Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte asema Mungu ni 'mpumbavu'

Rodrigo Duterte

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Duterte anafahamika kwa kutamka maneno ya kuzua ubishi

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amemwita Mungu "mpumbavu", hatua ambayo imekera sana watu katika taifa hilo lenye Wakatoliki wengi.

Kiongozi huyo amesema hayo kwenye hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga.

Aidha, amekosoa vikali hadithi ya Adam na Hawa kuhusu jinsi walivyotenda dhambi na kuondolewa kutoka kwenye neema ya Mungu.

Kadhalika, amekosoa wazo kwamba kila binadamu tangu wakati huo huzaliwa akiwa na dhambi asilia.

Bw Duterte anajulikana sana kwa matamko yake yenye kuzua utata pamoja na matusi yenye kutumia lugha kali dhidi ya wapinzani wake.

Ingawa kanisa na raia wamemshutumu kwa hilo, afisi ya rais huyo imesema alikuwa tu anaeleza imani yake binafsi.

Rais huyo amewahi kumshutumu pia Papa kwa kutumia maneneo makali na ana historia pia ya kuwatusi viongozi wengine.

Tamko la sasa alilitoa katika hotuba mji wa Davao, mji ambao alikuwa kiongozi wake kabla ya kuwania urais.

Huku akiuliza "Ni Mungu yupi huyu mpumbavu?", Bw Duterte amekosoa hadithi ya Biblia kuhusu kuumbwa kwa dunia na binadamu na kufukuzwa kwa Adam na Hawa kutoka Shamba la Eden baada ya kula "tunda walilokatazwa".

"Uliumba kitu kisicho na doa na kisha ukafikiria tukio la kuweka uumbaji wako kwenye vishawishi na kuharibu ubora wa kazi yako," amesema.

Rais huyo ameshutumu pia wazo kwamba kila mtu sasa huzaliwa akiwa na dhambi kutokana na kosa hilo la Adam na Hawa, kwa kusema: "Haukuwa umezaliwa, lakini sasa una dhambi asilia."

"Ni dini ya aina gani hii? Siwezi kuikubali."

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Kanisa Katoliki limetaja maneno hayo ya bw Duterte kama 'kufuru'

Askofu wa kanisa Katoliki eneo hilo Arturo Bastes amejibu kwa kumweleza rais huyo kama "mwenda wazimu" na kutoa wito kwa watu kumuombea kwa sababu ya "maneno yake ya kufuru na tabia za kidikteta."

Bw Duterte anajulikana wazi kwa kuwa mpinzani wa Kanisa Katoliki ingawa taifa lake asilimia 90 ya raia wake ni Wakristo na wengi wao Wakatoliki.

Tamko lake kwa hivyo lilitarajiwa kuzua mjadala mkali mitandaoni.

Msemaji wa rais Harry Roque amemtetea Duterte na kusema amekuwa tu akielezea imani yake.

Amefafanua kwamba pengine rais huyo amesema hayo kutokana na hali kwamba alidhalilishwa na kasisi wa kanisa Katoliki wakati wa utoto wake.

Rodrigo Duterte aliingia madarakani Julai 2016 kwa msimamo wake mkali wa kukabiliana na uhalifu na dawa za kulevya.

Ameongoza kampeni katili ya kuwaua walanguzi na wanaotumia mihadarati, ambayo imeshutumiwa vikali na watetezi wa haki za kibinadamu.

Mapema mwaka huu, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilianzisha uchunguzi kuhusu makosa yaliyotendwa wakati wa vita hivyo dhidi ya mihadarati.

Mwaka 2017, Duterte alikiri kwamba alimuua mtu kwa kumdunga kisu alipokuwa kijana mdogo.

Rekodi ya shutuma na ubishi

Mwaka 2016, alimtusi Obama na kusema hangekubali ukosoaji wa Bw Obama kuhusu vita dhidi ya mihadarati iwapo hilo lingeibuka katika mkutano wao uliokuwa umepangwa.

"Lazima uwe na heshima. Si kurusha tu maswali na taarifa. Mwana wa kahaba, nitakutusi katika mkutano huo," Bw Duterte alisema, akionekana wazi kumrejelea Bw Obama.

Baadaye alisema alijutia matamshi hayo. Mkutano huo ulifutwa.

Baadaye tena, alimtusi Obama na kushutumu Muungano wa Ulaya.

Kiongozi huyo alisema Bw Obama anaweza "kwenda jehanamu".

Umoja wa Ulaya, ambao pia umekuwa ukimkosoa Bw Duterte, unaweza "kuchagua kwenda eneo la kutakasia dhambi ndogo, kwa sababu jehanamu kumejaa", amesema.

Alieleza Marekani kama mshirika asiye wa kutegemewa.

"Badala ya kutusaidia, wizara ya mambo ya nje (ya Marekani) ndio wa kwanza kutukosoa, kwa hivyo wanaweza kwenda jehanamu, Bw Obama, unaweza kwenda jehanamu."

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Rais Obama na Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte waangaliana

Baadaye, alitahadharisha kwamba: "Mwishowe huenda, nikiwa bado uongozini, nikajitenga na Marekani. Heri kwenda kwa Urusi au Uchina."

Amekuwa akitetea mauaji ya walanguzi wa mihadarati.

Wakati mmoja, alisema: "Hitler aliwaua Wayahudi milioni tatu ... Kuna waraibu milioni tatu wa mihadarati. Ninaweza kufurahia sana kuwaua."

Alimwita Papa Francis "mwana wa kahaba" (Ufilipino ni taifa lenye Wakatoliki wengi). Amewahi kumtusi pia aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry kwa kumuita "mwendawazimu" na pia alimweleza balozi wa Marekani nchini Ufilipino kama "mpenzi wa jinsia moja ambaye ni mwana wa kahaba".

Aprili 2016 alifanya mzaha na kusema kwamba alipokuwa meya angekuwa mtu wa kwanza kumbaka Mmishenari wa kike kutoka Australia aliyebakwa na kuuawa wakati wa fujo gerezani mwaka 1989.

"Iliniuma sana kwa sababu alibakwa. Jambo moja pekee lakini. Kwamba alikuwa mrembo sana, meya alikuwa kuwa naye kwanza, ni hasara kubwa."

Baadaye aliomba radhi.

Mapema mwaka huu, bw Duterte aliwaambia wanajeshi wa Ufilipino kwamba wanafaa kuwapiga risasi waasi wa kike wa Kikomunisti ukeni.

Wiki chache zilizopita, alimpiga busu hadharani mfanyakazi wa Ufilipino aliyekuwa akifanya kazi nchi za nje wakati wa hafla iliyokuwa inapeperushwa moja kwa moja kupitia runinga.

Unaweza kusoma pia: