Kombe la Dunia 2018: Kipa El Hadary aweka historia, aomba radhi baada ya Misri kushindwa tena

Essam El Hadary

Chanzo cha picha, Reuters

Mlinda lango wa Misri Essam El Hadary ambaye ameweka historia ya kuwa mtu wa umri wa juu zaidi kucheza fainali za Kombe la Dunia ameomba radhi baada ya Misri kushindwa tena Kombe la Dunia.

EL Hadary alifanikiwa kuokoa mkwaju wa penalti lakini hilo halikutosha kuzuia Misri kufungwa 2-1 na Saudi Arabia ambao walikuwa wamechapwa 5-0 na Urusi mechi ya ufunguzi.

El Hadary alikomboa mkwaju wa Fahad Al Muwallad kipindi cha kwanza lakini Salem Al Dawsari alifunga dhidi ya Saudi Arabia dakika za mwisho mwisho za mechi Jumatatu.

Kipa huyo alicheza akiwa na miaka 45 na siku 161 na kumfanya kuwa mchezaji mkongwe zaidi kuwahi kucheza Kombe la Dunia.

"Nawaomba radhi kwa watu wa Misri kwa niaba yangu, na kwa niaba ya wenzangu, baada ya kushindwa mara tatu," amesema.

"Najionea fahari yale ambayo nimetimiza na ufanisi huu ni wa thamani kwa Misri.

"Tulijaribu lakini bahati yetu haikusimama - hii ni soka."

Katika mechi hiyo ya mwisho ya Kombe la Dunia kwa Misri, ambao walikuwa wakishiriki michuano hiyo mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 28, Misri waliongoza kupitia bao la nyota wa Liverpool Mohamed Salah dakika ya 22.

Lilikuwa bao la kwanza kwa Misri kupitia uchezaji wa kawaida (si kupitia penalti) katika Kombe la Dunia tangu 1934.

Lakini Salman Al Faraj aliwafungia Saudi Arabia penalti sekunde chache kabla ya muda wa mapumziko baada ya El Hadary kukomboa mkwaju wa Al Muwallad.

Al Dawsari alifunga bao la ushindi sekunde chache kabla ya mechi kumalizika na kuwazawadi Saudi Arabia ushindi wao wa kwanza Kombe la Dunia tangu 1994.

Kocha wa Misri Hector Cuper anasema anatumai "kila mtu Misri anafurahia" kwamba El Hadary alivunja rekodi iliyowekwa na kipa wa Colombia Faryd Mondragon, aliyekuwa na miaka 43 na siku tatu alipocheza katika michuano ya Kombe la Dunia Brazil mwaka 2014.

"Hakuna tofauti kubwa sana kati ya walinda lango wetu watatu lakini alifaa zaidi kucheza leo," alisema Cuper.

Aidha, alipuuzilia mbali tetesi kwamba Mo Salah anafikiria kustaafu kutoka kwenye timu ya taifa kwa sababu hajafurahishwa na kutumiwa sana kwa sababu za kuitangaza timu.

"Sifikiri kuna ukweli wowote hapo. Anafurahia sana fursa yoyote anayoipata ya kuichezea timu ya taifa," amesisitiza kocha huyo.

Egypt walimaliza wakiwa wanashika mkia Kundi A baada ya kushinda kupata hata angalau alama moja. Walishindwa na Urusi, Uruguay na Saudi Arabia.