Korosho zazua gumzo Tanzania, kwa nini?

Tanzania Haki miliki ya picha USHIRIKA
Image caption Zao la korosho linazalishwa kwa wingi kusini mwa Tanzania

Mjadala mkali unaendelea nchini Tanzania kuhusu mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2018 /2019 kuhusu zao la korosho. Mapendekezo hayo ni pamoja na kuondolewa kwa ruzuku ya asilimia 65 iliyokuwa inaenda kwenye Mfuko wa Maendeleo wa Korosho na badala yake, iende kwenye mfuko mkuu wa serikali.

"Haya mabadiliko ya sheria ya matumizi ya fedha yaani, Finance Bill, hatuyaungi mkono mpaka pale ambapo bunge litakapofanya uamuzi," hayo ni kwa mujibu wa Nape Nnauye ambaye ni mbunge wa jimbo la Mtama lililopo kusini mwa Tanzania.

Mjadala huo, unaonekana kugusa zaidi hisia za wabunge hasa wa mikoa ya kusini ambao moja kwa moja wametoafikiana na mpango huo. Wakati huo huo, hofu kubwa imetanda miongoni mwa wadau wa kilimo cha korosho.

Mahamud Seleman Lupanda, ni mkulima wa korosho kutoka Mtwara mjini anasema kilio chao haswa ni pembejeo, mara ya kwanza walikuwa wanazipata kwa njia ya ruzuku lakini sasa ruzuku ikiondolewa upatikanaji wa pembejeo utakuwa wa shida sana.

Mkulima huyu aliogeza kusema kuwa kama pembejeo zitapatikana kwa bei nafuu na kuwepo kwa usimamizi mzuri, basi itakuwa sawa lakini usimamizi uliopo sasa sio mzuri.

Kwa sasa wakulima wa korosho wanatumia mfumo wa stakabadhi ghalani na wanasema wanaufurahia na wanaupenda lakini tatizo lipo kwa watendaji.

"Mpaka leo hii sijalipwa kilo 5000 za korosho, wakulima tunalima na hatujapata fedha zetu kwa muda mrefu sasa na hilo ni tatizo sana. Tuna imani hizo korosho zimeshafika kwa wanunuzi na sisi hatupati pesa zetu na tunataka kuanza kuandaa shamba," amefafanua Mohamud.

Salum Muhidin ni msafirishaji na mnunuzi wa korosho katika minada mkoani Mtwara anasema mabadiliko ambayo serikali inataka kuweka yamekuwa na ukakasi .

"Nikiwa mkazi na mzawa wa Mtwara ambapo korosho nyingi zinatoka naelewa kuwa, kama mbolea ya salfa hakuna basi uzalishaji wa korosho utaathirika sana."

Haki miliki ya picha USHIRIKA
Image caption Zao la Korosho limekuwa na matokeo chanya kwa miaka 10

Salum anaendelea kusema kuwa wakulima wamezoea serikali kuchangia nusu asilimia na wao wanalipa inayobaki, lakini kuona kuwa ruzuku inaondolewa kabisa bila maandalizi litaathiri uzalishaji sana.

Wakati hayo yakijiri, imeelezwa kuwa, hali ya upatikanaji wa pembejeo ni mbaya kusini mwa Tanzania hivyo kusababisha ongezeko la bei kwa asilimia 80.

Wakulima hao, ambao wameongea na BBC wamesema, kwa sasa sio rahisi kuonekana kwa athari ya mabadiliko hayo, kwa sababu, msimu wa korosho unaanza mwezi wa 9 mwishoni mpaka mwezi wa pili.

Aidha wadau hao wa korosho wanaona kuwa serikali ilitakiwa kutoa elimu na kuwaandaa kuwa wanatakiwa kununua mwenyewe na hofu kubwa ipo kwa wakulima wadogo.

"Salfa inanunuliwa na matajiri, je mkulima wa kijijini Newala ataweza kununua, yani mkulima ataipata wapi hiyo salfa?" amehoji mfanyabiashara wa korosho kutoka Mtwara.

Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania limedai kuwa hata kwao taarifa hiyo imewashtua lakini ni fundisho ambalo wanapaswa kulisimamia.

Image caption Mtwara wanazalisha zaidi Korosho

Katibu Mtendaji wa Shirikisho hilo la ushirika, Abel Mbepera, anasema tangu wameanza kuhudumia korosho kwa miaka kumi sasa, kuna mafanikio makubwa ambayo yametokea.

"Mwaka 2007/08 ndio ushirika ilianza kazi ya kisimamia korosho na uzalishaji ulikuwa chini ya tani elfu sabini kwa mwaka lakini sasa umepanda mpaka karibu tani laki tatu kwa mwaka na bei ilikuwa shilingi 250 mpaka 500 kwa kilo ila sasa hivi wastani ni shilingi 3000 mpaka 5000 kwa kilo," Mbepera alieleza.

Mbepera alisisitia kuwa kama mabadiliko hayo yataanza basi hayataweza kuathiri kwa kipindi kirefu hata tukiangalia kwa kipindi cha nyuma wakati zao la kahawa limebadilishwa mfumo hali ilikuwa hivyo lakini zao hilo linaweza kujisimamia sasa.

Chama cha ushirika kinadhani kwamba kama wataweza kusimama imara basi wataweza kuondokana na hii changamoto na hakuna haja ya kuwa tegemezi kwa serikali .

"Hilo suala tutalitatua na tumeanza kuleta teknolojia ya kunyunyizia na ushirika itakuwa inaagiza hizo pembejeo nje ya nchi badala ya watu binafsi ambao wanaongeza na faida na hata kuzalisha hiyo salfa.

Kwa takribani miaka 10, korosho imekuwa zao lililoleta matokeo chanya. Mazao yanachelewa kulipwa kwa sababu soko linakuwa gumu. Walikuwa wamezoea kuwauzi watu binafsi kwa kiasi kidogo cha fedha," amesema Mbepera.

Na mtaalamu wa uchumi na biashara nchini Tanzania, Johakim Bonaventure anasema serikali imeamua kutekeleza sera ya kuweza kuhodhi ile kodi ya kuuza nje, mwanzoni ilikuwa inahozi kwa asilimia 35 ya kipato hicho lakini sasa hivi imechukua na ile asilimia 65.

'Ni jambo jema lakini kiuchumi kuna mambo kadhaa ambayo yanaweza kuwa yameandamana nayo na mojawapo ni kupunguza uwezo wa vyombo vinavyosimamia mazao sio korosho pekee yanayolimwa katika baadhi ya maeneo.'

Pia amesema bajeti ya Tanzania bado tegemezi kwa kiasi fulani hivyo haziwezi kupangiliwa, mfano ikitokea janga kubwa la kiafya wakulima wanakuwa sio kipaumbele bali ni matatizo yaliyopo.

Mtaalamu huyo amesema kama zao la korosho likiweza kuathirika basi pato linaweza kuathirika pia.Bado kuna uwezekano wa kukaa chini kuangalia faida na hasara.

Mwaka jana zao la korosho limeweza kuleta mapato makubwa katika taifa na sasa linatangazwa kuanzishwa katika maeneo mengine 17.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii