Noura Hussein anasubiri miujiza kuepuka kunyongwa Sudan

picha

Noura alizidiwa na machozi alipomuona mamake mapema mwezi huu. Ni ziara ya kwanza ya familia yake kwake tangu alipotiwa kizuizini mwaka mmoja uliopita.

Akidondokwa na machozi, alimfafanulia mamake kuwa alipanga kujiua baada ya kubakwa na mumewe.

"Aliichukia nafsi yake baada ya kubakwa," alisema mamake Noura, Zainab Ahmed.

"Aliandaa kisu tayari kujiua iwapo mumewe angemgusa tena."

Na muda ulipowadia - mumewe alipomgusa Noura kwa mara nyingine, alimshambulia.

Mamake anashikilia mwanawe alikuwa akijikinga.

Noura alipohukumiwa mwezi mmoja uliopita, kampeni za kumtetea #JusticeforNoura zilianzishwa mtandaoni na kuenea duniani kote.

Mwanamitindo maarufu Naomi Campbell na muigizaji Emma Watson ni baadhi ya watu tajika walioungana na wanaharakati kushutumu hukumu hiyo ya kifo wakitaka iondolewe.

Na shirika la kuetea haki la Amnesty International lilipowahimiza wafuasi wake kumuandikia waziri wa haki wa Sudan barua pepe ili aingilie kati, Waziri alilazimika kuwa na anwani mpya ya barua pepe kutokana na idadi kubwa ya barua alizopokea.

Na ni pale tu mamake alipomtembelea akiwa gereza la wanawake la Omdurman lililo na hali ngumu ndio Noura aligundua kiwango hiki cha uungwaji mkono duniani.

Kwa sasa, dunia yake imesalia kuwa chumba cha gereza na kuta nne ambapo wafungwa wote wanaishi pamoja.

"Hakuna paa na wanawake hutumia shuka zao kujikinga dhidi ya jua," Mshirika wa Sudan wa shirika la Justice Africa, Hafiz Mohammed, amesema.

Noura amesalia na pingu alizovikwa tangu alipokamatwa.

Ingawa anaonekana kuwa katika hali nzuri ya afya, kwa mujibu wa mamake, anaonekana kuvunjika moyo.

Noura, mwana wa pili kati ya watoto wanane, Noura Hussein, alikuwa katika kijiji cha al-Bager, Kilomita 40km (Maili 25) kusini mwa Khartoum.

Ni eneo lenye vumbi jingi, linalozingirwa na milima midogo ya mawe na mchanga, usiokuwa mbali na Mto Nile.

Matunda na mboga zilizopangwa juu ya vitambara vya kuvutia katika soko la mjini huonyesha rangi za kuvutia na zinazopamba eneo lililo na umaarufu wa kuwa na rangi ya mchanga na ardhi kavu.

Alitaka kuwa wakili

Zainab Ahmed anamsifu bintiye kwa kuwa mtulivu na mwenye akili nyingi.

"Alikuwa na ndoto nyingi," Zainab anasema. "Noura alikuwa na ndoto za kusomea Uwakili katika chuo kikuu na baadaye kuwa mhadhiri."

Familia yake iliondoka eneo la Darfu lililokumbwa na vita na kuhamia al-Bager Noura akiwa mchanga. Familia haikuwa na pesa za kutosha lakini biashara ya babake Noura - duka dogo la kuuza vifaa vya ujenzi na mafuta, ilimaanisha Noura angewewza kupokea elimu bora.

Hili lilimfurahisha Noura.

Lakini 2015, Noura alipokea pendekezo la kuolewa kutoka jamaa wa familia yake mwenye umri wa miaka 32, Abdulrahman Mohamed Hammad. Noura alikuwa na umri wa miaka 16.

Mamake anasema kuwa Noura hakuonekana kuchukukizwa na wazo hilo, lakini aliomba aruhusiwe aendelee na masomo. Alipendekeza pia ndoa hiyo iahirishwe hadi mamake - ambaye alikuwa mja mzito wakati huo - ajifungue.

Lakini presha kutoka familia zikaongezeka - zikiwemo kutoka babake-Hussein.

"Wasichana wengi eneo hilo walikuwa wakipachikwa mimba na kupata watoto nje ya ndoa," anasema Hussein.

Hussein anaongeza kuwa hakutaka Noura naye akutwe na hali hiyo na asalie bila mume.

Licha ya kushiriki kwenye sherehe ya awali ya ndoa, ilibainika wazi kuwa Noura alikuwa anapinga wazo hilo.

Alitoroka hadi kwa shangaziye mji wa Sinnar, ulioko kilomita 350 na kusalia naye kwa siku mbili.

Alishawishiwa arejee nyumbani akifahamu kuwa ndoa hiyo haitakamilishwa.

Ndoa yake

Hata hivyo, alipofika tu, sherehe ilikuwa imekamilika. Lakini hakuhitajika kuishi na mumewe. Miaka miwili iliyofuata aliishi na familia yake.

Abdulrahman alipomtembelea ,alikuwa akimueleza wazi hakutaka kufunga ndoa naye.

Licha ya hayo, wazee wa familia walianza kusisitiza Noura na mumewe wahalalishe uhusiano wao na kuishi kama wanandoa.

Kulingana na mila yao, sauti ya wazee zilisikika na ndio waamuzi wa masuala muhimu.

Heshima na taji la familia ni mojawapo ya masuala muhimu kwenye tamaduni zao.

Babake Noura, Hussein anasema hakuona sababu ya bintiye kukataa uhusiano huo.

