hali hiyo ya dharura Ijumaa kutokana na 'uwepo wa hatari ya kuongezeka kwa silaha katika rasi ya Korea na hatua na sera za serikali ya Korea kaskazini'.

Haki miliki ya picha AFP

Haya "yanaendelea kuzusha tishio lisilo la kawaida kwa usalama wa kitaifa, sera ya nchi za nje na uchumi wa Marekani", alisema katika taarifa kwa bunge.

Wanachama wa Democratic wanasema tamko la sasa kutoka ikulu ya White House linakwenda kinyume na majigambo ya awali ya rais Trump kuhusu ufanisi wa mkutano wa Singapore.

Katika mkutano huo wa kihistoria kati ya rais wa sasa wa Marekani na kiongozi wa Korea kaskazini Viongozi hao walisaini taarifa ambapo Marekani iliahidi usalama kwa KOrea kaskazini na mwenzake akaahidi "kushughulika kusitisha mipango ya nyuklia katika rasi ya Korea" - pasi kufafanua maana ya ndani ya makubaliano hayo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema kuwa vikwazo dhidi ya Korea kaskazini vitasalia wakati majadiliano yanaendelea kuhusu silaha zake za nyuklia.

Hatahivyo, vyombo vya habari Korea kaskazini vimeripoti kuwa Trump alikubali 'kuondosha vikwazo' wakati uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ukiendelea.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii