Mahakama ya juu zaidi Marekani yaidhinisha marufuku ya usafiri ya Trump

Raia wa Yemen waliozuiwa kuingia Marekani kutokana na kusitishwa kwa marufuku hiyo awali walirudi nchini

Chanzo cha picha, EUROPEAN PHOTOPRESS AGENCY

Maelezo ya picha,

Raia wa Yemen waliozuiwa kuingia Marekani kutokana na kusitishwa kwa marufuku hiyo awali walirudi nchini

Mahakama ya juu zaidi Marekani imeidhinisha marufuku ya usafiri ya utawala wa rais Trump inayowalenga raia kutoka nchi kadhaa za Kiislamu.

Mahakama za chini zilitaja marufuku hiyo kwenda kinyume na katiba, lakini mahakama hiyo ya juu zaidi imepindua uamuzi huu kwa ridhaa ya baadhi ya majaji katika tangazo lililotolewa Jumanne.

Marufuku hiyo inawazuia raia kutoka mataifa ya Somalia, Libya, Iran, Syria na Yemen kuingia Marekani.

Kumekuwa na shutuma kali kutoka kwa wakimbizi na mashirika ya kutetea haki za binaadamu dhidi ya marufuku hiyo.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Marufuku ya kwanza ilikabiliwa na shutuma kali na maandamano nchini Marekani

Uamuzi huu una maana gani?

Uamuzi huu umepindua wa awali wa mahakam ndogo uliozuia marufuku hiyo kutekelezwa.

Marufuku hiyo inazuia wahamiaji wengi, wakimbizi na watu walio na viza kutoka mataifa ya kiislamu - Iran, Libya, Somalia, Syria and Yemen - pamoja na Korea kaskazini na Venezuela kuingia Marekani.

Lakini kesi haikuhusisha marufuku dhidi ya Korea kaskazini na Venezuela.

Uamuzi wa leo wa mahakama ya juu zaidi pia unaidhinisha kuwa rais ana haki ya kuidhinisha marufuku ya aina hii - na wenye maoni ya kulipinga hili hawawezi kuzuia uwezo huu.

Marufuku ya Trump inasema nini?

Vipengee muhimu vinasema:

  • Raia wa nchi za Iraq, Syria, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen - hata wenye viza - ni marufuku kuingia Marekani;
  • Marufuku ya muda kwa wakimbizi wote;
  • Kupewa tena kipaumbele kwa msingi wa dini (kwa maana ya Ukristo) katika kuwapa wakimbizi hifadhi;
  • Marufuku kwa wakimbizi wote wa Syria;
  • Kuweka kipimo kwenye jumla ya wakimbizi wanaoingia Marekani kila mwaka kuwa 50,000.

Chanzo cha picha, Reuters

Kwa mujibu wa amri hiyo ya Trump, wakimbizi wote wanaofika mipakani mwa Marekani kwa sababu ya kutoroka vita makwao au sababu yoyote nyengine hawataruhisiwa kuingia nchini na mfumo wa upekuzi na ukaguzi wa kina anaouita "extreme vetting" utaidhinishwa.

Kiongozi huyo anasema mikakati hiyo inalenga kuzuia Waislamu walio na itikadi kali kutoingia kabisa Marekani.

Mataifa ya Iraq na Chad yalijumuishwa kwenye orodha ya awali lakini yameondoloewa.

Kwa wakati mmoja, jimbo la Hawaii liliwasilisha kesi kupinga marufuku hiyo na jaji mmoja alizuia utekelezaji wake.