Tanzania kutumia teknolojia ya kisasa kuwalinda faru Serengeti

Faru Malelane 30 September 2004 Haki miliki ya picha AFP

Serikali ya Tanzania imeanza kutumia teknolojia kuwafuatilia faru katika mbuga ya taifa ya Serengeti ili kukabiliana na uwindaji haramu.

Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa) linashiriki katika mpango wa kuweka faru kifaa cha kidijitali kwenye pembe.

Kifaa hicho kitakuwa kikitoa maelezo kuhusu mwenendo wa faru maeneo wanamokwenda.

Mradi huo ambao utagharimu dola 111,320 za Kimarekani (Sh253m) unatekelezwa kwa ushirikiano wa maafisa wa TANAPA, maafisa wa Shirika la Wanyama la Frankfurt (FZS) na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori ya Tanzania (Tawiri).

Mradi huo umefadhiliwa na Mfuko wa Uhifadhi wa Friedkin Tanzania (FCF).

Kufikia sasa, faru 21 wamewekwa kifaa hicho kilicho na mitambo ya kisasa zaidi ya kuwafuatilia wanyama, kwa kitaalamu LoRaWAN na hutumia teknolojia ya VHF.

Mwakilishi wa FZS nchini Tanzania Gerald Bigurube alisema kuwafuatilia faru mara kwa mara kutawahakikishia usalama wao na kupunguza ujangili.

Alisema mpango huo ni wa kipekee Afrika.

"Shughuli hii inaendelea ndani ya Mbuga ya Taifa ya Serengeti. Lengo ni wafuatilia faru na pia kujua hali yao ya kiafya," alisema, kwa mujbiu wa shirika la habari la Xinhua.

Huwezi kusikiliza tena
Fausta: Faru mzee zaidi duniani anayeishi Tanzania

Baadhi ya maafisa wa wanyamapori Tanzania wamepelekwa Uholanzi kwa mafunzo zaidi kuhusu utenda kazi wa kifaa hicho.

LoRaWAN ni kifaa kidogo sana chenye uwezo mkubwa ambayo huwekwa kwenye pembe za faru.

Kimeundwa kufanya kazi kwa karibu njia sawa na kifaa cha GPS lakini huhifadhi kawi vyema zaidi, jambo ambalo linahakikisha kinaendelea kufanya kazi kwa muda mrefu bila kuwasumbua faru.

Kwa mujibu wa Bw Bigurube, ndege zisizo na rubani pamoja na helikopta zitatumiwa pia kuwalinda faru.

Mtafiti mkuu wa Tawiri Dkt Edward Kohi alinukuliwa na gazeti la The Citizen akisema teknolojia hiyo inafaa sana katika kuwalinda wanyama walio hatarini wakiwemo faru na tembo na imefanikiwa sana maeneo mengine duniani.

Mada zinazohusiana