Watu 10 wa familia moja wapatikana wamenyongwa kwa pamoja Delhi, India

Street scene in the Delhi neighbourhood of Burari on 1 July 2018
Maelezo ya picha,

Wenyeji wa eneo hilo wamevyambia vyombo vya habari kuwa familia hiyo ilikuwa ni yenye furaha na sehemu ya jamii.

Watu 11 wa familia moja wamepatikana wakiwa wamekufa kwenye nyumba iliyo katika mji mkuu wa India Delhi, 10 kati yao wakiwa wananing'inia kutoka kwa dari la nyumba hiyo, kwa mujibu wa polisi.

Mwanamke mmoja aliye na takriban miaka 70 alipatikana kwenye sakafu ya nyumba. Wengi wa wale waliokuwa wamekufa walikuwa wamefungwa macho na mikono nayo ilikuwa imefungwa kwa kamba mgongoni.

Kilichosababisha vifo hivyo hakijulikani na polisi hawajakanusha uwezekano wa kuwepo mauaji.

Lakini pia wametoa taarifa wakisema kuwa wamegundua mambo yasiyoeleweka kwenye familia hiyo.

Taarifa ya polisi inazungumzia karatasi zenye maandishi walizozipata kwenye nyumba hiyo ambazo zinaashiria kufanyika kwa matambiko yanayooonekana kuwa na uhusiano na vifo hivyo.

Bado wanasubiri matokeo ya upasuaji, wakiwahoji majirani na kuchunguza video za CCTV eneo hilo.

Afisa mmoja wa polisi aliiambia AFP kuwa bado ni mapema kujua kile kilichotokea.

Maelezo ya picha,

Gurcharan Singh aligundua miili hiyo alipoenda kununua maziwa

Familia hiyo imeishi wilaya ya Burari mjini Delhi kwa zaidi ya miaka 20, licha ya kwamba wametokea huko Rajasthan. Walikuwa wanamiliki maduka mawili katika ghorofa ya chini katika jengo la ghorofa tatu.

Miili yao iligunduliwa na jirani ambaye alikuwa ameenda kununua maziwa siku ya Jumapili asubuhi.

"Wakati niliingia dukani, milango yote ilikuwa imefunguliwa na miili ya watu wote ilikuwa inaning'inia kutoka darini huku mikono yao ikiwa imefungwa nyuma," Gurcharn Singh aliimbia idhaa ya Kihindi ya BBC.

Waliokufa ni pamoja na ndugu wawili, wake zao na watoto pamoja na ajuza. Mbwa wa familia hiyo alipatikana akiwa hai.

Kugunduliwa kwa miili hiyo kumezua mshangao eneo hilo.

Wenyeji wa eneo hilo wamevyambia vyombo vya habari kuwa familia hiyo ilikuwa ni yenye furaha na walikuwa wanashiriki katika shughuli za kawaida za kijamii na kutangamana na wengine.