Rwanda yaunda gari lake la kwanza aina ya Volkswagen

Rais wa Rwanda Paul Kagame Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais wa Rwanda Paul kagame wakati wa uzinduzi wa gari la kwanza lililotengezwa nchini humo.

Rwanda imezundua gari lake la kwanza aina ya Volkswagen lililotengezwa na kiwanda kilichopo nchini humo katika mji mkuu wa Kigali.

Gari hilo aina ya Polo ni la kwanza lililotengezwa katika kiwanda hicho huku kampuni hiyo ya magari ya Ujerumani ikitarajiwa kutengeza magari 5,000 katika awamu ya kwanza ambayo pia itatengeza magari yake aina ya Passat, Tiguan, Amarok na Teramont

Kampuni ya magari ya Volkswagen ambayo ndio kubwa zaidi barani Ulaya, imefanya uwekezaji wa $20m (£15m) nchini Rwanda unaotarajiwa kuajiri watu 1000.

Kampuni hiyo inapanga kuuza magari hayo mbali na kuyatumia kama teksi ambapo wateja watawasilisha maombi ya kutaka huduma hiyo kupitia simu zao.

Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Gari hilo limetengenezewa Kigali

Umiliki wa magari ni wa kiwango cha chini nchini Rwanda. Kuna takriban magari 200,000 ya watu binafsi yaliosajiliwa katika taifa hilo lenye watu milioni 12 kulingana na halmashauri ya kutoza ushuru nchini humo.

Kampuni hiyo ya Ujerumani inapanga kupanua uwekezaji wake katika eneo la Jangwa la sahara baada ya kufungua kiwanda chake nchini Kenya 2016.

''Wengine hawaamini kwamba magari ya Ujerumani yanaweza kutengezwa nchini Rwanda, na leo tayari magari ya kwanza yameanza kuzinduliwa', alisema rais Kagame katika hafla ya kuzinduliwa gari hilo.

''Kiwanda hiki ni mwamko mpya katika safari ya Rwanda ya ukuwaji wa kiuchumi'', aliongezea.

Kagame alitumia hafla hiyo kusisitiza hoja yake kwamba anapendelea vitu vinavyotengezwa nyumbani badala ya vile vinavyoagizwa kutoka mataifa ya kigeni , hoja ya kibishara ambayo imezua utata kati ya Rwanda na Marekani kuhusu nguo za mitumba.

''Rwanda haiwezi kuwa eneo la kutupa magari yaliotumika ama nguo'', alisema.

''Afrika na Rwanda zinahitaji mambo mazuri na hii ni njia mojawapo ya kuonyesha kwamba tuna uwezo'', alisema Kagame.

Mbali na nguo za mitumba , Rwanda imekuwa ikiyatoza ushuru wa juu magari yanayoagizwa kutoka nje tangu 2016, hatua ambayo itaifaidi kampuni ya Volkswagen inayopanga kutengeza magari 5000 kwa mwaka katika kiwanda hicho ikiwemo gari la Polo, lile la Passat na Teramont.

Hatahivyo bei ya $15,000 kwa gari la thamani ya chini zaidi , ni wazi kwamba magari hayo yatakuwa ghali mno kwa raia wengi nchini Rwanda.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii