Uraibu ni 'ugonjwa' unaotibika kwa kubadili fikra

  • Esther Namuhisa
  • BBC Swahili
Heroine ni miongoni mwa dawa inayotumika zaidi
Maelezo ya picha,

Heroine ni miongoni mwa dawa inayotumika zaidi

Wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya kimataifa ya kupambana na matumizi ya mihadarati, wapo ambao janga hili la dawa za kulevya limewaathiri kiafya, kiuchumi na hata kusababisha vifo.

Alex ambaye kwa sasa ana miezi miwili tangu afike kwenye nyumba ya kurejesha utimamu, anafikiri kwamba wazazi wake wamempeleka hapo baada ya ndugu yake mmoja kufariki kutokana na ulevi wa kupindukia.

Siku moja alikutwa kwenye mfereji akiwa amekufa kwa sababu ya ulevi, alikunywa pombe kupita kiasi.

Tukio la kifo cha ndugu yake liliishtua familia yao, ingawa yeye mwenyewe hakushitushwa mpaka alipofika kwenye 'sober house' ndipo ameanza kutambua tatizo lake japo ni vigumu kukiri kosa.

"Nimeelewa kuwa mraibu huwa haponi ila vilevi ni sawa na mzio, ni sawa na wale watu ambao wakila samaki wanadhurika basi hata sisi tukirudia kwenye pombe au vilevi tunakuwa watu wa ajabu".

"Sikuelewa tatizo langu kwa sababu kila mtu anatumia pombe na niliona kilevi changu kuwa ni halali, sikuona tatizo maana wengi wanatumia na wanalewa sana hata serikali inapata kodi kutokana na uuzwaji wa pombe."

Maelezo ya picha,

Pombe ni dawa ya kulevya

Alex hayuko peke yake, wapo wengi, tatizo lipo katika kutambua kuwa mraibu ni mgonjwa, kwani hili ni jambo geni kwa jamii Watanzania walio wengi.

Henry Rubagumya ni mlezi wa nyumba ya kurejesha utimamu jijini Dar es salaam, anasema hakutegemea kwamba atatumbukia kwenye janga hilo la madawa kwa sababu amekulia kwenye maadili mema na alipata uelewa wa tatizo hilo la madawa kutokana na taaluma yake, ana shahada katika saikolojia.

Maelezo ya picha,

Uraibu ni ugonjwa unaohitaji tiba na tahadhari

"Kwa miaka 12 nimeteseka na uraibu wa madawa ya kulevya, nimefanya majaribio mengi sana ya kutaka kuacha, nilikaa kwenye nyumba za utimamu mara nyingi bila mafanikio."

Henry anasema miaka mitatu nyuma alikata shauri la kutaka kuondokana na adha hiyo na kutaka kusaidia na wengine wenye hali kama yake.

''Niliamini kwamba nikiweza kusimama mimi basi nitaweza kusaidia wengine."

Mtaalamu huyo wa saikolojia anasema kuwa ni wakati muafaka sasa kwa jamii kutafuta ufumbuzi au tiba ya maradhi hayo ya uteja kama ilivyo kwa magonjwa ya saratani, malaria au ugonjwa wa moyo.

Haya ni wakati Umoja wa mataifa umetoa ripoti mpya leo kuwa matumizi ya mihadarati aina ya opioids imeongezeka.

Ripoti hiyo "World Drug Report" imebaini kwamba madawa aina ya opioids yanachangia zaidi ya robo tatu ya vifo vinavyotokana na matumizi ya madawa ya kulevya duniani .

Maelezo ya picha,

Mihadarati inayofanana na bangi

Kuwa mraibu wa dawa za kulevya au vilevi ni maradhi ambayo jamii imefumbia macho, ni ugonjwa wanauonea aibu.

Kemikali yoyote anayoitumia binadamu na kumbadilisha hisia, ni dawa za kulevya. Hata hivyo, ni bahati mbaya kamba watu wengi hawaamini kama ni madawa ingawa huo ndio ukweli wenyewe, pombe nayo ni dawa ya kulevya.

''Tiba ipo pale unapomsaidia mtu kuelewa tatizo lake, kumpa mtu nyenzo ya kukabiliana na changamoto ya maradhi yake kwa kubadili fikra na tabia."

Maradhi ya uteja yapo ya aina mbili, kuna ambao wanapata maradhi haya kwa kurithi na wengine huyapata kutokana na mfumo wao wa maisha(lifestyle).

Aidha aliongeza kuwa jambo la msingi ni mtu mwenyewe kuelewa tatizo au maradhi yanayomkabili.

Changamoto kubwa tunayokutana nayo ni mtazamo wa watu, wengi wamezoea kuwa waraibu wanapona kwa njia ya kupata dawa ya methadoni jambo ambalo ni gumu kufikia malengo, uelewa ndio jambo la msingi kuanza nalo.

Inawezekana kuacha matumizi ya madawa ya kulevya.

Maelezo ya picha,

Fikiri Salum,alitumia na kuuza madawa

Fikiri Salum, kijana wa miaka 31 ana miezi sita tangu ameingia kwenye nyumba hiyo ya kurejesha utimamu.

Anasema alianza kuingia kwenye janga hilo miaka nane iliyopita kwa kuvuta bangi, lakini kadri siku zilivyosonga mbele na ushauri aliopata kutoka kwa marafiki, aliingia kwenye uuzaji wa dawa za kulevya aina ya heroine na cocaine ili atoke kimaisha.

Fikiri anasema amekulia katika mazingira ambayo jirani zake, yaani barazani kwao, tangu mdogo kama miaka saba hivi, aliona wanavuta bangi nje ya nyumba yao.

''Sehemu niliyokuwa naishi ni Manzese, ilikuwa kawaida kuona kila baada ya nyumba mbili watu wanavuta bangi au madawa kwenye karatasi za nailoni zenye rangi ya silva, kuvuta bangi katika maeneo ya Manzese ni jambo la kawaida ingawa hairuhusiwi kisheria," anaeleza Fikiri.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Bangi ni miongoni mwa dawa za kulevya zinazotumika kwa wingi Tanzania

Fikiri alliongeza kuwa alipoanza kutumia dawa za kulevya, ilikuwa siri sana na aliamini kuwa ataweza kulitatua tatizo lake mwenyewe lakini baadaye hali ilivyozidi kuwa mbaya, jamii ilimtenga, jambo lililomuumiza sana, alijiona hana maendeleo akijilinganisha na watu aliosoma nao.

''Sikujua njia ya kuacha, nilijaribu mara nyingi sana, zaidi ya mara 30.

Nilikuwa nina tabia ya kuamka asubuhi najisemea, nimeacha, lakini hata saa tano haifiki ninaanza kuumwa tena na tiba pekee ilikuwa kuvuta unga. Nilikuwa siwezi kufika siku mbili au wiki bila madawa.

Hii ni mara ya kwanza kumaliza miezi 6 bila kuvuta madawa nikiwa uraiani.

Jela ndio mahali pekee palipokuwa pananifanya nishindwe kupata madawa.

Nilifungwa mara nyingi, kuna wakati nilikaa mahabusu miaka miwili, mara nyingine miezi mitatu hadi sita.

Kufungwa kwangu mara kwa mara kulisababishwa na kesi za madawa lakini kila nilipotoka jela nilirudi kwenye madawa."

Maelezo ya picha,

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na madawa ya kulevya pamoja na uhalifu leo inatoa ripoti yake kuhusiana na kiwango cha matumizi ya mihadarati duniani na mbinu za kukabiliana na madawa hayo

Fikiri aliongeza kuwa hata wakati wazazi wake wanampeleka kwenye soba house alidhani kuwa hao watu walikuwa wanataka kuiba tu fedha za wazazi wake .

''Nilikuwa siamini kwenye suala la kutoka kwenye janga la uteja, lakini sasa ninaona kuwa narejea kwenye utimamu wangu na ninaondokana na hali ya uwazimu iliyosababishwa na madawa na naona faraja sasa.

Biashara ya madawa ilikuwa ina vikwazo vingi sana kutoka serikalini na hata kwa matajiri wenyewe.

Natamani sana elimu ya madawa ianze shule ya msingi".''Uzuri ni kuwa tunafundishwa na walimu ambao walipitia hali kama yetu na sasa wako fiti," alisema John.

Wakati Donald mwenye umri wa miaka 35 amekuwa mraibu wa pombe kwa miaka 20, akianza unywaji tangu akiwa sekondari, hakumbuki hata kiwango cha pombe alichokuwa akinywa, anachofahamu ni kwamba kilikuwa kikubwa.

Maelezo ya picha,

Opioids ni mkusanyiko wa madawa yote ya mengine kulevya

Athari ya unywaji wake ulisababisha mke wake na mtoto kukimbia, hakujua kutumia pesa vizuri, alitumia pesa yake yote kwenye pombe na kila alipopata kazi alifukuzwa. Jambo zuri kwake, alikuwa mchoraji kwa hiyo alipata pesa lakini zote ziliishia kwenye ulevi, akilewa hadi kulala nje ya nyumbani kwake.

''Sasa naona nuru na amani na nina imani kuwa nitakuwa mtu safi ambaye jamii itanikubali."

Aina ya dawa za kulevya zinazotumiwa zaidi Tanzania

Dawa za kulevya zinazotumiwa kwa wingi Tanzania ni heroine, bangi, pombe haramu aina ya gongo,vumbi vumbi la cocaine(cocaine residuals) maarufu kama pele, uyoga, ugoro, bangi, kuberi (inafanana na ugoro).

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Bangi ni miongoni mwa dawa za kulevya zinazotumika kwa wingi Tanzania

Vichangamshi

-mirungi/miraha

-Cocaine

Viyeyusho

Petrol

Dawa za kuulia wadudu

Dawa za kutolea rangi kucha

Dawa ya ganzi kama Helium

Vileta njozi

Bangi

Kuberi(inafanana na ugoro)

Uyoga

Maelezo ya picha,

Uyoga pia ni dawa ya kulevya inayotumika Tanzania,glasi inauzwa shiling 1000 ya Tanzania

Vipumbaza

Inapunguza kasi ya ufanyaji kazi

Pombe

Maelezo ya picha,

Ripoti ya dawa zinazonaswa duniani