Familia ilikuwa na subra kwa miaka kadhaa.

Kwa lazima, Noura alikubali kuishi na Abdulrahman mwezi Aprili 2017.

Kulingana na taarifa zilizotibitishwa na CNN, Noura anasema kuwa alikataa kushiriki tendo la ndoa na mumewe wiki ya kwanza.

Alilia. Alikataa kula. Abdulrahman alipolala, alijaribu kuondoka chumbani, lakini ilifungwa.

Siku ya tisa, Abdulrahman aliwasili chumbani pamoja na jamaa wa familia waliorarua vazi lake na kumzuia sakafuni huku mume huyo akimbaka.

Kulingana na ripoti hiyo ya CNN.

Siku iliyofuata, Abdulrahman alijaribu tena. Awamu hii Noura alichukua kisu alichomweleza mamake kuwa angekitumia kujiondoa uhai.

Kulingana na Noura ni katika makabiliano yake na mumewe ndio mkono wake ulikatwa na Abdulrahman alimuuma begani.

Noura alitumia kisu alichokuwa nacho kumdunga mumewe

Noura alitoroka hadi kwa wazazi wake akiwa na kisu kilichojaa damu.

Hussein na mkewe walishtuka walipomwona mwanao usoni mwao akishikilia kifaa kilichotekeleza mauaji.

"Nimemuua mume wangu aliponibaka," aliwaeleza, huku akishikilia kisu hicho.

"Ndipo niligundua jinsi hali ilivyokuwa," amefunguka Hussein.

Kutokana na ufahamu wake wa familia ya Abdulrahman, hakuwa na shaka wangetaka kulipiza kisasi.

Familia nzima ya Noura ilikuwa hatarini, anasema, kwa hivyo alichukua uamuzi wa kuwapeleka wote hadi kituo cha polisi kwa usalama wao.

Anafafanua kuwa alifanya hivyo kwa maslahi yao, tofauti na madai kuwa alipanga kumtelekeza Noura huko.

Lakini Noura alikamatwa na kuhukumiwa kwa mauaji ya kupangwa.

Wazazi wake walirudi nyumbani wakitaka kufanya mazungumzo na wazee ili wawasaidie kufanya makubaliano na familia ya Abdulrahman.

Walipinga, wakisisitiza Hussein na Zainab wasimtembelee Noura iwapo wangetaka kuwalinda watoto wao.

Pindi makazi na biashara yao zilipoteketezwa, Hussein na Zainab waliitikia wito huo.

Lakini, vitisho vilipozidi Hussein na Zainab waliwachukua wanao na kukimbia.

Mahakama moja ya Omdurman, mji mkuu wa pili wa Sudan, baadaye ilimpata Noura na hatia ya mauaji ya kupangwa.

Na mwezi uliopita, familia ya mumewe ilipokataa fidia, mahakama hiyo ilifanya uamuzi huo rasmi.

Mawakili wa Noura wamekata rufaa dhidi ya hukumu hiyo na wanasaka ahurumiwe.

Majibu yanatarajiwa ndani ya siku kadhaa.

Hussein anasema hajakutana na bintiye tangu usiku huo kutokana na viwango vya vitisho vya kumjeruhi yeye na wanawe iwapo ataonana na bintiye.

"Mimi pia nataka kumuona binti yangu na kumtembelea gerezani kumpa motisha, lakini siwezi," amemaliza.

Hata hivyo amewasiliana naye kupitia njia ya simu na amemuhakikishia yuko katika hali nzuri ya afya.

Zainab Ahmed anatumaini kutakuwa na muujiza kwa bintiye.

Haki miliki ya picha Getty Images

Anahisi kuna uwezekano wazee wa familia wataingilia kati na kuishawishi familia ya Abdulrahman kuiuliza mahakama kubadili hukumu ya kifo iliyotoa.

Amnesty International inafikiri ni matumaini duni.

"Kwa wakati huu, hili linaonekana kutowezekana. Wangefanya hivi wakati uamuzi ukitolewa, wangeomba kupunguzwa kwa adhabu.

Kwa sasa, familia haina ushawishi wowote kwenye uamuzi wa mahakama. "Ameeleza Dkt. Joan Nyanyuki, mkurugenzi wa Amnesty, Afrika Mashariki.

Aidha, presha za kimataifa huenda zikafaulu, ameongeza.

"Tulipowaambia watu wamuandikie waziri wa sheria wa Sudan wakiitisha Noura asamehewe, alilazimika kufunga anwani yake ya barua pepe ndani ya majuma mawili. Ilikuwa na mchango mkubwa. Iwapo watu wangeandika barua pepe kwa ubalozi wa Sudan katika mataifa yao wakitaka aachiliwe, hilo pia lingekuwa na mchango mkubwa."

Ameongeza kuwa: "Kuna mamia ya watu kama Noura ambao hatujasikia kuwahusu, kwenye ndoa ya lazima wakibakwa. Vita hivi ni kwa ajili yao pia."

Wazazi wa Noura sasa wanaishi katika kijiji mbali na al-Bager.

Wanafunguka kuwa ndoa yao ni dhabiti na wanasaidia pamoja na watoto wao ndani ya hali hiyo ngumu. Kilichomkuta Noura bado kinawakanganya.

"Hakuna anayetaka maisha magumu kwa bintiye," Amesema Hussein.

"Sikutarajia mambo yatafika hadi kiwango hiki. Tuna matumaini Mungu atamuokoa."

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii