Mashabiki wa Uswisi wachanga fedha kusaidia kulipa faini ya FIFA

Granit Xhaka (kushoto) na Xherdan Shaqiri

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Granit Xhaka (kushoto) na Xherdan Shaqiri

Mashabiki wa Uswizi wamekusanya pesa kuwalipia faini wachezaji watatu wa timu ya taifa waliotozwa na shirikisho la soka duniani FIFA.

Granit Xhaka, Xherdan Shaqiri na Stephan Lichtsteiner wamechukuliwa hatua na FIFA kutokana na jinsi walivyosherekea ushindi wao dhidi ya Serbia.

Xhaka na Shaqiri wametozwa fainiw ya 10,000 sarafu ya Uswizi au takriban pauni elfu nane huku nahodha Lichtsteiner akitozwa 5,000 sarafu ya Uswizi (au pauni £3,816).

Huenda malipo hayo yakagharamiwa na mashabiki kwani kufikia sasa wamechangisha dola elfu $16,000 lengo likiwa ni kufika dola elfu $25,000 chini ya saa 18.

Wachezaji hao wameadhibiwa kwa kuonyesha ishara ya mkono inayoashiria mwewe kwenye bendera ya Albania.

Maelezo ya picha,

Lichtsteiner pia alifanya ishara hiyo baada ya kufunga goli dhidi ya Serbia

Xhaka na Shaqiri ni wazawa wa Kosovo wenye asili ya Albania, ambapo serikali ya Serbia iliendesha operesheni dhidi ya raia wa Albania kabla ya kuingiliwa kati na wanajeshi wa Nato mnamo 1999.

Harakati hizo za kuchanga pesa zilianzishwa kwani watatu hao "walileta furaha kwa Waswizi na raia wa Albania kote duniani"

Waanzilishi wanasema kuwa iwapo shirikisho la soka la Uswizi litakataa kupokea pesa hizo, watazitoa kwa msaada.